Bukobawadau

Pinda kachoshwa na mfumo unaomtumikisha , si watu anaowatumikia


Na Prudence Karugendo
DREVA  anayeendesha gari bovu, mara limekata mafuta, mara likose breki, mara gia zikatae kuingia, mara lishindwe kuwaka na kuhitaji kusukumwa, mara halina honi, lakini tajiri mwenye gari akimwambia dreva wake huyo kwamba ni lazima gari liendeshwe hivyohivyo ili likaingize pesa, potelea mbali lenye kuwa na liwe, hawezi kuyasingizia makelele ya abiria wanaohofia usalama wao pale la kuwa linapokuwa limejiri.
Mfano hai ni wa ajali iliyotokea Mjini Bukoba mwaka 1984, iliyolihusisha basi lililokuwa likiitwa Safari Leo. Kabla ya ajali hiyo yalitokea mabishano kati ya dreva na mwenye gari, dreva akisema kwamba gari halina breki kwahiyo abiria wateremkie katika sehemu inayoitwa Kibeta Amjuju, kusudi gari liweze kushusha mteremko mkali wa kuingia Bukoba mjini likiwa tupu bila mzigo.
Mwenye gari hakukubaliana na ushauri huo wa dreva wake, akasema twendeni hivyohivyo! Dreva, maarufu kwa jina la Kyakuboto, akaliwasha gari moto.  Maajabu, kutokana na gari kutokuwa na breki, likawa kama linapaa katika mteremko mkali wa kuingia Bukoba mjini na kwenda kujibamiza kwenye mti mkubwa katika kona ya Nyangoye, nusu ya abiria maisha yao yalizimikia pale akiwemo mwenye gari. Dreva alisalimika!
Isingwezekana hata kidogo dreva Kyakuboto akawalaumu abiria katika ajali ile wala kuwahusisha nayo kwa namna yoyote ile. Tatizo lilitokana na bosi wake kulazimisha mambo yasiyowezekana na yeye, Kyakuboto, kukubali kuyatii wakati akielewa kwamba hayawezekani. Pale ni kwamba Kyakuboto alikuwa amechoshwa na mfumo uliomtumikisha na si abiria aliowatumikia.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba waziri mkuu wa 9 wa Tanzania, Mizengo Kayanza Peter Pinda, kavunja rekodi ya kutoa kauli zenye utata kwa mawaziri wakuu wote waliomtangulia. Nadhani sihitaji kuziorodhesha kauli zake hizo kwa vile naamini kila Mtanzania anazifahamu.
Ila itoshe tu kusema kwamba ni kauli zenye utata uliopindukia, maana ni kauli zinazovunja sheria za nchi, kauli zenye uchochezi, uchonganishi, kufarakanisha jamii nakadhalika. Kibaya zaidi kauli za Pinda zinaonekana kuvunja hata Katiba ya nchi huku zikiwa zimekiuka haki za binadamu wakati mwingine!
Ni wazi kwamba Mheshimiwa Pinda anaonekana kukata tamaa kana kwamba kazi hiyo ya uwaziri mkuu anaifanya kwa kulazimishwa!
Yeye akiwa kiongozi mkuu, baada ya rais na makamu wake, anayepaswa kutumia kila mbinu zilizojaa maarifa na hekima kuhakikisha usalama na amani ya nchi na wananchi vinalindwa, anawezaje kutoa kauli bila kigugumizi kwamba “wao wapigwe tu”? Wao kina nani?
Nani asiyeona kuwa kauli hiyo ni ya kuwatenganisha wananchi na kuwafarakanisha ikiwa imewachochea kuanzisha vurugu iwapo wanaoamriwa kupigwa watasema kwamba hatukubali? Nani asiyeona kuwa Pinda anawachonganisha wananchi na vyombo vyao vya dola kiasi cha kuanza kutazamana kama maadui, kitu ambacho hatukuwa nacho tangu tumejipatia uhuru wetu toka kwa wakoloni?
