Bukobawadau

JK: Tujiandae kisaikolojia muundo wa Serikali Tatu

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amewataka wana CCM nchini, kujiandaa kisaikolojia juu ya muundo wa Serikali tatu pindi Watanzania watakapoamua hivyo.
Chanzo chetu cha habari kilichokuwa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, kilichokutana mjini Dodoma jana, kilisema Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose Migiro, kuwasilisha hoja yake katika kikao hicho kilichokaa kama Baraza la Katiba.

“Mjadala wa Katiba umechukua nafasi kubwa kwani baada ya mjadala kuanza, Rais Kikwete aliwataka wajumbe kujiandaa kisaikolojia.

“Alisema mwaka 1992 wakati nchi inaingia katika mfumo wa vyama vingi, Rais wa wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere akiwa katika kiti, alisema pamoja na wengi kukataa mfumo wa vyama vingi kwa asilimia 80, waliokubali kwa asilimia 20 lazima wasikilizwe.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni wazi ilionyesha ukomavu kwa wajumbe wengi, lakini pamoja na yote michango ambayo ilikuwa ikitolewa, wengi waling’ang’ania mfumo wa Serikali mbili kama ilivyo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya waliopinga walisema kuna haja ya kuendelea na mfumo wa Serikali mbili, kwa kuwa ndio unaokubalika.

Pamoja na hayo, chanzo hicho kilisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho ambaye ni mjumbe wa NEC, Zanzibar alisema ni vema chama hicho kikaachana na mjadala wa Katiba Mpya kwani haliko katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Mjumbe huyo wa NEC kutoka visiwani Zanzibar, alisema si vema kwa CCM kujadili rasimu ya Katiba wakati baadhi ya ahadi zilizotolewa na chama hicho, hazijatekelezwa.

Katika kikao hicho kilichoingia kwa siku ya pili, hadi kufikia jana wajumbe hao waliweza kujadilia Rasimu ya Katiba Mpya kwa kina na kuchambua udhaifu uliopo.

Baadhi ya wana CCM wamekuwa wakitofautiana na pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba, linalopendekeza muundo wa Serikali tatu.

Katika kupingana na maoni ya tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, Kamati Kuu ya CCM, iliyoketi Juni mwaka huu, iliamua wana CCM kuanzia ngazi ya matawi waunde mabaraza ya Katiba ya chama hicho ili kujadili rasimu hiyo, hasa hasa kuangalia muundo wa Serikali ya Muungano.

Akisoma taarifa kwa wajumbe wa NEC juzi, Katiba Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema katika mabaraza hayo ya Katiba, wanachama milioni 2.6 walitoa maoni yao ambayo yamefanyiwa kazi huku wengi wao wakiwa ni wana CCM.

Wakati huo huo, mgogoro wa kufukuzwa kwa madiwani wanane wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, bado haujapatiwa ufumbuzi.

Utata huo umekuja baada ya viongozi wanaohusika na mgogoro huo, kuitwa mbele ya Kamati Kuu kwa ajili ya kuhojiwa.

Hata hivyo, baadhi yao walichelewa kuwasili mjini Dodoma na hivyo kikao kuahirishwa hadi jana jioni.

Pamoja na baadhi yao kuchelewa, Kamati Kuu iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete, iliwahoji Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Constacia Buhiye na Katibu wake, Avelin Mushi.

Hadi tunakwenda mitamboni, Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki, ambao wanahusika katika mgogoro wa madiwani hao, walikuwa hawajahojiwa.
VIA MTANZANIA.

Next Post Previous Post
Bukobawadau