Bukobawadau

Wahamiaji 6,000 wakamatwa Operesheni Kimbunga

na Ashura Jumapili, Bukoba
JUMLA ya wahamiaji haramu 6,809 wamekamatwa katika Operesheni Kimbunga iliyofanyika katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Katika operesheni hiyo iliyoanza Septemba 6, mwaka huu, pia silaha 22 na risasi 367 zilikamatwa katika mapori mbalimbali katika mikoa hiyo.
Mkuu wa Operesheni za Kipolisi nchini, Simon Sorro, ambaye pia ni Mkuu Msaidizi wa Operesheni Kimbunga, alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Kati, mjini Bukoba.
Kamanda Sirro alisema operesheni hiyo ni uendelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwa wananchi wakati wa ziara yake mkoani Kagera.
Alisema katika msako huo wa awamu ya kwanza unaotarajiwa kumalizika Septemba 20 mwaka huu, wamefanikiwa kukamatwa wahamiaji haramu 6,809 wakiwamo Wanyarwanda 1446, Warundi 4229, Waganda 647, Wacongo 443, Wasomali 42, Raia wa Yemeni mmoja na Raia wa India mmoja.
Alisema wahamiaji 2377 wamerudishwa makwao kutokana na maamuzi ya mahakama; 369 wameachiwa huru baada ya kufanya uhakiki wa kina, 1866 wamerudi kwa hiari katika nchi zao na 2170 wanaendelea kuhojiwa katika makambi mbalimbali.
Pia alisema katika operesheni hiyo walikamata suruali moja ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Burundi moja, kofia moja ya jeshi la Burundi. Vitu hivyo vilikutwa katika mapori ya Kimisi na Burigi, jambo ambalo amedai kuwa linaonyesha kuwa zilikuwa zikitumiwa na majambazi hao wakati wanapokwenda kuteka magari katika maeno mbalimbali.
Alitaja vitu vingine vilivyokamatwa katika msako huo kuwa ni ngozi moja ya duma, ngozi mbili za swala, vipande 10 vya nyama vinavyodhaniwa kuwa ni nyara za serikali, magogo 86, mitambo miwili ya kutengenezea magobole na fataki nane.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Issa Njiku, alisema kuwa operesheni hiyo inaendelea kufanyika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Kanali Njiku ambaye pia ni MKuu wa Wilaya ya Misenyi alisema operesheni hiyo imelenga kufanya uhakiki wa silaha, ili kuwabaini wanaomiliki kinyemela, wafugaji haramu, wanaojihusisha na ujangili ukiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha na kuwafikisha mahakamani.
Next Post Previous Post
Bukobawadau