Bukobawadau

Mahakama yawatema makada Chadema

 MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, imesema haina uwezo wa kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Makada hao wanakabiliwa na shitaka la ugaidi, ambapo Juni 24, mwaka huu, waliachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Igunga, kisha na wakakamatwa kwa tuhuma za kummwagia tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, Mkoa wa Tabora, uliofanyika mwaka 2011.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa ni Evodius Justunian (30), mkazi wa Bukoba, Oscar Kaijage, mkazi wa Shinyanga, Seif Magesa wa jijini Mwanza na Rajabu Daniel, mkazi wa Dodoma.

Watuhumiwa hao, walipokamatwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga, kabla ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo kukamatwa na kuunganishwa kwenye kesi hiyo.


Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, Issa Magoli, alisema mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa kusikiliza shauri hilo ambapo aliliahirisha hadi Julai 22, mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Magoli, aliwashauri mawakili wa upande wa utetezi, kuwasilisha hoja zao Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuwa huko ndiko kunakoweza kupatiwa ufumbuzi wa kisheria wa shauri hilo.

Katika shauri hilo, washitakiwa hao walifunguliwa kesi mbili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, baada ya kesi ya awali ya kudhuru mwili kwa tindikali kufutwa na kufunguliwa kesi ya ugaidi dhidi ya makada hao wa Chadema.

Awali, katika shauri hilo yalizuka mabishano ya kisheria kati ya mawakili wa upande wa utetezi, wakiongozwa na Peter Kibata na Profesa Safari, huku upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili Juma Masanja na Edifonce Mkandala.

Wakati wa mabishano hayo, mawakili wa upande wa utetezi waliomba Mahakama ifute kesi hiyo, kwa kile walichosema kuwa ni batili kutokana na baadhi ya vifungu vya sheria kukiukwa, huku mahakama hiyo ikiwa haina uwezo wa kuisikiliza isipokuwa Mahakama Kuu peke yake.

Mawakili hao walisema kuwa, washitakiwa walikamatwa sehemu tofauti, hivyo kesi zao zilipaswa kusikilizwa katika maeneo waliyokamatiwa badala ya kusikilizwa katika eneo moja.

Ulinzi mahakamani

Kabla ya washtakiwa hao kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi mkoa hapa liliimarisha ulinzi katika eneo la mahakama ambapo ilipotimu saa 4 asubuhi, walifikishwa wakiwa katika gari la Polisi lenye namba za usajili PT 1816, huku wakiongozwa na askari wa kutuliza ghasia FFU
Next Post Previous Post
Bukobawadau