Bukobawadau

Mama Tibaijuka kuongoza kamati ya soko la kahawa

Mama Anna Tibaijuka pichani
Na Edson Kamukara
RAIS Jakaya Kikwete ameunda kamati ya kuchunguza na kuboresha soko la bei ya kahawa na ndizi katika Mkoa wa Kagera ambayo itaongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
Rais alifikia uamuzi huo hivi karibuni akiwa ziarani mkoani humo, ambapo mbali na mambo mengine alipewa taarifa ya kuporomoka kwa bei ya kahawa na ugonjwa wa mnyauko unaoshambulia migomba.
Pia Rais Kikwete alielezwa tatizo la kushamiri kwa biashara ya magendo ya kuvusha mazao hayo kwenda nchini Uganda, hivyo kuamua kuunda kamati hiyo.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Waziri Tibaijuka ambaye pia ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM), alisema kuwa kamati hiyo itatafuta njia ya kukomesha magendo ya mazao hayo nchini Uganda.
Uchunguzi wa kihabari uliofanywa na gazeti hili mkoani humo hivi karibuni, ulibaini magendo ya kahawa yanasababisha serikali kuu pamoja na halmashauri za wilaya husika kukosa mapato.
Biashara hiyo inafanywa na wafanyabiashara wa Uganda kwa kuwatumia baadhi ya Watanzania, hivyo kuifanya nchi kushika nafasi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa uzalishaji wa kahawa kwa wingi.
Biashara hiyo inadaiwa kuwahusisha wadau wengi wakiwamo viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na askari polisi wasio waadilifu.
Baadhi ya askari hao wanadaiwa kuwasindikiza wafanyabiashara hao kuvusha kahawa hiyo kwa ujira wa sh 1,000 kwa kila gunia moja.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera-KCU (1990) Ltd, Vedastor Ngaiza, aliliambia gazeti hili kuwa hali hiyo inaua chama hicho kwa kukikosesha kahawa.
Bei ya kahawa imekuwa ikiyumba kila msimu, hivyo wakulima kushawishika kuwauzia wanunuzi binafsi ambao hutoa bei zaidi kidogo ya ile ya KCU.
Mathalani msimu huu bei imeshuka kutoka sh 1,550 kwa kilo hadi sh 1,100 kwa kahawa ya maganda ya Arabica wakati ile ya Robusta nayo imeporomoka kutoka sh 1,300 hadi sh 1,000 kwa kilo.
Kahawa safi iliyokobolewa nayo imeporomoka bei kutoka sh 3,300 hadi sh 2,300 kwa kilo ya Arabica huku Robusta nayo ikiteremka kutoka sh 2,700 ya mwaka jana hadi sh 2,200 kwa kilo moja.
Vichochoro vinavyotumika kuvusha kahawa hiyo mpakani vipo Minziro, usafiri wa majini, Kigalama na Mulongo.
Via; Tanzania Daima
Next Post Previous Post
Bukobawadau