Bukobawadau

KILO 180 ZA DAWA ZA KULEVYA...Upo wapi usalama wa taifa?

MWANZO nilidhani ni uzushi; hata hivyo, baada ya muda wa kutafakari kwa kina na kuthibitishwa kwa uchunguzi na sayansi ya hoja (mantiki) imeniweka kwenye mazingira ya kutilia shaka ulinzi na usalama wa taifa letu juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya! Kilo 180 za dawa za kulevya si mchezo wa kuigiza kwenye tamthilia yoyote iwayo, isipokuwa ni ukweli uliothibitishwa kutokea kwenye nchi ambayo wengi wanaiita “kisiwa cha amani.” Kwa jinsi yoyote iwayo, ni dhahiri kwamba Tanzania si “salama” bali pia ni uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya!
Kupitishwa kwa kilo 180 kwa wakati mmoja kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu J. K. Nyerere (Dar es Salaam) kunanifanya niweke dhana kwamba “kuna uwezekano mkubwa Tanzania ina viwanda vidogo vidogo vya uchakataji na ufungashaji wa dawa za kulevya.”
Kama nilivyotangulia kuandika hapo mwanzo kwenye usuli, binafsi nilidhani kilo 180 za dawa za kulevya ni uzushi…; ni kweli na walioshiriki katika kupitisha mzigo huo mkubwa ni walinzi wa usalama wa uwanja wa ndege wa kimataifa (Dar es Salaam)! Usalama wa uwanja wa ndege ulikufa, na ulipwaya kiasi kikubwa kwa kulainishwa na ufisadi wa kimfumo; hii ni dhana ya kila mtu, siyo?
Kama ndiyo, upo wapi “usalama” wa taifa? Dhamira ya kuweka swali hili hapa ni kutaka kuonyesha ni kwa jinsi gani mfumo wa ulinzi na usalama ulivyoathirika na ufisadi wa kimfumo hata kuufanya mfumo wa ulinzi na usalama kushindwa kunusa na kubaini mbinu na mazingira yanayozunguka biashara ya dawa za kulevya kupitia uwanja wa ndege wa J. K. Nyerere (Dar es Salaam). Wako wapi wanausalama walioandaliwa kwa weledi, mbinu na mikakati ya ulinzi na usalama?
Dawa za kulevya ni hatari kwa “usalama wa taifa” kwa kuwa ni sumu inayowaangamiza vijana wa Tanzania na kutishia uhai wa taifa letu! Dawa za kulevya kwa vyovyote viwavyo ni hatari kwa usalama wa taifa kuliko hata hatari nyingine; kwa kuwa dawa za kulevya zinaharibu shakhsiya (haiba) ya vijana kimtazamo, kifikra na kifalsafa na kuwaacha wanaotumia na kuathirika na dawa za kulevya wakiwa mazezeta kama misukule isiyokuwa na thamani kwa nguvukazi ya taifa. Na kwa mtazamo huu, binafsi kama kijana wa Tanzania, nadhani vyombo vya usalama Tanzania hususan Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) vina wajibu usioepukika kushughulika na hatari hii.
Kazi ya kuzuia uingizaji, usafirishaji, usambazaji, uuzaji na utumizi wa dawa za kulevya ni wajibu usioepukika kwamba lazima taarifa za kiintelijensia zipatikane na zitumike udhibiti wake. Hivyo basi, ni wajibu wa Idara ya Usalama wa Taifa kufanya jitihada za makusudi katika kutafuta, kuoanisha (kulinganisha) na kutathmini taarifa za kiintelijensia katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Kwa wafuatiliaji wa masuala ya ulinzi na usalama na wale waliosomea fani za intelijensia na uchunguzi wanakubali juu ya ukweli kwamba ili uweze kuwa na mpango wa ulinzi na usalama wenye kuzingatia weledi wa hali ya juu katika kudhibiti hali ya hatari inayoweza kutokea pasipokutarajiwa, ni wajibu wa kiintelijensia kuwa na mikakati ya kuzuia kabla matukio hayajotokea. Kinyume chake, vyombo vya ulinzi na usalama vya uwanja wa ndege wa J.K. Nyerere vimepoteza uwezo wake wa ulinzi na usalama hata kuufanya kuwa uchochoro wa dawa za kulevya!
Katika mazingira ya kawaida ni muhali kudhani kwamba kilo 180 ziliweza kupitishwa na watu wachache kiasi cha watano au zaidi pasipo ushiriki wa watu wengi wenye nguvu ya aidha kisiasa, kiuchumi au kijamii.
Inasikitisha, na inatia huzuni unapoona idadi kubwa ya vijana wakiangamia kwa dawa za kulevya huku baadhi ya watendaji ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama wakishiriki kuwapatia ulinzi waagizaji, wasafirishaji na wauzaji wa biashara hii. Biashara hii, imekuwa maarufu sana Tanzania kama ilivyo duniani, hususani nchi za Amerika ya Kusini, Kati na nchi za Ulaya kama vile Hispania, Ugiriki, Italia na Uholanzi kwa sababu inaingiza fedha kubwa.
