Bukobawadau

‘Hivi ndivyo polisi walivyomuua baba’ -

KIFO cha marehemu, Selemani Mwinyimsanga, anayedaiwa kuuawa na askari polisi wa Kituo cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam, kinaendelea kuibua mapya. Mtoto wa marehemu huyo, Geofrey Banzi (19), ambaye alishuhudia polisi wakimpa kipigo baba yake, aliiambia MTANZANIA katika mahojiano maalumu jana, kwamba hata kama Jeshi la Polisi litakana kuhusika na kifo hicho, ukweli utaendelea kuwa ni ule ule, kwamba kifo cha baba yake kilisababishwa na kipigo cha polisi.

Wakati marehemu baba yake akipigwa wakiwa nyumbani kwao Kurasini, Banzi alisema alikuwapo pia Mjumbe wa Nyumba Kumi aliyemtaja kwa jina moja la Boni. “Nakumbuka ilikuwa ni Ijumaa ya Julai 19 mwaka huu, saa tisa mchana ukiwa ni muda mfupi baada ya kutoka shule, nilisikia watu nje wakiuliza kwa wapangaji wenzetu, chumba cha baba Jasmini kiko wapi?

“Walipoonyeshwa nikaona askari wawili wa kike wanaingia ndani kwetu, wakati huo nilikuwa nacheza ‘game’ kwenye TV.

“Walipofika waliniuliza uhusiano wangu na baba Jasmini, niliwajibu ni baba yangu wa kufikia, wakaniuliza mama yangu yuko wapi, nikawaambia amekwenda Kigogo kwenye msiba, wakaniambia nimpigie simu nimwambie nyumbani kuna wageni.

“Nilimbip mama kwa sababu sikuwa na salio na wakati huo askari wakinisisitiza nimwambie arudi haraka nyumbani,” alisema Geofrey.

Aliendelea kusema kuwa, baadaye askari hao walimuamuru atoe vitu vyote vilivyokuwa juu ya meza ikiwamo chupa ya chai, kikombe na sukari na kuvipeleka chumbani.

Baada ya kufanya hayo, alisema alitoka nje kisha akawaona askari wa kiume wapatao watano hivi wakiwa wamembeba baba yake kwa kushirikiana.

“Wengine walimshika miguuni, wengine sehemu ya kiuno na kichwani, wakamuingiza ndani, huku akiwa amefungwa pingu mkononi na kumkalisha chini.

“Askari mmoja wa kike alikwenda uani kwetu na kuchukua ufagio mrefu wa nje akauvunja, akarudi nao ndani na kuanza kumpiga baba kabla ya kuanza upekuzi.

“Baba alilia sana, akawa ananiomba msaada, lakini askari huyo aliendelea kumpiga sehemu mbalimbali za mwili, hasa tumboni na kwenye mikono.

“Wakati wanaendelea kumpiga, nilisikia uchungu sana, nikaona siwezi kuvumilia kuendelea kuangalia tukio hilo na nilipotaka kutoka nje, askari walinizuia na kunikalisha chini huku upekuzi ukiendelea chini ya mjumbe wa nyumba kumi.

“Kwa bahati nzuri hawakupata kitu na hakuna kitu chochote walichokichukua, lakini walitusainisha nyaraka fulani mimi na mjumbe wa nyumba kumi.

“Wakati wanataka kuondoka, nilisikia wakimwambia baba atajuta huko mbele ya safari. Walimtoa ndani na kumuweka kwenye korido na kumwamuru asimame, atembee hadi kwenye gari lao, baba alishindwa kwa sababu ya maumivu ya miguu, inaelekea miguu yake ilikuwa imevunjika,” alisema kijana huyo.

Alisema kwamba, marehemu aliposhindwa kutembea, askari hao walimburuza hadi kwenye gari lao na kuondoka naye.
Mke wa marehemu
Mke wa marehemu, Honoratha Gido, ambaye ameachwa na mtoto mchanga mwenye umri wa miezi mitano, alisema anahisi anaweza kuwa na mwisho mbaya kwa kuwa anatafutwa na polisi.

“Hapa nilipo sijui nitaishije, nasikia na mimi ninatafutwa, sijui wakinikamata na mimi wataniua au vipi,” alisema mama huyo na kutoa machozi.

Alieleza kuwa, kitendo alichofanyiwa mumewe ni cha kinyama, kwa sababu amefia mikononi mwao.

“Hata kama mume wangu alikuwa jambazi kama polisi walivyodai, sheria ingechukua mkondo wake badala ya kumuua kikatili,” alisema Honoratha.

Akizungumza kwa uchungu, alisema aliishi na marehemu kwa miaka mitano, lakini hajawahi kuhisi kama mumewe alikuwa jambazi.

“Mume wangu alikuwa anauza vitenge kwa miaka mingi, alikuwa akinunua robota zima na kuwapa vijana wanatembeza na jioni wanamletea hesabu.

“Tuliendelea hivyo, mtaji ulipokua, tukafungua genge kubwa lililofanana na duka, tulikuwa tunauza vitu mbalimbali ukiwamo unga na mafuta ya taa.

“Marehemu mume wangu alipoona biashara hiyo imechanganya, alinunua pikipiki ambayo aliifanya bodaboda, alimkabidhi kijana mmoja wa Kigogo ambaye alikuwa akituletea fedha kila wiki.

“Pikipiki hiyo iliibiwa wakati mume wangu akiwa kijijini Tununguo kule Morogoro kumuuguza baba yake.

“Baadaye mtaji wetu uliyumba na hilo genge tukafunga. Mume wangu aliendelea na biashara ya vitenge ambayo aliizoea, alikuwa akikopesha watu mbalimbali ambao mimi siwafahamu.

“Kwa maana hiyo, nachukua nafasi hii kuwaomba waliokuwa wanadaiwa na marehemu, wanipatie fedha hizo ili niweze kujikimu na mtoto huyu mchanga,” alisema Honoratha.

Marehemu Mwinyimsanga aliuawa hivi karibuni kutokana na kinachodaiwa kuwa ni kipigo cha askari polisi wa Kituo cha Oysterbay.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camilus Wambura, alisema marehemu ambaye alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za ujambazi, hakuuawa kwa kipigo cha polisi bali alifariki baada ya kupigwa na wananchi wakati alipokuwa akiwakimbia polisi waliotaka kumkamata.
via mtanzania
Next Post Previous Post
Bukobawadau