Bukobawadau

MBOGORO KAMA KINYONGA KWA KCU(1990)LTD

Na Prudence Karugendo

WAKULIMA wa kahawa wa mkoa wa
Kagera pamoja na wadau wote wa vyama vya ushirika nchini wameonyesha kufarijika
kutokana na uamuzi wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini,
Willigs Mbogoro, wa kuikana kauli yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari
akikisafisha chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha mkoani Kagera.

Kufuatia malalamiko ya
wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wakiutuhumu na kuushutumu uongozi wa chama
chao, kutokana na uongozi huo kufanya kinachojionyesha ni ufisadi uliokithiri
unaotishia kukiangamiza chama hicho, vyombo vya habari viliamua kumwendea
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, kumuuliza
ana kauli gani juu ya kuunusuru ushirika huo kwa kutumia mamlaka
aliyokabidhiwa kiutendaji.

Akizungumza na mwandishi wa
chombo kimojawapo cha habari, Mhandisi Chiza alikiri kuufahamu uchafu wote
uliogeuka uozo ndani ya chama hicho cha KCU (1990) Ltd. pamoja na kutaja
mikakati ambayo ameishaiandaa ya kuushughulikia uozo huo katika jitihada zake
za kuisafisha na kuinusuru KCU (1990) Ltd.

Lakini, wanaushirika wa
KCU (1990) Ltd. wakiwa wamepata faraja kutokana na kauli hiyo ya waziri,
wakiamini kuwa hakuna kubwa linaloishinda serikali, mara yakaanza
kujitokeza majigambo kwa upande wa uongozi wa KCU (1990) Ltd. kwamba hakuna
litakalofanyika kwa vile uongozi huo umeiweka serikali mfukoni mwake!

Wakati wanaushirika wakiwa
wameduwazwa na majigambo hayo yaliyotolewa na uongozi wa chama chao, mara
akajitokeza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC),
Willigs Mbogoro, akaitisha mkutano na wanahabari kwa lengo la “kuifagilia” KCU
(1990) Ltd.!

Mbogoro akawaeleza wanahabari
kwamba katika vyama vyote vya ushirika nchini chama kinachopaswa kutolewa mfano
ni KCU (1990) Ltd.! Akaeleza namna chama hicho kinavyowanufaisha wanachama
wake, na kwenda mbali zaidi akiwaonya wanasiasa na wafanyabiashara kutoingilia
shughuli za ushirika!

Ni katika hatua hiyo
wachambuzi tukaanza kujiuliza inawezekanaje mtendaji huyo mkuu wa vyama vya
ushirika autenganishe ushirika na siasa wakati siasa ndiyo msimamizi na
mwelekezaji wa kila kitu hapa nchini. Tukianza na rais, mkuu wa nchi, ni
mwanasiasa, waziri mkuu ni mwanasiasa, bosi wake Mbogoro, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, ni mwanasiasa. Sasa iweje leo mtu aliye chini ya wanasiasa
atake kuwaruka wakubwa wake hao na kuwaonya wasimuingilie katika shughuli zake?

Kwa upande mwingine wadau wa
ushirika nao walimshangaa Mbogoro alipojaribu kuutenganisha ushirika na
wafanyabiashara. Sababu kimsingi mtazamo wa ushirika ni kupata faida, ambayo ni
kanuni kuu ya biashara. Kwa maana hiyo ushirika ni biashara. Sasa
utawatenganishaje wafanyabiashara na ushirika halafu uendelee kuwa na ushirika ulio
hai?

Kama lengo la ushirika
lingekuwa ni kufanya shughuli zisizozalisha faida, kama
vile kuzikana, kufanyiana matanga au hata kucheza ngoma kwa ajili ya
kuburudishana tu, kauli ya Mbogoro ya kwamba wafanyabiashara wasiingilie
shughuli za ushirika isingekuwa na utata wowote. Utata ulijitokeza baada ya
Mbogoro kutaka kuwatenga wadau ambao ndio mhimili mkuu wa ushirika,
wafanyabiashara.

Na kama wafanyabiashara ni
wadau katika ushirika hakuna namna ambayo unaweza kuwazuia wasiuongelee
ushirika hasa pale wanapoona mabo yanaenda kombo kutokana na kitu
kinachojionyesha wazi kama ufisadi.

Katika kuonyesha jinsi
walivyoguswa na kauli ya Mbogoro, wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wakaeleza
ukaribu alio nao katibu huyo mtendaji wa TFC kwa KCU (1990) Ltd. na kusema kwamba
pengine ndio unaomsukuma kukisafisha chama hicho.