Wanaofanya biashara hii hawaifanyi bila uhakika wa kuwezeshwa na mfumo wa kitaasisi na wa kisheria; na ndiyo kusema, hata pale inapotokea wahalifu wanapokamatwa na vidhibiti vinavyotosha kuwatia hatiani na kuwapa adhabu inayostahiki kwa makosa yaliyoainishwa na sheria, kumekuwapo na hila za makusudi zinazofanywa na baadhi ya wenye dhamana ya ulinzi na usalama kuharibu vielelezo vinavyoweza kutumika kama ushahidi katika kuthibitisha uhusika wa watuhumiwa.
Kama mfano, dawa za kulevya kilo sita zilikamatwa lakini zikafikishwa kwa mkemia mkuu wa serikali zikiwa kilo 5 na nusu; hapa tayari ushahidi umeshaharibika; kwa kuwa “hati ya mashitaka” itaandikwa kilo 6 ilhali taarifa ya vipimo vya mkemia mkuu wa serikali vitaonyesha pungufu ya nusu kilo! Ushahidi maana yake hautakuwa umekamilika na kwa kuwa hukumu za kisheria hutolewa kwa mujibu wa “kuthibitisha pasipokuwa na shaka yoyote;” watuhumiwa wamekuwa wakiachiwa pamoja na kukamatwa. Au wakati mwingine ushahidi uliokamatwa ulikuwa “cocaine” badala ya kukaa kwa muda na mtuhumiwa kufikishwa mahakamani, ushahidi unageuka majivu au sukari!
Kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye mfumo wa kitaasisi, ni wajibu kwa wenye dhamana ya kutafuta, kusanifu, kupembua, kutathmini taarifa za kiintelijensia na kulifanyia kazi suala la kuongezeka kwa biashara ya dawa za kulevya Tanzania. Nchi inapelekwa kwenye msongo wa tamaa ya utajiri wa haraka kwa njia za mkato.
Kuna mambo yanayofichwa juu ya nani wanaoshiriki kwenye biashara hii? Wapo wanaojisifu, kwa kuwa biashara hii inafanywa na “mapedeshee”, na wapo wanaosema juu ya ushiriki wa viongozi wa kisiasa, kijamii na kitaasisi wanaoshiriki katika kuwapatia ulinzi wahusika wa dawa za kulevya. Kwanini biashara hii ishamiri kwenye mazingira ambayo ulinzi na usalama ni mkali? Pamoja na dhana ya kuwa na ulinzi na usalama unaosimamiwa na taasisi zilizopewa mamlaka kisheria, hakuna matokeo mazuri kwenye kudhibiti biashara hiyo hadi pale njia za zimamoto zinapotumika.
Tumeshindwa kuzuia; badala yake tunawekeza kwenye mapambano ya zimamoto dhidi ya dawa za kulevya. Kama tungalikuwa na akili timamu na kufanya uamuzi makini kwenye ulinzi na usalama wa taifa letu, tungaliwekeza katika kutafuta taarifa za kiintelijensia kutoka kwenye mzunguko na mnyororo wote wa ugavi wa dawa za kulevya kutoka kwenye asili (chanzo) hadi kwa mtumiaji wa mwisho.
Ulinzi na usalama wa taifa si kwa viongozi pekee. Kama ulinzi na usalama wa viongozi wa juu wa serikali hususan rais, makamu wa rais na waziri mkuu umepewa kipaumbele cha juu, hivyo hivyo vijana walitakiwa walindwe dhidi ya dawa za kulevya kwa kuwa ndilo kundi hatari sana kuathirika na ndiyo anguko na angamizo la kizazi cha sasa na cha baadaye. Vijana wanaoathirka na dawa za kulevya hawatakuwa na uwezo wa kulitumikia taifa; na hii ndiyo hatari kubwa kuliko hatari zote zinazolikabili taifa.
Tumekuwa tukishuhudia mitaa yetu wakiibuka matajiri wasiokuwa na kazi maalumu. Utajiri huu ndio unaowavutia vijana kwenye biashara hiyo, na ndio zinazowavutia baadhi ya watendaji wa ulinzi na usalama katika biashara hii.
Tanzania imepata sifa mbaya! Dawa za kulevya zimeliingiza taifa kwenye hatari ya kutambuliwa kama taifa linaloongoza kwenye upitishaji au chanzo cha dawa za kulevya. Na kwa jinsi hiyo, heshima ya nchi imeshuka, hadhi na utu wa wananchi wa Tanzania wanaposafiri kwenda nchi za ng’ambo umeingia doa. Kila msafiri raia wa Tanzania anaposafiri na kuingia kwenye nchi za kigeni anachukuliwa kama mhalifu wa dawa za kulevya!
Usalama wa taifa ubadilishe mbinu za utafutaji wa taarifa; na kwa hiyo, taarifa za kiintelijensia zinahitajika zaidi katika kuzuia biashara ya dawa za kulevya. Tunaweza kuendesha vita dhidi ya dawa za kulevya, kwa kuwashirikisha wazalendo wa nchi katika kujenga mazingira ya kupatikana kwa taarifa sahihi na makini za kiintelijensia. Kama tukishindwa sasa kwenye mapambano ya vita hii, basi usalama wa Tanzania upo hatarini – kifo cha nguvukazi na rasilimali watu – ndiyo kitakuwa kifo cha Tanzania siku zijazo!
NaBakari Mohammed
+255 713 593347 maligwa1968@yahoo.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau