Bukobawadau

MH JASSON RWEIKIZA (CCM) AISHAURI SERIKALI IWAFUNGULIE MILANGO WALIMU EAC

Serikali imeshauriwa kufungua milango kwa walimu wanaotoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufanya kazi nchini kwa masharti nafuu.

Hali hiyo imeelezwa kuwa itachagiza kasi ya kukabiliana na upungufu wa walimu uliopo nchini na hivyo kuboresha sekta ya elimu.

Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Brilliant ya jijini Dar es Salaam, Jasson Rweikiza, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya tatu ya shule hiyo.

Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), alisema pamoja na jitihada za uboreshaji wa elimu nchini, bado uhaba wa walimu umekuwa tatizo sugu linalokwamisha azma hiyo.

“Tunaweza kuboresha mazingira yote katika sekta ya elimu, lakini kama hatutakuwa na walimu wa kutosha, ni dhahiri kwamba ufundishaji utakwama na azma ya kupata matokeo bora ya wanafunzi haitafikiwa,” alisema. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja.

Rweikiza alisema mazingira yaliyopo sasa yanakabiliwa na vikwazo katika kupata vibali kwa walimu hasa wanaotoka nchi za EAC kufanya kazi nchini. Kwa mujibu wa Rweikiza, gharama za kibali kwa mwalimu mmoja kutoka nje, zinakadiriwa kufikia Shilingi milioni mbili.

Akizungumza katika halfa hiyo, Ngereja, pamoja na mambo mengine alisema wakati umefika kwa serikali kutilia mkazo namna bora za kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu.

Alisema changamoto hizo ikiwamo wa ukosefu wa walimu, zinakwamisha ama kurudisha nyuma jitihada za maendeleo ya nchi na raia wake.

Alitoa mfano kuwa hata ufanisi katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) utapatikana ikiwa sekta ya elimu itaboreshwa na kuwezesha kupatikana kwa wataalam.
Next Post Previous Post
Bukobawadau