Bukobawadau

Sumu ya nyuki inavyoangamiza VVU


Wengi tunafuga nyuki, tunakula asali lakini hatujui kama nyuki wana faida zaidi ya hizi hapa.
Wanasayansi kutoka chuo kikuu cha tiba Washington, Marekani  wamegundua katika utafiti wao kuwa sumu iliyopo katika mwili wa nyuki iitwayo toxin melittin inaweza kuvivunjavunja na kuviharibu virusi vya Ukimwi pasipo kuacha madhara katika chembehai za mwili.
Habari hii imeelezwa katika taarifa ya tiba za dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi iliyotolewa mapema mwaka huu.
Watafiti hawa wanaeleza kuwa matokeo ya utafiti huu kufika katika hatua kubwa inayoleta matumaini ya kupamba na VVU  kwa kuweza kupata dawa ya kupaka ya majimaji ndani ya uke itakayotumika kupambana na maambukizi ya VVU.
Dk Joshua Hood anasema: “Matumaini yetu ni kwa maeneo ambayo hali ya maambukizi yapo juu na vigumu kuzuilika, dawa ya majimaji mazito inaweza kutumika kupaka ndani ya uke katika kuzuia maambukizi ya mwanzoni kabisa.”
Sumu ya nyuki, melittin, imeonyesha uwezo wa kupambana na VVU kwa kuvunja ganda linalomzunguka kirusi na virusi wengine kwa kulitoboa na kuacha matundu.
Mwandishi mwandamizi wa makala za biokemia,  Dk Samuel Wicline, Profesa wa Biochemia wa Taasisi ya Russel Hornsby anafafanua kuwa kuwa vijipande vidogo vilivyoshindiliwa vya sumu ya nyuki vimeonyesha kuwa na tabia ya kuweza kuua chembe hai zenye saratani.
Anaeleza mtaalamu huyo kuwa hii si mara ya kwanza katika ugunduzi wa tiba ya namna hii, kwani mwaka 2004 wanasayansi wa Croatia walitoa taarifa yao katika jarida la sayansi ya chakula na kilimo kuwa mazao ya nyuki, ikiwamo asali na sumu ya nyuki  vina uwezo wa kutumika kutibu na kuzuia saratani.
Chembehai za mwilini zenye afya huendelea kubaki salama pasipo kupata madhara wakati wa tiba kwani sumu hiyo ya nyuki imetengenezewa na kitu kama ngao ambayo ikikutana na seli za mwili hudunda na kwenda mbali bila kujishikiza.
Hii ni kwa sababu ya seli za mwili ni kubwa kimaumbille kuliko sumu ya melittin, wakati kwa  virusi vya Ukimwi ni vidogo kuliko melittin, hivyo ikikutana navyo ngao hiyo haiwezi kuzuia kirusi kidunde kwani ni kidogo, hivyo  kirusi hudakwa na melittin na kushikamana, hivyo kirusi huweza kuharibiwa.
Dk Hood anaeleza kuwa vijipande vilivyoshibishwa na sumu ya melittin huweza kushikamana na kirusi na kutoboa tundu katika ganda la kirusi na kuchana ganda lote, hivyo kirusi huweza kuvunjwa.
Wakati tiba kwa kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU, yaani ARVs zinafanya kazi kwa kuzuia uwezo wa virusi kujidurufisha, kwa tiba ya melittin hushambulia sehemu muhimu ya kimaumbile ya  virusi ambayo ndiyo nguzo imara kwa virusi.
Tatizo katika tiba ya kuzuia uwezo wa kirusi kujidurufisha ni kuwa maambukizi yanakuwapo na hayakomi mwilini, hivyo hayazuii maambukizi kuwepo mwilini.
Baadhi ya vipande vya virusi vya Ukimwi vimepata uwezo wa kujibadili hivyo kuzuia ufanyaji kazi wa ARVs na hivyo kuendelea kuzaliana na kuvamia seli za mwili.
Mtaalamu huyo anaeleza: “Tunashambulia sehemu ya kimaumbile ya kiurithi ya VVU, kinadharia, tunasema hakuna namna yoyote ya kirusi kuweza kujibadili ili kukabiliana na mazingira mapya ya kujihami na mashambulizi ya tiba hii ukilinganisha na mashambulizi ya ARVs’ kirusi kitahitaji kuwa na ganda la kujikinga lenye ngozi  ya tando mbili ili kuweza kujibadilisha.
Dk Hood anaamini kuwa sumu ya nyuki iliyoshibishwa vijipande vya melittin ina uwezo wa kitiba wa aina mbili katika kutibu na kuzuia, moja ikiwa kutumika kama maji mazito ya kuweka ukeni (vaginal jelly) ili kuzuia maambukizi ya VVU kuenea .
Tiba ya pili ni kutumika kwa maambukizi ambayo tayari yapo mwilini hasa kwa maambukizi yaliyoleta usugu wa dawa, kinadharia ni kuwa kama sumu ya melittin itadungwa mwilini na kuingia katika mzunguko wa damu inaweza kuviangamiza virusi vya Ukimwi.
Anaeleza Dk Hood kuwa, “Kimsingi, vijipande hivi vya tiba vilivyotumika vilianza kufanyiwa majaribio ya kimaabara miaka mingi iiliyopita ikiwa kama zao la damu bandia ya kutengenezwa maabara.
Hata hivyo, haikufanya vyema katika kubeba na kusambaza hewa ya oksijeni, lakini ikawa ikizunguka katika mzunguko wa damu ikiwa salama mwilini na hivyo ilitupa mwanga wa kuweza kupata mbinu mpya ya kupambana na maambukizi ya aina tofauti.”
Melittin inashambulia tando mbili za ngozi laini pasipo kutofautiana, hii inaifanya melittin iwe dawa yenye uwezo wa juu kitiba katika mapambano dhidi ya maambukizi VVU.
Virusi kama Hepatitis B (homa ya ini) na C ambavyo navyo vina ganda la kuwakinga la namna hii navyo vinakuwa miongoni mwa virusi vinavyoweza kuangamizwa na tiba ya melittin.
Pia, majimaji mazito (jelly) ya melittin pia huenda yakalenga mbegu za kiume. Mtafiti Hood anaeleza kuwa inaweza kutumika kama dawa za kuzuia mimba, hivyo kuwa kama njia ya uzazi wa mpango. Hata hivyo, bado hawajalifanyia kazi.
Pia, wanaangalia uwezekano wa wenza wawili ambao mmoja wao aliyeambukizwa VVU pale watakapohitaji kupata mtoto aliye salama, kwani vijipande hivyo vya melittin ni salama kwa mbegu za kiume kwa sababu hiyohiyo ni salama pia kwa seli za ukeni.
Dk Hood anasema bado ni mapema mno kwani mpaka sasa majaribio yote ni ya kimazingira ya kimaabara. 
Next Post Previous Post
Bukobawadau