Bukobawadau

Kauli ya JK yawaponza wakazi Rutoro

na Ashura Jumapili, Muleba
KAULI ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka wahamiaji haramu kuondoka katika ardhi ya Tanzania imewaweka katika wakati mgumu wakazi wa Kata ya Rutoro iliyoko Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera baada ya wafugaji kutoka Rwanda waliopo nchini kinyume cha utaratibu kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wananchi na kulisha mazao yote.
Hayo yalibainishwa na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Muleba.
Alisema siku rais alipotangaza kuondoka kwa wahamiaji haramu kabla ya msako kuanza wakati akiwahutubia wakazi wa Wilaya ya Biharamulo, Wanyarwanda walichukua mifugo yao na kuingiza katika mashamba ya wananchi wa kata hiyo.
“Wanyarwanda wanadai rais amewauzia nchi, nilimweleza rais kuhusu taarifa hizo akachukia,” alisema Mwijage.
Alisema mamlaka ya Mkoa wa Kagera haiwezi kutatua tatizo la wafugaji haramu na wazawa wa Kata ya Rutoro kwa sababu mtandao huo una nguvu za kifedha na unawezeshwa na nchi za nje.
Aidha, alisema wananchi wamekosa imani na Jeshi la Polisi kwa madai wakienda kutoa taarifa za uhalifu zinazowahusu wahamiaji haramu wanageuziwa kibao wao.
Alisema serikali kupitia Wizara ya Ardhi wameamua kufuta vitalu vyote ili wapime upya waweze kubainisha maeneo ya wananchi na wafugaji.

Next Post Previous Post
Bukobawadau