MBUNGE ASIYEKAA JIMBONI AONGOLEWE
Kipengele kilichomo ndani ya Rasimu ya katiba kinacholezea kuwa wananchi watakuwa na haki ya kumwondoa mbunge wao madarakani endapo ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu za msingi kimeleta mvutano miongoni wa wajumbe wa mabaraza ya katiba wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini.
Mvutano huo ulijitokeza baada ya kundi lililopewa kazi ya kuchambua na kujadili eneo la maadili kuhusu utambulisho wa bunge la jamhuri ya Muungano kuwasilisha maoni yao ya kukubaliana na kipendele hicho kilichopo katika ibara ya 124 cha haki ya wapiga kura kumwajibisha mbunge.
Aliyezusha mvutano huo ni Diwani wa Kata ya Mnyuzi, Muhidini Rajabu ambaye alisema haafiki kipengele hicho kuwepo kwa sababu wapiga kura wanaweza kutumia fimbo hiyo kumwajibisha hata mbunge mzuri lakini kutokana tu na fitna zitakazojengwa dhidi yake.
Mjumbe huyo alisema kipengele hiki katika siku za usoni kitaleta mzigo kwa Taifa wa kugharimia chaguzi ambazo zisingekuwa na lazima ana akataka kiondolewe.
Hata hivyo wajumbe waliokuwa katika kundi lililounga mkono kipengele hicho waliweza kutetea na kusema kuwa kinastahili kuwepo ili kujenga heshima na uwajibikaji wa wabunge kwa wapiga kura wao.
Aliyemaliza mvutano huo ni mjumbe kutoka kata ya Mashewa, Nicholas Kingazi ambaye alisema hakuna haja ya kukipinga kipengele hicho kwa sababu miongoni mwa waliopendekeza kiwemo wakati Tume ya mabadiliko ya Katiba ilipowasili kuchukua maoni ya wananchi kwa awamu ya kwanza ni wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini.
Wananchi wanaweza kumwajibisha mbunge iwapo hataunga mkono sera yenye maslahi kwao na taifa.