Bukobawadau

Kagera yailaza Kusini Pemba 2-1 ufunguzi wa Copa Coca-Cola

TIMU ya soka ya Kagera Wavulana chini ya miaka 15 ya Copa Coca-Cola imeanza vema fainali za taifa baada ya kuifunga Kusini Pemba mabao 2-1 kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam jana.

Baada ya mashambulizi ya kila upande, Kagera walipata bao la kuongoza dakika ya 16 likifungwa na Najimu Mugisha baada ya kuwazidi mbio mabeki wa Kusini Pemba na kuachia shuti lililomshinda kipa Mohamed Ally.

Kusini Pemba walirudi kwa kasi kipindi cha pili na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini washambuliaji wao hawakuwa makini na kujikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 76 baada ya kutokea piga nikupige na Farou Aben kutupia mpira kambani.

Ally Juma Kombo, aliipatia timu yake ya Kusini Pemba bao pekee la kufutia machozi dakika ya 88.

Katika uwanja huohuo, ilipigwa mechi ya wasichana iliyowakutanisha Ilala na Dodoma, ambapo wenyeji walipiga mtu mabao 9-0.

Mabingwa watetezi Morogoro, walishindwa kuonesha cheche zao baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mjini Magharibi kwenye uwanja wa Tumbi Kibaha.

Mechi nyingine iliyochezwa jana asubuhi, iliikutanisha timu ya wavulana ya Kilimanjaro iliyowatambia Tabora kwa bao 1-0.
Next Post Previous Post
Bukobawadau