Bukobawadau

Dk. Vedastus Kyaruzi na historia iliyopotea

Na Prudence Karugendo

Historia ya nchi yetu inayataja mambo mengi mbalimbali ambayo kwa pamoja ndiyo yameifanya nchi yetu kuwa namna ilivyo. Na tunapotaka kuitendea haki historia hatuna budi kukitaja kila kitu kilichotoa mchango wake, uwe hasi au chanya, katika kulifikisha taifa letu mahali lilipo.

Lakini kwa bahati mbaya, au pengine kwa makusudi, tumekuwa tukiipotosha historia kwa kuyachuja baadhi ya mambo na kuyaondoa katika historia tukiyataja tu yale ambayo tunaona yanatufurahisha kuwa ndiyo yanayofaa kubaki kwenye historia ya nchi yetu huku mengine tukiyafanya yasahaulike kana kwamba hayakuwahi kuwepo.

Katika makala haya nimekusudia kumuangalia Marehemu Dk. Vedastus Kyaruzi Kyarakishaija Nshunju Kaembe, mmoja wa wasomi wa kwanza nchini kujitumbukiza katika harakati za ukombozi wa Mtanganyika. Dk. Kyaruzi aliugua ghafla na akafariki tarehe 20 Mei, 2012, mjini Bukoba, baada ya kuwa amesahaulika kwa muda mrefu katika historia ya nchi yetu.

Ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona kwamba Dk. Kyaruzi, mmoja wa waasisi wa harakati za ukombozi wa taifa letu, na mmoja wa watumishi wa kwanza waadilifu wa Tanganyika huru na baadaye Tanzania, anasahaulika kiasi cha kizazi cha Muungano wa Tanzania, nina maana ya Watanzania walizaliwa baada ya Muungano, kutojua lolote juu ya mzalendo huyo wa kabla ya uhuru. Watanzania wengi waliokuwa hawamjui Dk. Kyaruzi wangepata nafasi ya kumjua pamoja na umuhimu wake kwao, kama historia ingetendewa haki na mamlaka husika.

Ni nani huyu Dk. Kyaruzi? Huyu ni mwanachi mzalendo aliyejitumbukiza katika harakati za kumkomboa Mtanganyika hata kabla ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hajafikiria kujiingiza kwenye siasa. Dk. Kyaruzi alikuwa katibu wa Tanganyika African Assocciation (TAA), tawi la Makerere, wakati akisomea utabibu katika chuo hicho kilichoko katika Jiji la Kampala nchini Uganda.

Katika maelezo yake, Dk. Kyaruzi alikuwa akisema kwamba wakati wako chuoni hapo, Nyerere, ambaye alikuwa nyuma yake kwa mwaka mmoja, alikuwa hajawa machachari katika siasa na ni kama alikuwa anaihofia siasa.

Baada ya Dk. Kyaruzi kurudi nyumbani, alipomaliza masomo yake, akajumuika na vijana wenzake wakati huo, baadhi yao wakiwa wasomi kama yeye, katika harakati za kuendeleza mapambano ya kudai haki na maslahi ya Mtanganyika. Alijumuika na akina Hamza Mwapachu, Dk. Luciana Tsere, Abdul Sykes, Mzee John Rupia, Stephen Mhando, Hamza Aziz na Tomas Marealle. Wakati huo Nyerere alikuwa akifundisha pamoja na Balozi Andrea Tibandebage katika shule ya St. Mary’s, Tabora.

Mwanzoni mwa mwaka 1950, TAA ilikuwa tayari imetekwa na wasomi, na harakati za wasomi hao ziliwatisha wakoloni wa Kingereza na hivyo wakoloni hao kuanza kufanya mbinu za kuvunja nguvu za umoja huo kwa kuwahamishia wasomi hao sehemu mbalimbali mikoani.

Katika mbinu hizo za kuvunja nguvu za TAA, Dk. Kyaruzi alipewa nafasi ya kwenda masomoni Ulaya lakini akaikataa. Kutokana na kuikataa nafasi hiyo akahamishiwa mkoani Morogoro. Lakini bahati nzuri katika kipindi hicho Nyerere alikuwa anarejea nyumbani toka masomoni Ughaibuni na akawa amepangiwa kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Pugu iliyoko karibu na Jiji la Dar es salaam.

Kwahiyo baada ya Nyerere kujiunga na TAA Dk. Kyaruzi akamkabidhi uenyekiti wa chama hicho na katibu wake akawa Abdul Sykes. Tofauti na akina Kyaruzi walioichukua TAA ikiwa haina hata ofisi, majalada na wafuasi wanaoeleweka vizuri, Nyerere aliichukua TAA wakati tayari ina ofisi, majalada na wanachama.

