Bukobawadau

KAGERA KUPELEKA WASHIRIKI 36 RIADHA

WAKATI joto la mashindano ya riadha ya taifa yanayotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro Agosti 23 na 24 likiendelea kushika kasi, Mkoa wa Kagera umewathibitisha wanariadha 36 watakaouwakilisha katika kinyang’anyiro hicho.

Wanariadha hao ambao wameweka kambi katika Klabu ya Holili Youth Athletic, iliyoko Holili, mkoani Kilimanjaro, wanatarajiwa kuondoka kwenda Morogoro Agosti 21 na 22 mwaka huu.

Kikosi hicho kinachoundwa na wakimbiaji, watupa tufe na warusha mkuki, kiko chini ya ukufunzi wa Kocha mzoefu, Adram Mikumi, na kinatarajiwa kuondoka na msafara wa viongozi watano, akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Kagera (KAAA), Sixbert Prosper.

Prosper aliiambia Tanzania Daima kuwa sababu zilizofanya wahamishie kambi Kilimanjaro ni kutokana na azima ya mkoa wake kufanya mapinduzi katika michezo, hasa riadha na katika kutimiza azima hiyo, waliipendekeza Klabu ya Holili ambayo kwa sasa inasifika kwa kuzalisha wakimbiaji wazuri.

Prosper alisema maandalizi yanakwenda vizuri, lakini wanakabiliwa na tatizo la udhamini, ambapo maombi waliyotuma kwa kampuni na taasisi mbalimbali hadi sasa ni Mfuko wa Hifadhi wa PSPF tu ndio uliotoa ushirikiano.
Next Post Previous Post
Bukobawadau