Bukobawadau

TANZANIA ,RWANDA ZIIGE MFANO WA THEOLOJIA YA KUINGILIA

Privatus Karugendo

WAKATI tunaelekea kuchanganyikiwa kwa kufikiri kuwa kupigana vita na jirani zetu ndio jibu pekee la kuondoa kutoelewana kwetu; wakati viongozi wetu wa nchi zetu za Tanzania na Rwanda, wakitaka kuonyeshana uwezo wa majeshi yao, tunahitaji busara za ‘Theolojia ya kuingilia.’

Tunawahitaji viongozi wetu wa dini zote kusimama katikati na kuzuia hali ya hatari iliyo mbele yetu. Vita si kitu cha kushabikia, vita si muziki wala sherehe, vita ni kifo na vita ni adui mkubwa wa uhai, amani na utulivu.

Viongozi wetu wa dini waache tabia ya kubembeleza urafiki na kujikomba kwa viongozi wa nchi; wawe tayari kusema ukweli hata kama ni kuhatarisha maisha yao. Waache woga; wawe tayari kusema hapana kwa mambo ambayo yanatishia uhai na ustawi wa wananchi.

Haitoshi kwenda makanisani na misikitini kuombea amani, bali yanahitajika matendo ambayo kwa kiasi fulani, yanaweza kusababisha viongozi wetu kuchafua mikono na wakati mwingine kupoteza maisha yao kwa lengo la kuleta faida kubwa.

Ni wazi kwa upande wa Rwanda, viongozi wa dini wana historia mbaya ya kushindwa kuingilia kati wakati wa mauaji ya kimbari. Hili ni dosari na kovu la kudumu. Hata hivyo, Wanyarwanda wameendelea kuwa waumini wakubwa wa dini za Kikristu na Uislamu na kwa kiasi fulani, viongozi wa dini hizi wanasikilizwa na wanaheshimika.

Huu ni wakati wao wa kuhakikisha Rwanda inasimama na kustawi. Ni wakati wa wao kuhakikisha Rwanda ina uhusiano mzuri na jirani zake. Kwa kushirikia na viongozi wa dini wa Tanzania, wanaweza kutekeleza Theolojia ya kuingilia.

Theolojia ya kuingilia ni theolojia iliyoanzishwa na Dietriech Bonhoeffer, Mchungaji kijana raia wa Ujerumani, wakati wa utawala wa Hitler.

Kitu cha kujifunza katika theolojia hii ni misemo miwili ya kijana Bonhoeffer, aliyenyongwa kwa sababu ya kupinga utawala wa Hitler. Misemo hiyo miwili ni: “Ikiwa gurudumu limechomoka na linaendelea kugonga na kujeruhi watu, kazi ya kanisa isiwe kuendelea kuganga vidonda vya majeruhi kwa kufunga bandeji, bali kuchukua kigingi na kusimamisha gurudumu hilo.”

Msemo wa pili ni: “Kanisa likishiriki kusafisha chombo kichafu, ni lazima lijiandae kuchafuka mikono yake.”

Hitler, aliwaua mamilioni ya watu aliodhani ni chanzo cha matatizo ya uchumi wa Ujerumani. Viongozi wa dini walilazimishwa kula kiapo cha kumtii, na yeye akijiita Mungu wa duniani.

Ilipita miaka ya ukimya, ububu, kigugumizi na woga, Hitler akakubalika. Taasisi za dini zilikwepa mateso na kifo na kuamua kukaa kimya! Dietriech Bonhoeffer, alikatisha kimya hicho kwa kuanzisha Kanisa mafichoni.

Ingawa alinyongwa, lakini ushawishi na cheche alizozianzisha kupitia kwenye theolojia ya kingilia zilienea duniani kote. Lengo la theolojia ya kuingilia ni kwamba ni heri kuzuia kuliko kuponya. Tanzania, inaweza kuiga theolojia hii!

Wanatheolojia wanaandika vitabu vya kuiongoza jamii katika mambo ya imani ndani ya maisha ya siku, kwa kuzisoma alama za nyakati. Wanafundisha mashuleni na vyuoni ili kujenga imani pevu miongoni mwa vijana. Wanatheolojia wengine ni waanzilishi wa shule za mawazo (School of thoughts).

Na kwingine waliingia msituni na kupigana bega kwa bega na waasi waliokuwa wanakataa utawala wa mabavu katika nchi zao. Mfano mzuri, ni nchi za Amerika ya kusini. Katika nchi zilizoendelea wanatheolojia ni watu mashuhuri na wanaheshimika sana, maana dini umekuwa msingi mkubwa wa maendeleo katika nchi hizo.

Aidha, ikumbukwe kwamba wanatheolojia ndio kundi linalounda jumuiya ya viongozi wa kidini. Hawa ndio mapadre, mashehe, maaskofu, makadinali na mapapa.

Hawa wana nafasi kubwa ya kuliokoa au kuliangamiza taifa lolote lile. Kuna baadhi ya nchi viongozi wa dini wamekuwa ni msingi wa maendeleo, utulivu na amani.

Lakini pia katika nchi nyingine, viongozi wa dini wamekuwa chanzo cha vurugu. Hapa Tanzania, wanatheolojia wetu wamekuwa kimya na kubaki makanisani na misikitini, wakiendesha ibada za kuomba mvua, utulivu na amani.

Kwa sababu ya historia na ‘unyonge,’ wanatheolojia wa Tanzania, hawasikiki, wamejawa woga na wala si mashuhuri. Tunao mapadre, wachungaji, mashehe, maaskofu na kadinali.

Tunao wanaofundisha mashuleni na vyuoni, na wengine wanaandika vitabu, lakini ukiwabana kwa hoja nzito, wako tayari kuyakana hata maandishi yao wenyewe.

Kama anavyosema Frieder Ludwig, kwenye kitabu chake cha Church and State in Tanzania: Aspects of Changing Relations (1961-1994) London, 2001, Kanisa barani Afrika linatuhumiwa kwa kutotumia madaraka ya kusema, na hii ni kasoro ya matumizi ya madaraka.

Anadhani sababu kadhaa zinazuia Kanisa kusema kama; viongozi wa Kanisa wanaishi mbali na watu wanaopaswa kuwasemea, dhambi za Kanisa zisizotubiwa zinalizuia kusema; ustaarabu na uungwana wa kutunza urafiki, na Kanisa kutoguswa na yale linayopaswa kuyasemea.

Theolojia ya kuingilia, ingekuwa msaada mkubwa kwa kipindi hiki cha kuchanganyikiwa. Tunahitaji mtu wa kuweka kigingi na kulizuia gurudumu kuendelea kuleta majanga.

Tunahitaji mtu wa kuwa tayari kuchafua mikono yake ili kuleta amani na utulivu katika taifa letu hili. Tunahitaji mtu wa kusimama na kusema ukweli kwamba vita si kitu cha kutetea na kulinda uhai.

Viongozi wetu wa dini zote wana nafasi hii kubwa, wana nafasi ya kukutanisha Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame, ili kuweka kigingi na kuzuia gurudumu hili linaloelekea kuleta maafa katika nchi zetu za Rwanda na Tanzania.

Theolojia ya kuingilia, ni silaha pekee ya kutusaidia kuondoa tofauti hizi za marais wetu. Tunahitaji mtu wa kujitokeza na kuwaeleza marais wetu wa Tanzania na Rwanda kwamba magomvi yao, pamoja na ukweli kuwa yanaweza kuzua vita kati ya nchi hizi mbili, si magomvi ya wananchi.

Kwa upande wao, wananchi wanaendelea kushirikiana, Wanyarwanda wanawaoa Watanzania na Watanzania wanawaoa Wanyarwanda; biashara inaendelea kati ya Watanzania na Wanyarwanda, na la muhimu zaidi ni uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizi mbili.

Hivi sasa vigezo vinavyotumika kuwatambua wahamiaji haramu, na hasa wale wa kutoka nchi jirani ya Rwanda, ni vya kiunyanyasaji na vinakiuka haki za binadamu.

Kuzungumza Kinyarwanda, haina maana mtu ni Mnyarwanda. Kuwa na sura ya Kitutsi, haina maana mtu ni Mnyarwanda. Kuwa na ndugu na jamaa Rwanda, haina maana mtu ni mnyawanda.

Hata hivyo, mipaka hii tuliyonayo iliwekwa mwaka 1885! Kabla ya hapo, mkoa wa Kagera ulikuwa sehemu ya Ufalme wa Bunyoro Kitara. Historia hii haijafutika hadi leo hii.

Kuna Watanzania wana jamaa zao Uganda, Rwanda na Burundi. Kesho kutwa, sote tutakuwa kwenye Shirikisho la Afrika ya Mashariki. Kwanini basi, tufukuzane na kutishiana maisha?

Tunahitaji viongozi wa dini shupavu kuelezea ukweli huo hapo juu. Kuwaeleza viongozi wetu kwamba alama za nyakati, zinatudai kuungana zaidi badala ya kutengana na kubaguana. Kwa vile ukweli huu waweza kuwa mgumu kupokelewa, kuna haja kubwa kufuata mfano wa Theolojia ya kuingilia.
Next Post Previous Post
Bukobawadau