Bukobawadau

BRAKING NEWS;CCM KAGERA YAWAFUKUZA MADIWANI WAKE 8 WA MANISPAA YA MJI WA BUKOBABukoba: Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera kimewafukuza uanachama wa chama hicho, madiwani wake wanane kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kukaidi maelekezo mbalimbali ya chama hicho, pia kushirikiana na upinzani kukihujumu.
Madiwani waliotimuliwa ni wale Manispaa ya Bukoba ambao wamekuwa wakitajwa kumuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye amekuwa akivutana vikali na Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani.
Miongoni mwa waliotimuliwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba na Diwani wa Kashai, Yusuph Ngaiza, aliyepata kuwa mbunge wa muda mrefu wa Bukoba Mjini na baadaye Meya wa Manispaa hiyo, Samuel Ruhangisa ambaye ni Diwani wa Kitendagulo na Diwani wa Buhembe, Alexander Ngalinda ambaye pia alikuwa Naibu Meya.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi alisema uamuzi wa kuwatimua madiwani hao umefikiwa jana na halmashauri ya CCM ya Mkoa kwa kile alichosema ni kwa ajili ya “kulinda masilahi ya chama na wananchi wa Bukoba”.
Ibara ya 93 (15) ya Katiba ya CCM inataja moja ya kazi za halmashauri ya chama hicho ngazi ya mkoa kuwa ni: “Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri ya CCM ya Mkoa”.
Hata hivyo kipengele cha 14 cha ibara hiyo ya 93 kinasema hatua kumwachisha au kumfukuza mtu uanachama itachukuliwa endapo halmashauri itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uanachama.
Hatua ya kuwafukuza uanachama madiwani hao ambao pia watakuwa wamepoteza nafasi zao za udiwani, imekuja siku chache tangu Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipozitaka pande zinazohusika katika mgogoro huo kumaliza kwa njia ya mazungumzo.
“Madiwani wote wa CCM walioendelea na mgomo hata baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kusaini barua ya kutaka Mkurugenzi aitishe kikao cha kumwondoa Meya tumefikia uamuzi mgumu wa kuwafukuza uanachama kwa masilahi ya chama na wananchi wa Bukoba,’’ alisema Mushi.
Mushi aliwataja madiwani wengine waliofukuzwa ni Robert Katunzi (Hamugembe), Deus Mutakyahwa (Nyanga), Richard Gasper (Miembeni), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu) na Dauda Kalumuna aliyekuwa Diwani wa Ijuganyondo.
Katibu huyo alisema Balozi Kagasheki na Meya Amani ambao mamlaka yao ya uteuzi ni ya kitaifa na wanatakiwa kumaliza tofauti zao kama walivyoelekezwa na Rais.
Mgogoro uliosababisha madiwani hao kutimuliwa uliibuka baada ya Kagasheki kumtuhumu Meya Amani kwamba ameingiza Manispaa katika miradi ya ufisadi hali ilioibua makundi na kukwamisha kufanyika hata vikao vya Baraza la Madiwani.

Waliofukuzwa ni;


1.Richard Gaspar (Miembeni )


2.Murungi Kichwabuta (viti maalum)


3.Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe)


4.Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai)


5.Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga)


6.Robert Katunzi (Hamugembe)


7.Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na


8.Dauda Kalumuna (ijuganyondo).

Credit:Matias Byabato
Chanel ten BUKOBA 
Next Post Previous Post
Bukobawadau