Bukobawadau

WILAYANI KARAGWE WANANCHI WAMSUSA MBUNGE WAO • WADAI ALIPORA USHINDI KWA MTUTU WA BUNDUKI

na George Maziku

MBUNGE wa Karagwe, Gozbert Blandes (CCM), ameshindwa kufanya mkutano wa hadhara katika mji wa Kayanga, wilayani humo baada ya kukosa wananchi wa kuwahutubia.

Blandes alipanga kufanya mkutano wa hadhara mjini Kayanga Jumamosi ya Agosti 3, mwaka huu, lakini alilazimika kuuahirisha baada ya mahudhurio ya wananchi kuwa hafifu.

Dalili za mkutano huo kutofanikiwa zilianza kuonekana siku moja kabla wakati mtu aliyekuwa akitangaza taarifa za kuwepo kwa mkutano huo kusema: “Wale waliokuwa wakisema Blandes hawezi kufanya mkutano Kayanga waje wajionee.”

Kauli hiyo iliashiria kuwepo shaka kwa waandaaji wenyewe kuhusu kufanikiwa kwa mkutano huo.

Akitoa taarifa za kuahirishwa kwa mkutano huo, Katibu wa CCM wilayani humo, Anatory Nshange, alidai kuwa Blandes asingefanya mkutano kutokana na kuwepo kwa shughuli ya bomoa bomoa ya nyumba mbili za wananchi katika eneo la Mgakorongo mjini hapa.

Hata hivyo, katibu huyo hakueleza uhusiano wa mkutano wa mbunge na bomoa bomoa, hasa ikizingatiwa kuwa nyumba zilizobomolewa ni za wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadena).

“Ndugu wananchi wa Kayanga, leo tulipanga kufanya mkutano wa mbunge wetu hapa mjini Kayanga, lakini tumeamua kuuahirisha kwa sababu kumejitokeza bomoa bomoa kule Mgakorongo.

“Tunawaomba radhi sana kwa usumbufu wowote, lakini tunawaahidi tutaandaa mkutano mwingine na tutawataarifu,” alisema Nshange.

Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa kuahirishwa kwa mkutano huo kunatokana na kukosekana watu hali iliyosababishwa na mgogoro wa kisiasa ulioibuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kufuatia utata wa matokeo yaliyompa ushindi Blandes.

Wananchi wengi wa jimbo la Karagwe wanaamini kuwa Blandes hakushinda uchaguzi huo na kwamba alipora ushindi wa aliyekuwa mgombea wa CHADEMA kwa kusaidiwa na Jeshi la Polisi wilayani humo.

“Huyu si mbunge wetu; mbunge wetu ni wa CHADEMA. Blandes alipata ubunge kwa kutumia mitutu ya bunduki za polisi na mabomu ya machozi.

“Hatuwezi kwenda kumsikiliza mtu aliyeingia madarakani kwa njia za mabavu kwani kukubali kumsikiliza ni sawa na kukubaliana na kuhalalisha uporaji wa kura aliofanya mwaka 2010,” alisema mwananchi mmoja.

“Hatuwezi kwenda kumsikiliza mtu ambaye aliwaagiza polisi kutufyatulia risasi za moto na kutupiga mabomu mwaka 2010. “Kwa nini tukamsikilize mtu aliyekusudia kutuua? Akawahutubie hao polisi wake,” alieleza mwananchi mwingine ambaye pia hakutaka kuandikwa jina gazetini.

Alipotafutwa mbunge huyo kuzungumzia sababu za kuahirishwa kwa mkutano wake, alikanusha kupanga kufanya mkutano huo kama ilivyotangazwa na viongozi wake wa chama.

“Siyo kweli! Sijapanga wala kuandaa mkutano Kayanga, kama hao viongozi wa CCM wamesema kuwa nimepanga kuhutubia hapo hawakuwa wakweli.

“Labda wao walipanga na walitaka kupata watu kupitia kwangu. Naomba uniamini mimi maana ubunge wangu hauna ubia na mtu yeyote,” alisem Blandes na kudai kwa sasa yuko nchini Uganda.
Next Post Previous Post
Bukobawadau