Bukobawadau

KCU tajiri, wakulima maskini

Edson Kamukara
CHAMA Kikuu cha Ushirika Kagera-KCU (1990) Ltd ni moja ya vyama vichache vikongwe vya ushirika nchini, ambacho kimekuwa mkombozi wa wakulima wa kahawa tangu mwaka 1950.
KCU kwa sasa kina ushirika wa vyama vya msingi 126 vyenye wanachama 60,000 wanaotoka katika wilaya za Muleba (50), Bukoba Vijijini (47), Misenye (27) na Bukoba Manispaa (3).
Wakulima hawa wamekuwa maarufu katika uzalishaji wa aina mbili za kahawa yaani Arabika na Robusta, zao ambalo limewainua kiuchumi na kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa KCU, Vedastor Ngaiza chama hicho ndicho kinaongoza nchini kwa kuuza kahawa nyingi nje ya nchi. Kwa mwaka wanauza hadi kontena 300.
Kutokana na mauzo hayo, KCU wameanzisha miradi mbalimbali kwa lengo la kujitegemea badala ya kutegemea ufadhili wa serikali.
Hadi sasa KCU kwa uchache inamiliki mali mbalimbali zikiwemo shule, hoteli, nyumba za makazi, nyumba za biashara, viwanja, magari pamoja na benki ya wakulima ya Kagera Farmers Co-OP Bank Ltd (KFCB).
Je, wakulima wananufaika na miradi pamoja na vitegea uchumi hivyo?
Tanzania Daima ilifanya utafiti wa kihabari mkoani Kagera hivi karibuni ili kuzungumza na wakulima na viongozi kupata ukweli.
Uchunguzi huo ulitokana na malalamiko ya baadhi ya wanaushirika wa KCU yaliyofikishwa kwa Waziri wa Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza wakimtaka aingilie kati kukagua utendaji wa chama chao wakidai viongozi wanatumia vibaya mali zao.
Walidai kuwa viongozi wamekuwa wakitumia fedha kugharamia miradi iliyoibuliwa kinyume na sheria ya vyama vya ushirika. Kwamba haina tija na maslahi yoyote kwao.
Baadhi ya miradi iliyotajwa ni ununuzi wa hoteli ya Yasila (sasa Bukoba Coop) iliyonunuliwa na KCU kwa sh milioni 500 za soko la hisa za biashara ya haki (Fair trade).
Kwamba ununuzi huo haukuidhinishwa na mkutano mkuu kama ilivyo matakwa ya sheria.
Malalamiko mengine yalihusu ujenzi wa jengo la ghorofa tatu katika Mtaa wa One Way katika Manispaa ya Bukoba ambao umegharimu sh milioni 750.
Wanachama hawa wanaona KCU haina manufaa kwao licha ya kumiliki mali nyingi, lakini inafika wakati msimu unafunguliwa chama hakina fedha ya kununulia kahawa yao.
Katika kulitazama hili, ni lazima kwanza kujua jukumu la serikali siku za nyuma kuwa lilikuwa kuvitupia macho ya ukaribu vyama hivi. Serikali ilijihusisha kwa kiasi kikubwa katika kutoa pembejeo, fedha na mafunzo.
Lakini kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika namba 20 ya mwaka 2003 na kanuni za vyama vya ushirika 2004, sera inayoongoza ushirika kwa sasa inasema serikali inawajibika katika uandaaji wa mazingira mazuri ya ushirika kustawi. Mihimili mikuu ya kukua itakuwa wanachama na menejimenti ya ushirika wenyewe.
Lengo ni kuwezesha vyama vya ushirika kujenga uwezo wa kujitegemea kidemokrasia na kujimudu kiuchumi. Sheria na kanuni hizi zinaelezea jinsi ushirika unavyopaswa kuanzishwa na kuendeshwa nchini. Zinakusudia kutekeleza kwa vitendo sera ya ushirika. Sheria hiyo inafafanua kuwa ushirika unapaswa kuanzishwa na kuendeshwa kwa mujibu wa kanuni za kimataifa za vyama vya ushirika zilizotajwa.
Serikali na waziri mwenye dhamana ya ushirika wana wajibu wa kuunda sheria zinazohamasisha uanzishwaji wa ushirika nchini. Aidha, rais kumteua mrajis wa vyama vya ushirika ambaye ndiye o?sa msimamizi wa utekelezaji wa sheria na kanuni zake.