Kauli za kuwafarakanisha wananchi na kuwachonganisha na vyombo vya dola kwa visingizio vya kuwadhibiti wanaoitwa wapinzani, kana kwamba hao ni maadui kutoka nchi nyingine, kamwe haviwezi kuijenga nchi wala kuuhami utawala unaojishuku kutokupendwa kama wananchi wameishauchoka.
Historia inatukumbusha na kutuonyesha kwamba yanayojitokeza nchini kwa sasa dawa yake pekee ni busara iliyoambatana na hekima. Lakini kauli kama hizi anazozitoa Pinda hazijawahi kuleta ufumbuzi wala kuwa mshindi katika hali ya aina hii.
Tuchukulie mfano wa karibu wa nchi ya Rwanda. Tangu enzi za wakoloni nchi hiyo iliingizwa katika ubatili wa “gawanya utawale”. Lakini ubatili huo haukuwafanya wakoloni waitawale Rwanda milele yote, ulishindwa. Baadaye ubatili huo ukarithiwa na Mfalme Kigeli (V) Ndahindurwa. Hatahivyo haukumsaidia lolote dhidi ya Gregoire Kayibanda aliyekuja kuwa rais wa kwanza wa Rwanda.
Kayibanda, ambaye naye aliuendeleza ubatili huo wa gawanya utawale, akaja kuondolewa madarakani na Habyarimana Juvenal. Lakini naye akaja kuuendeleza ubatili uleule dhidi ya kina Kagame.
Kumbuka ni ubatili huo uliozaa mauaji ya kimbari baada ya ndege ya Habyarimana kuanguka akitokea Dar es salaam kwenye mazungumzo ya upatanishi, mwaka 1994, na kumuua.
Yale magenge ya wafuasi wake aliyokuwa ameyatengeneza ili yakawadhibiti wapinzani wake, katika hali ileile ya kubaguana kwa mtindo wa “piga tu hao” yakaanza kuchinja watu ovyo.
Lakini hatahivyo historia ilikataa kubadili mkondo wake, jamii ya waliochinjwa kwa lengo la kuangamizwa ikaibuka na ushindi na kwa sasa ndiyo imeishikilia nchi hiyo ya Rwanda.
Mfano mwingine wa karibuni ni mtawala wa Libya, Muammar Gaddafi. Mtawala huyo alijaribu kuwachonganisha Walibya akiwa amewatenga wale alioona ni wapinzani wake. Aliwaita wapinzani wake panya na mende na kuapa kuwa angewaangamiza wote. Lakini kinyume chake akaja kuona maajabu, mende wakaangusha kabati! Yeye akageuzwa panya na kisha kukamatiwa kwenye mtaro wa maji machafu na hao mende wake!
Tukirudi kwa Mheshimiwa Pinda, anayedai kachoka, naona yafuatayo. Mimi siamini kama uchovu huo anaouona waziri mkuu unatokana na wananchi, au tuseme wapinzani kama ambavyo angependa ieleweke. Wapinzani hawajafanya lolote la kumchosha Pinda. Maana hawa ni sawa na abiria wanaopiga kelele wakilalamikia mwenendo wa gari lao bovu unaojionyesha kwa kila mmoja  wao huku ukiutishia uhai wao.
Kwahiyo dreva makini hawezi kusingizia kelele za abiria kuwa ndizo zinazompa uchovu. Ni lazima atakuwa anachoshwa na ubovu wa gari analolazimika kuliendesha jinsi lilivyo na ubovu wake.
Anachoweza kukilalamikia Pinda nisitie neno ni mfumo unaotumika kutawala hapa nchini kwa sasa chini ya Chama Cha Mapinduzi. Huu ni mfumo uliochoka kiasi  kwamba unahitaji kupumzishwa. Kuendelea kuung’ang’ania au kuung’ang’aniza ni kuwachosha zaidi wale wanaoutumikia sawia na wananchi, ambao kwa mantiki hiyo, ndio wanaotumikiwa. Kwa hilo naungana na Pinda kwamba amechoka na wananchi wamechoka vilevile.
Hebu fikiria mfumo wa utawala unaotoa maelekezo wananchi wapigwe mabomu ya kutoa machozi na kumwagiwa maji ya kuwasha kwa madai kwamba wananchi hao wamekusanyika bila kibali ilhali ikieleweka kwamba watu hao wamekusanyika kwa ajili ya maombolezo na maandalizi ya mazishi. Lakini hiyo inafanyika kwa vile wananchi wa eneo husika wanaonyesha upinzani kwa mfumo unaotawala!
Ugumu wa mfumo huu unaotumika kutawala nchi yetu kwa sasa tunaweza kuupima kupitia kwenye nasaha za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alizozitoa kama wasia karibu na mwisho wa uhai wake.
Mwalimu alikuwa akionesha mashaka makubwa kila alipokuwa anauangalia mwenendo wa chama chake alichokianzisha. Mfano alipokuwa anagusia Azimio la Arusha, moja ya mambo muhimu na muhimili wa siasa za nchi yetu, ambayo CCM iliyarithi na kuamua kuyatelekeza kinyemela kwa sababu ambazo hakuna anayeweza kuziweka wazi, alikuwa akionyesha wazi ugumu kilio nao chama chake hicho.
Kila mara Mwalimu alipokuwa anagusia Azimio la Arusha, wakati huo kabla hajaaga dunia, alikuwa akitania kwamba kuliongelea Azimio hilo kwa wakati huo ilitakiwa mtu uwe na roho kama ya mwendawazimu. Kwa tafsiri pana ya utani huo wa Mwalimu ni kwamba kuitumikia CCM, kwa jinsi ilivyo kwa sasa, ni lazima uwe na roho kama ya mwendawazimu. Naitafsiri hivyo kauli hiyo kwa vile Azimio la Arusha ndio uliokuwa utambulisho namba moja ambao chama hicho kiliurithi na kuapa kuulinda na kuuendeleza.
Fikiria unavyoweza kuitumikia jumuiya iliyoamua kupoteza utambulisho wake. Utaitumikia ukijitambulisha kama nani? Si ni lazima uwe na roho kama ya mwendawazimu?
Pengine hilo ndilo tatizo linalochochea kauli tata kama zile za “atakayekamatwa kwa kosa fulani auawe hapohapo”, “lenye kuwa na liwe maana tumechoka”, “mimi nasema hao wapigwe tu” nakadhalika.
Lakini hatahivyo, kama nilivyosema awali, mimi siamini kama Pinda kachoshwa na nguvu za upinzani anaotaka ushughulikiwe vya kutosha. Nahisi matendo haya ya kinyama yanafanyika kutokana na watawala kuyafurahia, kufurahia kuona watu wakipigwa, wakijeruhiwa na hata kuuawa kwa amri zao.
Kumbuka watawala wa Kirumi walikuwa nao ugojwa wa aina hiyo wa kufurahia kuwaona watu wakiteseka kwa njia mbalimbali. Mtu angeweza kurushwa ndani ya eneo lenye simba mwenye njaa huku watu wakiangalia jinsi anavyoraruliwa na kutafunwa kama mchezo wa kuburudisha!
Kama kweli haya yangekuwa yamewachosha watawala wetu, kama alivyodai Pinda, kwa nini yeye, Pinda, chama chake na serikali wanayoitawala wasichukue uamuzi kama wa waziri mkuu wa mwisho wa makaburu, F. W. de Klerk? Yeye alipoyachoka madai ya wazalendo wa nchi yake tulikiona kilichofuatia. Hakuendelea kuwaamuru polisi kwamba “piga hao tu”.
Tunamjua Pinda, mtu asiye na makuu, asiye na majivuno, mtu aliyeendelea kuishi kwenye “flat” ya kupanga pale Kinondoni Makaburini hata baada ya kuwa waziri kamili kabla ya kuwa waziri mkuu. Ni mtu ambaye akijitambulisha kama mtoto wa mkulima hakuna aliyetia shaka. Lakini tusisahau kauli ya Nyerere kwamba 

kulitaja Azimio la Arusha, kwa maana ya kuitumikia CCM,  ni lazima uwe na akili kama ya mwendawazimu.

prudencekarugendo@yahoo.com  0784  989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau