Bukobawadau

JK AMJIBU KAGAME KATIKA HOTUBA YAKE YA MWISHO WA MWEZI JULAI

Uhusiano na Nchi ya Rwanda

Ndugu wananchi;
Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.

Napenda kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.

Ndugu Wananchi;
Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu. Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yo yote. Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo. Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.

Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi. Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.

Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.

Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi
kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.

Source: Hotuba ya Rais Mwisho wa Mwezi Julai 2013
Next Post Previous Post
Bukobawadau