AWAMU ya kwanza ya Operesheni Kimbunga, imemalizika na kufanikiwa kukamata wahamiaji haramu 12,704 waliokuwa katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita tangu ilipoanza Septemba 6 mwaka huu. Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Siro, alisema katika mikoa hiyo, wahamiaji haramu waliokamatwa walikuwa wametoka katika nchi za jirani na mataifa ya Asia.
Naibu Kamishina Siro alisema kuwa, operesheni hiyo iliwezesha kukamatwa kwa wahamiaji haramu 3,448 kutoka Rwanda, 6,125 kutoka Burundi, kutoka Uganda na DRC walikuwa ni 589, Somalia 44, Yemen mmoja na aliyekamatwa kutoka India ni mmoja.
Kwa mujibu wa Siro, jumla ya wahamiaji 194 walirudishwa na kupokelewa nchini baada ya kukataliwa na nchi zao.
“Hawa 194 wako kwenye ulinzi mkali wakisubiri hatua za kisheria kuchukuliwa kutokana na kukosa sifa za kuwa raia wa Tanzania na pia wamekosa sifa ya kuwa raia wa nchi jirani ambapo Serikali iliwapeleka baada ya vigezo vya kuwathibitisha kuwa ni raia wa nchi hizo kutokamilika,” alisema.
Akielezea Operesheni Kimbunga katika awamu yake ya kwanza, alisema wahamiaji haramu 2,129 walikubali kuondoka nchini kwa hiari yao na wengine 8,696 waliondoshwa nchini kwa amri ya Mahakama na wenzao 1,852 waliachiwa huru baada ya kuthibitisha uraia wao kwa Serikali.
Pamoja na kuwakamata watu hao, alisema wakati wa msako huo zilikamatwa silaha mbalimbali zilizokuwa zikitumika katika matukio ya uhalifu.
Naibu Kamishina Siro alieleza kuwa, pia walifanikiwa kukamata nyara za Serikali za wanyama kama ngozi za duma, swala na nyati.
Kuhusu changamoto zilizojitokeza, alisema ni pamoja na jinsi Watanzania walivyokuwa wakiishi na kushirikiana katika mambo mbalimbali na wahamiaji hao.
Ili kukabiliana na wahalifu, alisema Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, vimeagizwa kuanzisha kila mkoa kikosi kazi kwa ajili ya kufuatilia wahalifu sugu wanaotumia silaha za kivita na wanaowafadhili watu ambao wamekuwa wakijihusisha na ujambazi nchini.
Operesheni Kimbunga imemaliza awamu yake ya kwanza, kwa kuvishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, TAKUKURU, Jeshi la Magereza, Idara za Misitu, Mifugo, Uvuvi, na Wanyamapori.