Kazi za mrajis ni kusajili, kuendeleza, kukagua na kuvishauri vyama vya ushirika kumshauri waziri wakati vinapohitaji msaada, kuhamasisha uanzishaji wa vyama katika maeneo yote ya uchumi.
Katika kuendesha shughuli za ushirika, ziko kanuni saba zilizoainishwa na Muungano wa Kimataifa wa Vyama vya Ushirika (ICA) ambazo ni uanachama wa hiari na wazi, uongozi wa kidemokrasia na ushiriki wa wanachama katika shughuli za kiuchumi.
Kanuni nyingine ni kujitawala na kujitegemea, elimu, mafunzo na habari, ushirikiano baina ya vyama vya ushirika na kuijali jumuiya.
Baadhi ya wakulima wa KCU waliohojiwa walikiri kuwa na uelewa mdogo katika masuala ya miradi na mali zinazomilikiwa na chama chao, na kwamba ndiyo sababu ya kutoona kama zinawanufaisha.
Benedictor Rwamleba ni mkazi wa Kata ya Kashasha, anasema licha ya chama chao cha msingi Rulongo kuwa na wawakilishi kwenye mkutano mkuu, mipango inayoidhinishwa huko taarifa zake haziwafikii.
Meneja Mkuu wa KCU, Ngaiza anasema chama hicho kinamiliki nyumba za makazi 28, za kibiashara 12, magari, hoteli mbili za Lake na Bukoba Coop (Yasila) na benki ya wakulima.
Anafafanua kuwa vitega uchumi hivyo ndivyo vinawawezesha kudhaminika wanapoomba mikopo kwenye benki au taasisi za fedha. Anatolea mfano hoteli ya Yasila kuwa imewawezesha kupata mkopo wa sh bilioni 1.5.
Yasila ni moja ya miradi inayodaiwa kununuliwa kinyume na utaratibu wa chama, lakini taarifa za vikao vya KCU zinaonyesha kuwa wakulima hao kupitia mkutano wao mkuu waliridhia ununuzi wake.
Hata jengo la ghorofa tatu katika Mtaa wa One way ambalo gharama zake zilikuwa zikilalamikiwa, wanachama waliridhia ujenzi wake ambao sasa umekamika na limezinduliwa Julai 24 mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.
KCU inamiliki shule tatu za sekondari za Kishoju iliyopo wilayani Muleba, Kashozi na Mugeza zilizopo Bukoba mjini.
Hata hivyo imebakia kuwa mmiliki tu kwani shule hizo sasa zinaendeshwa na serikali.
Chama hicho kinamiliki na kuendesha benki ya wakulima, lakini bado ina mtaji mdogo usioiwezesha kukopesha fedha za kununulia kahawa, badala yake KCU inaendelea kukopa katika benki ya CRDB na hivyo gharama nono ya riba kwenda huko.
“Kwa msimu tunakopa kama sh bilioni 14 CRDB kwa ajili ya kununulia kahawa ya wakulima. Fedha hii bado ni nyingi, benki yetu ya KFCB mtaji wake bado mdogo, haiwezi kutoa mkopo huu.
“Tunachofanya ni kuijengea uwezo wa mtaji benki yetu ili kwa baadaye tuwe tunakopa huko. Na tumeanza kutenga fedha tangu mwaka jana ambapo tumeipa sh bilioni 1.5,” anasema Ngaiza.
Pamoja na mapato na matumizi hayo ya KCU kujadiliwa na kupitishwa na mkutano mkuu, kasoro kubwa iliyobainika katika utafiti ni uwepo wa elimu duni ya ushirika kwa wanachama.
Kanuni ya tatu ya ICA inawataka wanachama kushiriki katika shughuli za kiuchumi wakati ile ya tano inasisitiza elimu, mafunzo na habari mambo ambayo hayafanyiki kwa ufasaha na baadaye yanaibuka malalamiko kwa masuala waliyoyaidhinisha wenyewe.
“Ni kweli kwamba vitega uchumi hivi vinaingizia KCU mapato makubwa, lakini wakulima wa kawaida faida hii ni kama hawaioni badala yake wanadhani ni mali za viongozi,” anasema Yustas Elizeus.
Kutokana na elimu ndogo ya ushirika kwa wakulima, utaona kwa mfano misimu takribani tisa kuanzia mwaka 2002/03 hadi 2010/11, KCU imekuwa ikiendeshwa kwa hasara na mizania iliyokaguliwa imekuwa ikiwasilishwa kwenye mkutano mkuu na kuidhinishwa.
Mwaka 2002/03 kulikuwa na upungufu wa sh milioni 579.3; 2003/04 ziada milioni 61.3; 2004/04 ziada milioni 112.2; 2005/06 upungufu milioni 644.5; 2006/07 upungufu milioni 326.6 na 2007/08 upungufu milioni 959.7.
Mwaka 2008/09 upungufu milioni 392.3; 2009/10 upungufu milioni 634 na 2010/11 upungufu sh milioni 427.2.
Leopord Rweyemamu ni mmoja wa viongozi wa zamani wa KCU. Anasema kuwa tatizo kubwa lililopo kwa wakulima ni elimu ndogo ya ushirika na hivyo kuchagua wawakilishi wasio na uelewa kuingia katika mkutano mkuu.
“Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kagera, Nestory Sharos naye ni tatizo, anapaswa kuondolewa. Maana ameshindwa kutekeleza majukumu yake, badala yake amegeuka kuwa sehemu ya KCU kutokana na sheria mbovu ya ushirika sasa,” anasema.
Anabainisha kuwa mrajisi huyo pamoja na Shirika la Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (Coasco), ndio wanapaswa kukagua matumizi na mapato ya vyama hivyo pamoja na kumshauri waziri pale inapobidi.
Naye Method Kalikila anasema kuwa tatizo la wakulima kutofuatilia mapato na matumizi ya vitega uchumi vyao lilianza pale ilipoundwa KCU 1986 Ltd baada ya mfumo wa ushirika kubadilishwa na kuwekwa chini ya mrajisi na kisha kuundwa Bodi ya Kahawa.
“Huo ndio ulikuwa mwanzo wa utengano baina ya wakulima na uongozi. Maana ilionekana kama kampuni kwa kuwa wakati huo viongozi walikuwa wakichaguliwa kutokana na mfumo wa kisiasa wa jumuiya za chama tawala,” anasema.
Anasema kuwa tofauti na sasa, enzi za nyuma kulikuwa na utaratibu na misingi ya mali za wakulima kama nyumba na nyinginezo, na kupitia vitu hivyo watoto wa wakulima walisomeshwa.
Anaongeza kuwa kutokana na hali hiyo, viongozi wa KCU wamefanikiwa kubuni na kuanzisha mradi bila hata wanachama kushirikishwa, lakini baadaye wakaiidhinisha kwenye mkutano mkuu.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembris Kipuyo, anathibitisha uwepo wa matumizi mabaya ya mali za wakulima, akitolea mfano wa mgogoro unaoendelea katika chama cha msingi cha Kata ya Magata wilayani humo.
Mgogoro huo ni baina ya wakulima na mmoja wa wajumbe wastaafu wa Bodi ya KCU, Yusuf Kakwata ambaye anadaiwa kujimilikisha shamba la shule ya Kishoju mali ya KCU wakati akiwa mwenyekiti wa chama cha msingi Magata.
Kwamba baada ya kuletewa malalamiko hayo ambapo ofisa ushirika wa wilaya na mrajisi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Kagera walikuwa wakilalamikiwa, aliamua kuingilia kati kutafuta ufumbuzi ili kunusuru mali za wakulima.
Wakulima hao walimlalamikia mrajisi kuwa amekuwa kikwazo kikubwa hadi kufikia hatua ya kufanya ujanja wa kutaka kumkingia kifua mmoja wa wakulima wakubwa, Shakim Yahaya ili aweze kukopeshwa sh milioni 100 kutoka KFCB bila taratibu kufuatwa.
Sharos hakuwa tayari kukubali wala kukataa tuhuma hizo kwa kisingizio kuwa yuko nje ya ofisi kila alipotafutwa kwa simu na ofisini. Mara ya mwisho alipotafutwa alisema yeye si msemaji bali atafutwe katibu tawala wa mkoa.

0714717115
Next Post Previous Post
Bukobawadau