Bukobawadau

PICHA YA SHEIKH ISSA PONDA ; HOSPITAL MUHIMBILI


na Shehe Semtawa
WAKATI Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa, akilazwa katika Kitengo cha Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kutibiwa jeraha alilodai kupigwa risasi na polisi, jeshi hilo limemruka.
Licha ya polisi kukwepa kumjeruhi kiongozi huyo, taarifa zinadai kuwa yalikuwepo mawasiliano baina yao mkoani Morogoro kuhusu Ponda kuhudhuria mhadhara ulioandaliwa na taasisi ya masheikh.
Akizungumza hospitalini hapo jana, mpwa wa Sheikh Ponda, Is-haq Rashid alidai mjomba wake hakuwahi kupata wito wowote wa kuhitajika polisi kabla ya tukio la kupigwa risasi.
Alisema kuwa hata waliposikia taarifa za kutafutwa kwake katika vyombo vya habari walimuuliza Sheikh Ponda kama alishapewa taarifa hizo kisheria.
Alifafanua kuwa Ponda aliwaeleza kuwa hajawahi kupata wito wowote kutoka polisi wala ujumbe wa kuitwa kupitia kwa mwanasheria wake hali iliyomfanya aendelee na ratiba yake ya kutembelea misikiti mbalimbali baada ya kutoka gerezani.
Mpwa huyo aliongeza kuwa katika kudhihirisha Ponda hakuwa mtu wa kujificha kama ilivyoelezwa na polisi, siku ya Idd Mosi alishiriki mhadhara wa wazi kwenye msikiti wa Kichangani na siku iliyofuata aliwasili mkoani Morogoro huku polisi wakiwa na taarifa zake.
“Walioandaa mkutano waliwaeleza polisi mkoani Morogoro juu ya Sheikh Ponda kuhudhuria na kuwa mgeni rasmi.
“Sasa tunashangaa kwa nini walitumia njia hiyo ya kumpiga risasi kwa kweli hatujui dhamira yao ilikuwa ni ipi,” alisema Is-haq.
Aliongeza kuwa baada ya Ponda kupigwa risasi kulikuwa na mabishano baina ya mfyatua risasi hiyo aliyevalia kiraia na askari waliovaa sare hali inayowathibitishia kuwa risasi hiyo ilitoka kwa mmoja wa askari waliolizunguka gari alilopanda mjomba wake.
“Kinachotusikitisha ni kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, kuwa ndugu yao hakupigwa risasi na polisi na wala jeshi hilo halimjui aliyerusha risasi hiyo,” alisema.
Akielezea tukio hilo, Is-haq alisema baada ya Ponda kumaliza mhadhara na kuondoka, magari matatu ya polisi yaliizingira gari lake hali iliyomfanya atelemke.
Baada ya kutelemka, mmoja wa askari alimpiga risasi iliyomfanya aanguke chini na muda huo kukawa na mgongano baina ya mrushaji na wenzake kisha watu walimuokota Ponda na kumuwahisha hospitali ya mkoa wa Morogoro.
“Alipofikishwa hospitali askari walikuwa wengi na kwa kuwa wananchi walioshuhudia tukio lile walishakuwa na wasiwasi, alitolewa pale na kupelekwa katika zahanati binafsi kabla ya kufikishwa jana MOI, Muhimbili, Dar es Salaam,” alisema.
Is-haq alidai kuwa baada ya tukio hilo polisi waliweka ulinzi na kukagua kila gari lililokuwa likielekea jijini Dar es Salaam na kwamba hata wao walikuwa katika hali ya taharuki bila kufahamu alipo Ponda hadi walipopigiwa simu jana kuwa yuko Magomeni katika moja ya teksi.
Kwa mujibu wa mmoja wa wafanyakazi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, Ponda amepasuka mfupa mkubwa wa upande wa mkono wa kulia ambapo kwa wakati huo ulikuwa ukifanyiwa upasuaji.
Polisi waruka
Msemaji wa polisi, Advera Senso, katika taarifa yake kwa vyombo vy habari alisema kuwa kongamano hilo lilifungwa saa 12:05 jioni amabpo watu walianza kutawanyika na baadhi yao wakiwa wamezingira gari dogo alilokuwa amepanda Sheikh Ponda.
“Baada ya kutoka eneo hilo, askari walilizuia gari hilo kwa mbele kwa nia ya kumkamata Ponda ambaye mpaka sasa anatuhumiwa kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi sehemu mbalimbali nchini yenye lengo la kuvunja amani.”
“Baada ya askari kutaka kumkamata, wafuasi wake waliwazuia kwa kuwarushia mawe askari. Kufuatia purukushani hiyo, askari walipiga risasi hewani kama onyo la kuwatanwanya,” alisema.
Senso aliongeza kuwa katika vurugu hizo, wafuasi wa Ponda walifanikiwa kumtorosha mtuhumiwa huyo na kwamba sasa imethibitika yuko Muhimbili akitibiwa jereha katika bega linalodaiwa alilipata katika purukushani hiyo.
Alisema kuwa timu inayowashirikisha wajumbe kutoka jukwaa la haki jinai ikiongozwa na Kamishna Issaya Mungulu imeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Nao Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay – atul Ulamaa), umeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa habari za kushambuliwa na kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari jana, mwenyekiti wa umoja huo, Sheikh Suleiman Kilemile, alisema Hay-atul Ulamaa, inaumia, kushtusha na kuwa na fadhaa kama jamii nzima ilivyoshtushwa na matukio mengine kama hili hapa nchini.
Tukio hilo linaashiria kuwa waliolitenda hawaitakii mema amani ya nchi yetu.
Sheikh Ponda baada ya kujeruhiwa kwa risasi mbili.
Next Post Previous Post
Bukobawadau