Bukobawadau

MAKALA YA PRIVATUS KARUGENDO JUU YA SAIDA KAROLI: Msanii machachari aliyezimika umaarufu kama mshumaa

Privatus Karugendo
SAFU yetu ya Mwanamama leo hii inamuangazia Saida Karoli, mwimbaji aliyevuma kwa nyimbo zake kama ‘Maria Salome’, ‘Kaisiki’, ‘Ndombolo’ na ‘Mimi Nakupenda’.
Karoli aliyejaliwa sauti nzuri ya kuimba na ufundi wa kupiga ngoma na kucheza, mashabiki wake walimbatiza jina la “Wanchekecha”.
Kwa wale waliofahamu lugha yake ya Kihaya, walifurahia sana maneno yake, lakini hata na wale wasiofahamu lugha hiyo, waliweza kufurahia nyimbo zake ambazo utamu wake ni wa muziki na wala haufuatani na maana ya maneno; Kama vile tunavyocheza na kufurahi muziki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), bila kuilewa lugha ya Lingala, ndivyo na Karoli anavyotumbuiza na kupendwa na Watanzania, Afrika ya Mashariki na Afrika yote na hata nje ya bara hili.
Ingawa umaarufu wake ulidumu kwa muda mfupi na baadaye kuzimika kama mshumaa, hakuna ubishi kwamba alikuwa mwimbaji wa kwanza Tanzania kupata umaarufu mkubwa nje na ndani ya nchi.
Ni bahati mbaya kwamba mwanamama huyu hakuwa na elimu ya kutosha kuweza kupigania mafanikio yake; mapromota waliomwibua ndio walioamua ‘kumzima’ baada ya kuvuna kiasi cha kutosha kutokana na jasho lake.
Kwa kiasi kikubwa mafanikio yake yameshuka, lakini akisimama juu ya jukwaa na kuimba, sauti yake bado haina mfano. Ni sauti nzuri na ya kuvutia, ni sauti ya kisanii kwa vigezo vyote. Ni msanii anayeweza kuimba, kupiga ngoma na kucheza.
Ukiachia zile nyimbo zake za zamani zilizovuma, hata zile alizozitunga siku za hivi karibuni ni nzuri na zitabaki hewani miaka mingi.
Karoli hakupata elimu ya kutosha, lakini ni mtu mwenye akili nyingi na anajifunza haraka. Alipoibuka na kuiteka anga ya muziki ya Tanzania na nchi za jirani, alikuwa anafahamu lugha ya Kihaya peke yake.
Hakuweza kuongea vizuri Kiswahili. Lakini baada ya muda, aliweza kuzungumza lugha hiyo, na hata Kingereza.
Ushabiki mkubwa ulioonyeshwa kwa Karoli ungekuwa wa faida kubwa, kama wale wote walioonyesha kumshabikia wangesaidia kumuendeleza, labda kiwango chake kingebaki juu na leo hii tungekuwa na mwimbaji wa kimataifa.
Kwa njia moja ama nyingine, sote tumeshiriki kumshabikia Karoli na kumsindikiza kwenye anguko lake. Hii si tabia nzuri kwenye jamii yetu ndiyo maana safu hii inawatafuta wanawake wenye mchango chanya katika jamii na kuandika habari zake.
Kwa njia hii tutawainua wanawake na kuwapatia moyo kuendelea kupambana na maisha.
Saida Karoli alizaliwa Aprili 4, 1976 mkoani Kagera. Ni msanii wa muziki wa asili ya Kihaya nchini.
Alipata elimu ya msingi mwisho darasa la tano tu ambapo ilibidi aache shule kutokana na kukosa msaada kutoka kwa baba yake ambaye hakuwa anaitazama sana elimu ya mtoto wake hivyo hakuweza kuendelezwa.
Karoli alikulia katika Kijiji cha Rwongwe mkoani Kagera na kutokana na mila za ukoo wake, wasichana walikuwa hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli za muziki.
Hata hivyo kwa vile mama yake alikuwa na kipaji cha muziki, alimpa moyo na kumfundisha masuala mbalimbali ya kimuziki.
Akiwa na miaka 20 mama yake mzazi alifariki dunia, lakini Karoli aliendelea kujijengea kipaji chake cha uimbaji na upigaji ngoma.
Alikuwa akizunguka kijiji kimoja hadi kingine akipiga ngoma na kucheza na wakati mwingine akiambulia chupa ya pombe za kienyeji. Hakuweza kupata mafanikio makubwa kwa kuimba na kucheza kule vijijini.
Pamoja na ukweli kwamba aliimba vizuri, lakini uimbaji wake kwa wakati ule haukuweza kumletea kipato.
Kukua kwake kimuziki
Kipaji cha usanii wa muziki kwa Karoli kilijitokeza ghafla baada ya kujikuta akichukuliwa na kudhaminiwa na FM Productions Ltd waliokuwa mkoani Kagera wakitafuta wasanii wenye vipaji kwa ajili ya kuwaendeleza.
Ilimchukua Karoli wiki tatu tu kurekodi wimbo wake wa kwanza ambao ulipotoka uliishitua Tanzania nzima pamoja na nchi za jirani za Afrika Mashariki.
Albamu yake ya kwanza iliyozinduliwa Septemba 2, 2001 ilipata mafanikio makubwa na kupata umaarufu sana kwa kuwa ilikuwa na vionjo vingi vya kabila la Kihaya.
Ilijulikana kwa jina la ‘Maria Salome’ japokuwa mashabiki wake waliibatiza jina la ‘Chambua kama Karanga’ kutokana na maneno aliyokuwa anaimba katika wimbo ‘Maria Salome’ uliobeba jina la albamu.
Albamu hiyo ilifuatiwa na ziara kubwa alizokuwa anafanya katika nchi za jirani kama vile Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya ambako alipata mafanikio makubwa na kujikuta akibatizwa kuwa malkia wa nyimbo za asili.
Mara tu baada ya kutoa albamu yake, wimbo wa ‘Maria Salome’ ulipanda chati katika kumi bora za redio kadhaa nchini na kufikia namba moja ikishikilia nafasi hiyo kwa wiki sita mfululizo.
Nyimbo nyingine zilizotamba katika albamu hiyo ni pamoja na ‘Kaisiki’ na ‘Ndombolo’.
Baada ya miezi mitatu tu tangu kutoa albamu hiyo, Karoli alipata mwaliko wa kuimba Uganda akialikwa na Kabaka wa Buganda katika sherehe ya kiutamaduni kama mmojawapo wa wanamuziki waliofanikiwa Afrika na kujulikana sana Uganda na pia kumfanya kuwa mwanamuziki wa mwaka katika sherehe hiyo.
Kujulikana kwake kwa kasi kulisababishwa na matumizi ya lugha ya Kihaya, inayofanana zaidi na lugha ya Kiganda inayotumika na Waganda wengi, sauti nyororo na ya kuvutia na vionjo kibao vya kuvutia vya kijadi katika nyimbo zake.
Juni 2003 akatoa albamu nyingine nzuri iliyokwenda kwa jina la ‘Mapenzi Kizunguzungu’ na kuweza kuteka soko la muziki tena kwa mara ya pili kutokana na vionjo kama vya awali vya kijadi.
Hata hivyo Karoli ametoa shukrani zake za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu wa FM Productions Ltd, Felician Mutta kwa kuona kipaji chake na kumpandisha chati kama mmojawapo wa wanamuziki maarufu chini Tanzania.
Mutta alisema nia yake kwa msanii huyo ni kuona anajulikana na kushika chati za juu katika bara zima la Afrika na kuweza kufanya ziara za kimuziki nchi nyingi duniani.
Kutokana na uwezo alionao na kipaji katika masuala ya muziki, ni rahisi kugundua kuwa Karoli si kwamba ana kiwango cha kuweza kupata mashabiki wa muziki wake mbali na Tanzania na Afrika ya Mashariki tu, bali hata nje ya Afrika.


0754 63 3122
Next Post Previous Post
Bukobawadau