Bukobawadau

Nyumba za nyasi Mtwara kufungwa umeme


SERIKALI imeongeza muda wa mwaka mmoja kwa wakazi wa mikoa miwili ya Mtwara na Lindi, kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu ya Sh 90,000 badala ya Sh 450,000. Chini ya mpango huo, nyumba za nyasi na udongo ni miongoni mwa nyumba zitakazoingizwa katika miradi sita ya kitaifa ya umeme iliyopangwa kutekelezwa kwa miaka mitatu ijayo.

Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo Maalumu cha Kusimamia miradi hiyo (MDU), Wanja Mtawazo wakati akitoa tathmini ya kongamano la wazi la Wizara ya Nishati na Madini lililofanyika wiki iliyopita.

Mtawazo alisema kila mkoa ambao umepitiwa na gridi ya taifa, vijiji 10 vitapatiwa umeme na kuongeza kwamba vijiji vilivyo mbali na gridi hiyo vitapata huduma hiyo inayotokana na jenereta na sola ya jua.

“Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba wale walio na nyumba za nyasi na zile za udongo watapatiwa umeme kwa sababu kuna vifaa maalumu ambavyo vitakuwa vinawekwa na ni rahisi kuvitoa pale hitilafu inapotokea.

“Tulipoamua kupeleka umeme vijijini, tulijua hali ya nyumba zetu ndio maana wataalamu wetu kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wakatengeneza mfumo huu.

“Lakini kikubwa tunachowaomba wasibweteke kupata umeme huo katika nyumba zisizofaa kwa miaka mingi, watumie muda mfupi kuanzisha biashara ili kujenga nyumba imara na za kisasa,” alisema.

Alisema kutokana na Serikali kutoa kipaumbele kwa wananchi wa mikoa hiyo, imeamua kuongeza tena mwaka mmoja hadi Juni 2014 ili wananchi waweze kufaidika na nishati hiyo ambayo waliikosa kwa muda mrefu.

“Tunawaomba wakazi wa mikoa hiyo kutumia nafasi hiyo tena kupata umeme kwa gharama nafuu, kwani awali mtu kupata huduma hiyo alitakiwa kulipa Sh 450,000 lakini gharama hizo Serikali imezibeba.

“Jambo kubwa tunaloliomba kwa wananchi ni ushirikiano kabla ya miradi na baada ya miradi, tunaomba wote tuwe walinzi wa miundombinu itakayojengwa katika maeneo yao.

“Serikali inawapenda wananchi wake kwani hivi sasa imepanga kwamba baada ya mradi wa umeme wa Makambako -Songea kukamilika nyumba 26,000 za wakazi wa mwanzo wataomba huduma hiyo ambayo itakuwa imelipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” alisema.

Kuhusu tathmini ya kongamamo la wazi la wizara hiyo, alisema wamefanikiwa kupata maoni mazuri ya wadau wa sekta hiyo ambayo asilimia kubwa yalifanana na malengo ya Serikali.

Alisema idadi kubwa ya washiriki zaidi 450 iliyojitokeza katika kongamano hilo, imetoa mwanga kwao kwamba wananchi wana kiu kibwa ya kutaka maendeleo ya nishati ya umeme.

Katika kongamano lililofanyika wiki iliyopita, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema muda wa maneno umekwisha na kilichobaki ni vitendo huku akiwataka watumishi wa wizara hiyo kujitathmini kama wanafanya kazi kwa kiwango.

Toa Maoni yako kwa habari hii

Next Post Previous Post
Bukobawadau