Bukobawadau

Taifa latikiswa *Matapeli wa kimataifa wajipenyeza serikalini *Wawekezaji wa kigeni walizwa mamilioni

MTANDAO wa matapeli wa kimataifa ambao umekuwa ukiendesha shughuli zake haramu sehemu mbalimbali duniani, sasa umejipenyeza katika taasisi na vyombo vya dola hapa nchini, MTANZANIA Jumatatu linaripoti.

Kubainika kwa mtandao huo hapa nchini, kumetokana na kuvuja kwa taarifa za siri za baadhi ya wawekezaji wa kigeni ambao wametapeliwa mamilioni ya Dola za Marekani na watu ambao wamekuwa wakijitambulisha kwao kuwa ni maofisa wa Serikali au makamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wenye ushawishi serikalini. 

Vyanzo vya habari vya MTANZANIA Jumatatu vilivyoko serikalini vimedokeza kuwa, wawekezaji waliokutana na dhahama hiyo ni wale ambao wanajihusisha na biashara ya madini kwa kificho mbali na kuendesha shughuli zao halali zinazotambuliwa na Serikali.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa, baadhi ya wafanyabiashara wa Kitanzania waliojenga mtandao wao kwa baadhi ya maofisa wa Serikali, wameingizwa kwenye genge hilo na ndio ambao wamekuwa wakitumiwa kuwarubuni hadi kuwaibia wawezekaji.

Watanzania wanaotajwa kuwa wanachama wa genge la matapeli wa kimataifa, ni wamiliki wa migodi ya madini iliyo sehemu mbalimbali hapa nchini na wanatajwa kuwa na makazi ya kudumu katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Ruvuma.

Tayari baadhi ya mawasiliano ya genge hilo la matapeli na wawekezaji, yamekwishanaswa na taasisi za dola na Mtanzania Jumatatu limefanikiwa kuyaona, lakini pia zipo taarifa zinazoeleza kuwa usiri uliotawala katika sakata hilo unakwamisha uwezekano wa kuwatia nguvuni.
Katika moja ya mawasiliano hayo ambayo gazeti hili limeyaona, Mtanzania anayetajwa kuwa kiongozi wa genge la matapeli (jina lake tunalihifadhi kwa sasa), anaandika ujumbe kupitia kwenye simu yake ya kiganjani kwenda kwa mwekezaji raia wa China (jina pia tunalihifadhi) akijitambulisha kuwa yeye ni Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika andishi lake hilo alilolituma kwa kutumia teknolojia inayojulikana kitaalamu kama ‘wahtsapp’ anamueleza mwekezaji huyo kuwa mpango wa kupatikana kwa shehena ya madini ya Shaba unakwenda vizuri.

Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa, wakati tapeli huyo akijitambulisha kwa wadhifa wa Jenerali wa JWTZ kwa mwekezaji wa Kichina, rekodi zake zinaonyesha kuwa hajawahi kupata mafunzo yoyote ya kijeshi na kwamba amekuwa akijihusisha na biashara zenye kutiliwa shaka, huku akifahamika zaidi kwa wafanyabiashara wa madini nchini kama mtaalamu wa lugha ya Kiingereza na pia kwa jina la Jenerali.

Ripoti ya uchunguzi wa mwenendo wa Jenerali ambayo gazeti hili limeiona, inaonyesha kuwa ndiye kiongozi wa mtandao wa genge la matapeli na pia hufanya kazi ya kufanikisha mawasiliano kati ya wafanyabiashara wa kigeni na wazawa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea Lugha ya Kiingereza.

Mbali na Jenerali, ripoti hiyo inamtaja Mtanzania mwingine anayependelea kuvaa mavazi ya asili ya Nigeria (jina lake tunalo lakini tunalihifadhi kwa sasa) ambaye hana uelewa wa kutosha wa Lugha ya Kiingereza, lakini akiwa na mtandao wake serikalini kuwa mkurugenzi wa fedha za genge la matapeli wa kimataifa kwa upande wa Tanzania.

Katika ripoti hiyo, matukio ya hivi karibuni ya utapeli yanayoelezwa kufanikishwa na genge hilo ni pamoja na lile linalomuhusisha mwekezaji raia wa China ambaye alitapeliwa Dola za Marekani 200,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 320 za Tanzania, baada ya kudanganywa kupatiwa madini ya Shaba kutoka katika Mgodi wa Madini hayo uliopo Tunduru, Mkoa wa Ruvuma.

Tukio jingine linalotajwa linamhusisha raia mwingine wa China, ambaye alitakiwa kutoa Dola za Marekani milioni tatu ili auziwe mgodi wa madini ya Shaba uliopo Tunduru mkoani Ruvuma.

Kabla tukio hilo la kihalifu halijakamilika, mfanyabiashara huyo wa Kichina alidokezwa kuwa tayari mgodi huo ulikwishauzwa kwa mfanyabiashara wa Marekani aliyetajwa kwa jina moja la Bravo, ambaye naye alitapeliwa Dola za Marekani milioni mbili wakati wa ununuzi wa mgodi huo.

Mbali na matukio hayo, linatajwa pia tukio lile la uuzaji tani 3,000 za Shaba safi kwa kundi la wafanyabiashara wa Kichina, nao baada ya kutoa malipo ya awali walibaini kuwa, katika shehena ya Shaba waliyokuwa wakinunua, Shaba halisi ilikuwa tani 100 tu.

Uchunguzi zaidi wa mwenendo wa genge hilo unaonyesha kuwa, limekuwa likijihusisha na uuzaji wa leseni ndogo za uchimbaji madini (Primary Lisence) kwa raia wa kigeni wasiofuata taratibu za nchi kuendesha biashara zao hapa nchini. Upatikanaji na uuzaji wa leseni hizi, unaelezwa pia kuwahusisha baadhi ya maofisa wa Serikali.

Kwa mujibu wa Sheria ya madini ya Tanzania, leseni hizo ni kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambao ni wazawa na hairuhusiwi kuingia ubia na wageni kwa kutumia leseni hizo.

Wakati hayo yakibainika, taarifa za hivi karibuni zilizolifikia MTANZANIA Jumatatu, zinaonyesha kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya genge la matapeli wa kimataifa lililoko Tanzania na nchini China, ambalo baadhi ya wanachama wake ni wafanyakazi katika kampuni moja ya silaha ya nchini humo.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama wa mtandao huo waliopo hapa nchini, wanadaiwa kujitambulisha kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, kuwa wao ni watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na hata baadhi ya makachero wanawatambua hivyo imekuwa vigumu kwao kuwatia nguvuni licha ya kutoridhishwa na nyendo zao.

MTANZANIA Jumatatu liliwasiliana na Idara ya Uhamiaji Makao Makuu, jijini Dar es Salaam ili kujua uhalali wa ukaazi wa baadhi ya raia wa kigeni, ambao wanamtandao wa kundi hilo waliopo hapa nchini, lakini katika hali isiyotarajiwa lilinyimwa ushirikiano hata pale lilipoonyesha baadhi ya vielelezo lilivyonavyo kuhusu sakata hilo.

Wakati utapeli huo ukishika kasi, jana Gazeti Dada la Mtanzania Jumapili, lilieleza jinsi ambavyo matapeli wamekuwa wakiwatapeli watu baada ya kujifanya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Miongoni mwa matapeli hao ni anayejiita Baraka Tibaijuka ambaye amefanikiwa kuwatapeli watu, baada ya kumchangia mamilioni ya fedha na yeye kuwapeleka Ikulu kwa ahadi kwamba, angewasaidia kupata kazi.
source; Mtanzania.
Next Post Previous Post
Bukobawadau