Bukobawadau

BAADHI YA WAHAMIAJI HARAMU WAGOMA KUREJEA KWAO

na Ashura Jumapili, Kagera
BAADHI ya raia wa Rwanda waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria wamegoma kurejea nchini kwao, badala yake wameamua kwenda katika nchi za Uganda na Burundi.
Akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti hili ofisini kwake, naibu kamishna wa uhamiaji ambaye ni kaimu afisa uhamiaji mkoa wa Kagera, Elizeus Mushongi, alisema raia hao wa Rwanda waliogoma kurudi kwao ni wengi.
Hata hivyo, alisema raia wengi wameitikia wito wa kurejea makwao na kwamba zaidi ya wahamiaji haramu 7,000 wamerejea katika nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.
Alisema idadi hiyo sio sahihi kwani kuna wahamiaji wengi waliorudi makwao kwa kupitia njia za panya, wengine kwa hofu ya kukamatwa au kunyang’anywa mali walizochuma wakiwa nchini.
Aliongeza kuwa kituo cha Rusumo kinaongoza kwa kupitisha wahamiaji haramu wengi ambacho kimepitisha jumla ya wahamiaji haramu 4748 wakielekea nchini Rwanda.
Alisema katika vituo vya Murusagamba walipita Wanyarwanda 35 wakielekea Burundi, Mutukula (13) wakielekea Uganda, Bugango (22) wakielekea Uganda, Kanyigo (7) wakielekea Uganda, Kabanga Warundi 522 wakielekea nchini Burundi na 10 kupitia kituo cha Murongo kuelekea Uganda katika kituo hicho Wanyarwanda 166 walipitia hapo kuelekea nchini Uganda.
Kadhalika bunduki 42 zimesalimishwa mkoani Kagera, huku maelfu ya mifugo inayodaiwa kumilikiwa na wahamiaji hao ikirejeshwa makwao.
Alisema kituo cha Murongo kimepitisha jumla ya wahamiaji 332, Murusagamba (78) na Mutukula (31) na eneo la Mgoma ambalo hakuna vituo vya idara ya uhamiaji walijisalimisha wahamiaji haramu (1734) katika ofisi za vijiji.
Alisema idadi ya ng’ombe walioondoka hadi kufikia jana ni 1996 kupitia kituo cha Rusumo hata hivyo alisema kuwa ng’ombe wengi wanaelekea Uganda kwa sababu Rwanda hawataki idadi kubwa ya ng’ombe.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za wahamiaji haramu walioondoka kwa hiari Wanyarwanda ni asilimia 64, Warundi (34) na Waganda (2).
Hata hivyo aliwataka wahamiaji hao haramu waendelee kuondoka kwa hiari kabla hawajafikishwa kwenye mkono wa sheria.
Aidha alisema Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera imesitisha utoaji wa vibali kwa muda wakisubiri maelekezo kutoka juu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali mstaafu, Fabian Massawe, amewatahadharisha wananchi kuwa makini wakati wa msako huo wa wahamiaji haramu sambamba na kuwafichua waliojificha.
Massawe alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria watu watakaobainika wakiwaficha na kuwawekea vifua wahamiaji haramu.
Alisema msako huo utaanza muda wowote kuanzia sasa na hawezi kutaja siku rasmi kwa sababu za kiusalama.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Philip Kalangi alisema jumla ya silaha 42 zimewasilishwa kwa hiari na wahamiaji haramu kufuatia agizo la Rais lililoisha jana kutoka sehemu mbalimbali hapa mkoani.
Alisema wahamiaji haramu wote watakaokamatwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Next Post Previous Post
Bukobawadau