Bukobawadau

Mgogoro wa CCM Bukoba:Amani asema nipo tayari kumgharamia CAG

Meya wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Dk. Anatory Amani, amesema yupo tayari kumgharamia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh, ili kufanikisha utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

CC ya CCM iliagiza katika kikao chake cha mjini Dodoma wiki iliyopita, kwamba CAG akazikague hesabu za manispaa hiyo, ikiwa ni sehemu ya kutafuta ukweli utakaohitimisha mgogoro unaomhusisha Dk. Amani na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Dk Amani alisema uamuzi wa CC unapaswa kuheshimiwa na kwamba lilikuwa moja ya maombi yake (Amani) kwa tume iliyoongozwa na Abbas Kandoro.

“Tangu mwanzo mimi niliomba aletwe CAG  ili aangalie mambo yote zikiwamo hesabu za manispaa, na hata sasa bado ninamhitaji ndiyo maana ingewezekana kumgharamia, nipo tayari ili wananchi wasiendelee kupotoshwa,” alisema.

Kuhusu taarifa kwamba yupo mjini Bukoba akishiriki kuweka sawa hesabu kabla ya ujio wa CAG, Dk Amani, alisema tangu ahojiwe na vikao vya CCM mjini Dodoma, bado hajarejea mjini humo (Bukoba).

Alisema, aliondoka Dodoma Alhamisi iliyopita kwenda jijini Dar es Salaam aliposhiriki kikao cha Umoja wa Mameya na Viongozi wa Manispaa wa Kupambana na Ukimwi Barani Afrika (AMICAAL) ambapo yeye (Amani) ni Makamu Mwenyekiti.

Pia, akizungumza na NIPASHE jana, Dk. Amani alisema alikuwa anawasili mjini Shinyanga kushiriki kikao cha Umoja wa halmashauri zinazozunguka Ziwa Victoria ambapo yeye ni Mwenyekiti kwa upande wa Tanzania.

Dk. Amani alisema baada ya kutoka mjini Shinyanga, atarejea tena jijini Dar es Salaam kushiriki kikao cha Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT).

“Nimesikia kuhusu upotoshwaji unaofanywa dhidi yangu, lakini ninaamini baada ya CAG kutekeleza wajibu wake, ukweli utajulikana,” alisema.

Dk. Amani alisema hatua iliyofikiwa na CC ya CCM kutafuta suluhu ya kudumu kupitia kwa CAG, inapaswa kuungwa mkono ili mgogoro huo ufikie ukomo wake na kuruhusu wigo mpana wa shughuli za maendeleo kutekelezwa.

Mbali na kumtaka CAG kwenda kukagua hesabu za manispaa ya Bukoba, CC ya CCM iliwaagiza Dk. Amani na Kagasheki ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini, kurudisha utulivu wa kisiasa katika eneo hilo la ukanda wa ziwa Viktoria.
 
SOURCE: NIPASHE
Next Post Previous Post
Bukobawadau