Mwaka 1954, Nyerere, kwa kushauriana na wenzake, wakaibadili TAA kutoka kwenye umoja wa kupigania haki na maslahi ya Watanganyika na kuwa chama cha siasa kilichoongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Baada ya Dk. Kyaruzi kuhamishiwa Morogoro, baadaye alipelekwa Nzega, Biharamulo na hatimaye Bukoba kabla ya kwenda masomoni Ulaya mwaka 1958. Alipotoka masomoni alirudishwa Nzega ambako alikutana na Nyerere na kumshauri juu ya kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi vijijini ili kuepuka kuelezwa hisia za uongo kutoka kwa watu ambao wakati huo walikuwa wanatafuta vyeo.

Tanganyika ilipopata madaraka, kabla ya uhuru kamili, Nyerere alimuomba Dk. Kyaruzi awe balozi lakini Dk. Kyaruzi akawa hakubaliani na ombi hilo. Ndipo Nyerere akamweleza kwamba alikuwa nao uwezo wa kuajiri wataalamu katika nyanja mbalimbali kutoka nje ya nchi, kama vile wahandisi na madaktari, lakini hakuwa na uwezo wa kuajiri watu kutoka nje ya nchi na kuwafanya mabalozi wa kuiwakilisha Tanganyika nje ya nchi.

Baada ya maelewano na makubaliano na Nyerere Dk. Kyaruzi alipelekwa London, Uingereza, na baadaye New Zealand ili kupata mafunzo ya kidiplomasia.

Tulipopata uhuru tayari Dk. Kyaruzi alikuwa Jijini New York kama balozi wa kwanza wa Tanganyika huru katika Umoja wa Mataifa akisaidiwa na Chifu Lukumbuzya na Balozi Christopher Ngaiza. Kwahiyo ni Dk. Kyaruzi aliyesimika bendera ya Tanganyika huru katika Umoja wa mataifa.

Muda mfupi baada ya uhuru Dk. Kyaruzi alirudishwa nyumbani na kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi. Ni katika wadhifa huo ambapo Dk. Kyaruzi alionyesha kile ambacho kingemfanya aendelee kukumbukwa zaidi na taifa hili, uadilifu uliotukuka katika kazi, tuseme uzuiaji wa ubadhirifu wa pesa za umma.

Katika moja ya masimulizi yake, Dk. Kyaruzi, alieleza alivyoondoka nchini, mwaka 1963, akiwa katika ujumbe wa Tanganyika ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Oscar Kambona wakati huo, kwenda Adds Ababa, Ethiopia, kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Alieleza kwamba watu wote walioidhinishwa na Rais kuwa katika msafara huo walijulikana na majina yao yote alikabidhiwa yeye, kama Katibu Mkuu, kwa vile ndiye aliyekuwa amebeba fungu la masurufu kwa ajili ya watu wote waliokuwa kwenye msafara huo.

Kumbe Waziri Kambona alikuwa ameliingiza kinyemela jina la rafiki yake, Dk. Wilbert Kleruu. Kwa vile jina hilo halikuwa katika orodha aliyokuwa nayo Dk. Kyaruzi akakataa kumhudumia Dk. Kleruu kwa nja yoyote akianzia na kutomlipia hoteli. Tendo hilo lilimfanya akwaruzane na waziri wake, Kambona, waziri huyo akidai kwamba Dk. Kyaruzi amemdhalilisha ugenini. Lakini yeye, Dk. Kyaruzi, alichokisimamia ni uadilifu katika kazi, maana kule walienda kikazi na si kwa ajili ya matanuzi kwa kutumia pesa za walipa kodi kama alivyotaka Kambona.

Waliporudi nyumbani Kambona akamchongea Dk. Kyaruzi kwa Nyerere ili amfute kazi. Naye Dk. Kyaruzi alipopata habari hizo akaomba kujiuzulu kazi. Ndipo Nyerere alipomwachia aende Lagos, Nigeria, kuongoza kitengo cha shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) Kanda ya Afrika Kusini ya Jangwa la Sahara.

Kwa hiyo tunapowataja makamanda wa vita dhidi ya ubadhirifu na ufisadi wanaojionyesha kwa sasa, makamanda ambao lakini hawako tayari kuachia ngazi kuonyesha jinsi wasivyoridhishwa na mwenendo wa vita hiyo inayosuasua, ndipo ingetubidi tuwakumbuke watu kama Dk. Kyaruzi aliyekubali kuachia ngazi, katika nafasi ya juu kitaifa, Katibu Mkuu wa Wizara, katika kuupinga ubadhirifu, au ufisadi kwa lugha ya sasa.

Huyu siyo mtu ambaye historia ya nchi hii inapaswa kumpa kisogo. Vinginevyo tukubali kwamba Watanzania kwa sasa tumepoteza kabisa uwezo wa kuweka kumbukumbu za taifa letu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Na taifa lisilo na kumbukumbu ni lazima lionekane ni taifa la ajabu.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau