Bukobawadau

Beatrice Munyenyezi ahukumiwa kifungo gerezani

Mama mmoja ambaye alidanganya kuhusu majukumu yake katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda, ili kupata hifadhi ya ukimbizi nchini Marekani, amekuhumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani.
Viongozi wa mashtaka wanasema kuwa Beatrice Munyenyezi, 43, ambaye alikwenda nchini Marekani mwaka wa 1998, kwa wakati mmoja alisimamia kituo kimoja cha ukaguzi ambako waathiriwa walichaguliwa ili kwenda kunyongwa.
Mama huyo amepewa kifungo hicho kwa kutoa habari za uongo kwa maafisa wa serikali.
Baada ya kukamilisha hukumu yake, Bi Munyenyezi atarejeshwa nchini Rwanda ambako anatarajiwa kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya halaiki.
Zaidi wa watu laki nane, wengi wao kutoka kwa kabila la Watusti, ambao ndio wachache nchini Rwanda, waliuawa mwaka wa 1994.
Munyenyezi ni mshukiwa wa kwanza kuhukumiwa nchini Marekani kuhusiana na mauaji hayo yaliyotokea nchini Rwanda.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mama huyo alilia mbele ya mahakama, mjini Concord katika jimbo la New Hampshire.
Wakati wa kesi hiyo, Jaji Judge Stephen McAuliffe alisema Munyenyezi alikuwa amepata uraia wa Marekani kwa njia ya ulaghai na udanganyifu.
Baada ya mauaji hayo kumalizika, alitorokea nchini Kenya ambako alifanikiwa kupata watoto wawili.
Baaadaye alikwenda nchini Marekani kama mkimbizi na alipata makao katika jimbo la Kaskazini Mashariki la New Hampshire, baada ya kusaidiwa na mashirika ya kutoa misaada.
Kisha alijiunga na chuo kikuu huku akifanya kazi katika ofisi moja ya serikali.
Lakini mashahidi waliliambia mahakama hiyo kuwa mama huyo alikuwa kamanda wa kituo kimoja cha ukaguzi mjini Butare Kusini mwa Rwanda, ambako Watutsi wengi waliuawa.
Mawakili wake wanasema wanapanga kukata rufaa.
Mume wake Arsene Shalom Ntahobali na mamake wanatumikia kifungo cha maisha nchini Rwanda baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda.
Next Post Previous Post
Bukobawadau