Kumbe Mbogoro ni mjumbe wa
Bodi ya Wakurugenzi wa TANICA, ambayo ni kampuni tanzu ya KCU (1990)
Ltd., ambapo mwenyekiti wa Bodi hiyo ndiye yuleyule mwenyekiti wa Bodi ya
KCU (1990) Ltd..

Kutokana na ukweli huo,
wadau, wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wakasema kwamba kwa mtaji huo Mbogoro
alishapoteza sifa ya kukitokea kauli chama chao kikuu cha ushirika kwa vile
tayari ana mgongano wa maslahi kutokana na yeye kuonekana kama
sehemu ya uongozi unaolalamikiwa na wanaushirika.

Kwahiyo wanaushirika hao
wakawataka wanahabari kumkabili Mbogoro ili akaitolee ufafanuzi kauli yake ya
kwamba KCU (1990) Ltd. ni chama chenye uongozi safi katika medani ya ushirika.
Kufuatia hoja hiyo ya wanaushirika wanahabari wakamfuata Mbogoro ofisini kwake.
Lakini Mbogoro aliyekuwa ofisini kwake akatokea kuwa mtu tofauti na yule
aliyeisafisha KCU (1990) Ltd. kwa wanahabari.

Kwa mujibu wa gazeti la Dira
ya Mtanzania toleo namba 240, la tarehe Juni 24 – 30, Mbogoro akadai kwamba
wanahabari walimnukuu vibaya, na kukiri kwamba KCU (1990) Ltd. ni chama cha
ushirika kilichozungukwa na kuelemewa na ufisadi! Na kuongeza kwamba
zisipofanyika jitihada za haraka, ambazo yeye yuko tayari kushirikiana na
uongozi wa wizara yake kuzifanya, za kuufikisha uongozi wa KCU (1990) Ltd.
mahakamani, basi chama hicho kitakuwa kaburini muda sio mrefu.

Kauli hiyo mbadala ya
mtendaji mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika, kwa mara nyingine tena
imekuwa faraja kwa wanaushirika wa KCU (1990) Ltd.. Wengi wametoa maoni yao wakisema kwamba
kiongozi anapaswa awe namna hiyo, anayeweza kujikosoa na kujirekebisha.

Archard Felician Muhandiki ni
mwakilishi wa chama cha msingi cha Kamachumu, Muleba. Anasema kwamba kama kweli
wanahabari walimnukuu vibaya Mbogoro, au kama yeye alipitiwa akateleza ulimi na
kutoa kauli tata katika mkutano wake wa awali na wanahabari, basi itambidi
aitishe tena mkutano mwingine na wanahabari ili kujisafisha yeye mwenyewe,
mkutano ambao utakuwa unaufuta ule wa kwanza uliokuwa na lengo la kuisafisha
KCU (1990) Ltd. lakini ukaishia kumchafua yeye.
Muhandiki anasema sio rahisi kujisafisha kupitia kwa mtu mmoja mmoja wakati
umejichafua mbele ya hadhara. Kwahiyo anachotakiwa kukifanya Mbogoro ni
kuitisha mkutano wa wanahabari na kuifuta kauli yake ya awali kusudi kila
chombo kilichokuwa katika mkuatano wa awali kiweze kurekebisha kauli hiyo
iliyotolewa mwanzo.

Vilevile wanaushirika wa KCU
(1990) Ltd. wanamkumbusha Waziri Chiza kwa kutumia methali ya Kihaya inayosema
kwamba “ajuna akanyonyi akajuna kakyaharara” ikiwa na maana ya kwamba anayetaka
kumnusuru ndege hufanya hivyo ndege husika akiwa bado ana uwezo wa kuruka, siyo
asubiri kwanza ndege akose uwezo wa kuruka ndipo ajifanye kumsaidia.

Hiyo maana yake ni kwamba kama Chiza amedhamiria kweli kuinusuru KCU (1990) Ltd.
angefanya hivyo bila kusita, kwa wakati huu.
Awachukulie hatua za kisheria mara moja wote wanaohusika na ufisadi katika
chama chao. Eti akisubiri chama kiishiwe na pumzi hatakuwa na jinsi nyingine ya
kuweza kukinusuru.

Vilevile wanaushirika hao
wanamshauri waziri kwamba, katika kulifanikisha hilo, angeagiza
chama hicho kiwe na uongozi wa mpito utakaoandaa utaraibu wa kukipatia uongozi
mpya huku uongozi uliopo kwa sasa ukiwa umesimamishwa ili kuepusha hujuma zinazoweza
kufanywa kwa makusudi na uongozi huo kwa lengo la kukikomoa chama chao na
kutengeneza mazingira mabaya kwa uongozi utakaofuatia kama njia ya kulipiza
kisasi.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau