HABARI KAMILI MABASI YALIYOTEKWA BUKOBA
• Yapora bunduki za polisi, abiria
Na Ashura , Kagera
MAJAMBAZI wapatao 10 waliokuwa na silaha za kivita aina ya SMG 6 na LMG 2 wameteka magari mbalimbali yakiwamo mabasi mawili ya abiria na kupora bunduki ya Jeshi la Polisi aina ya SMG katika pori la Hifadhi ya Biharamulo mkoani Kagera.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, alisema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 2:30 asubuhi katika Kijiji cha Kasindaga, eneo lijulikanalo kama Mlima wa Simba kwenye pori la Hifadhi ya Biharamulo.
Majambazi hao licha ya kupora bidhaa mbalimbali za abiria, walimpiga risasi na kumjeruhi vibaya shingoni abiria mmoja aliyefahamika kwa jina la Frederick Rugahiula (47) mkazi wa Bukoba, mkoani Kagera.
Kamanda Kalangi alitaja mabasi ya abiria yaliyotekwa kuwa ni RS, lenye namba za usajili T 495 AGT, lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea jijini Dar es Salaam na NBS T 644 BUR, lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea Arusha.
Alisema baada ya kuteka mabasi hayo majambazi hao wanaoshukiwa kuwa ni raia wa nchi moja jirani kutokana na lafudhi ya maneno waliyokuwa wakiongea, waliwashusha abiria na kuwapora simu za mikononi pamoja na fedha taslimu. Pia walipora bunduki ya Jeshi la Polisi aina ya SMG yenye namba 14302551 iliyokuwa mikononi mwa polisi.
Alisema wakati wakiwa katika harakati za kuwapora abiria, askari polisi waliokuwa katika basi la Mohammed Trans lililokuwa nyuma ya mabasi hayo, waligundua kuwa wenzao wametekwa, ndipo walipoanza kuwashambulia majambazi hao na kuzuka majibizano makali ya risasi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa askari polisi wapatao wanne waliokuwa wakisindikiza mabasi hayo walizidiwa nguvu kutokana na uchache wao, hivyo wakaamuru kugeuza basi hilo na kukimbia kwa ajili ya kutafuta msaada zaidi.
Akielezea tukio hilo lilivyotokea, Kamanda Kalangi alisema, kwanza majambazi hayo yaliteka gari dogo na kuzuia njia kana kwamba limeharibika, hivyo mabasi yalipofika yalilazimika kusimama na ndipo yalipotekwa.
Hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kuwa msako mkali unaendelea kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori katika eneo la Hifadhi ya Burigi na pori la Biharamulo.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana na matukio ya uhalifu, kwa kuzingatia kuwa watendaji wake ni wachache na maeneo ni makubwa.
Hata hivyo alisema kuwa Mkoa wa Kagera unaathirika zaidi na wageni wanaotoka nchi jirani zilizokuwa katika vita, wanaoingiza silaha ambazo zinatumiwa na majambazi kwenye matukio ya uhalifu.