Bukobawadau

TUNA KILA SABABU YA KUMUENZI NYERERE

Tuna kila sababu ya kumuenzi Nyerere
 
Na Prudence Karugendo
 
LEO ni miaka 14 tangu tutengane kimwili na mpendwa wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tumetengana naye kimwili, kwa maana ya kwamba hatuwezi kupata tena nasaha zake mpya, lakini kiroho na kimawazo tuko naye pamoja, sababu kila siku kupitia kwenye vyombo mbalimbali, redio, tv, video na hata kwenye magazeti tuko naye tukipata nasaha zake zisizochuja. Hiyo ina maana kwamba tutakuwa naye daima.
 
Mbali na Nyerere kuwa mmoja wa wapigania uhuru wa nchi yetu ya Tanganyika,  na kisha kuwa rais wa kwanza wa nchi yetu, Tanganyika huru, na baadaye rais wa kwanza wa Muungano wa Tanzania, yapo mambo mengi ya ziada tunayoyakumbuka na mengine kuyaona kwa macho yetu aliyowazidi warithi wake waliomfuatia. Mambo hayo hayana kingine cha kumuongezea Nyerere zaidi ya kumfanya aonekane ni Baba wa Taifa kwa maana halisi.
 
Hebu nikumbushe kidogo, muda mfupi baada ya Tanganyika kuwa huru, mwaka 1963, aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo, Jonh Fitzgerald Kennedy maarufu kama JFK, alimwalika Mwalimu Marekani na kumpa mapokezi makubwa ya kitaifa ambayo sidhani kama kuna rais mwingine wa nchi hii ambaye aliwahi kupata heshima kama hiyo nchini humo.
 
Hata Rais Barack Obama, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 2 ya kuzaliwa,  aliiongelea ziara hiyo ya Nyerere alipoitembelea Tanzania.
 
Siyo kwamba hakuna marais wengine wa Tanzania waliokwishatembelea Marekani, wapo, na wengine wameitembelea mara nyingi sana kuliko Nyerere, ila kauli ya Obama kuhusu ziara hiyo ilionesha kwamba ziara ya Nyerere ndiyo pekee imewekwa kwenye kumbukumbu ya taifa hilo kubwa duniani.
 
Katika picha za video za ziara hiyo ya Nyerere ya mwaka 1963, Nyerere anaonekana akitoa hotuba katika viwanja vya White House, Ikulu ya Marekani, baada ya kukagua gwaride la heshima pamoja na kupigiwa mizinga. Hiyo ni heshima ambayo Wamarekani hawaitoi kwa kila mgeni wao.
 
Katika hotuba hiyo Nyerere alisema kwamba Tanganyika ni nchi inayoundwa na jamii ya watu wa aina mbili, wenyeji na wahamiaji, akasisitiza kwamba watu hao wote wana haki sawa.
 
Hiyo maana yake ni kwamba Nyerere hakuwahi kuwa na fikra za kuwatimua watu nchini kisa eti wanatoka nchi nyingine.
 
Sababu zake za kufanya hivyo zilikuwa wazi, ni kwamba yeye alikuwa msitari wa mbele katika kupinga vitendo vyote vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanyika kuanzia Marekani mpaka Afrika Kusini vikiwa vimejikita kwenye tofauti za rangi na asili ya mtu.
 
Mpaka Nyerere anaaga dunia msimamo wake ulikuwa kwamba watu wanaojiita wazawa wa nchi hii wakiwabagua wengine kuwa ni wahamiaji ni makaburu tu. Akawa anasisitiza kwamba ukaburu sio rangi bali ni tabia ya mtu.
 
Jambo la kujivunia zaidi kwa Nyerere, mbali na hilo la kutuondolea kubaguana kwa rangi na asili, alitupatia heshima kubwa katika jumuiya ya kimataifa. Inakumbukwa kwamba baada ya ziara yake ya Marekani mwaka 1963, miaka 14 baadaye, mwaka 1977, alifanya ziara nyingine nchini humo akiwa amearikwa na rais wa Marekani wa wakati huo, Jimmy Carter.
 
Hata ziara hiyo ya pili rasmi ya Nyerere nchini Marekani ililifanya taifa hilo kubwa kuzizima likionesha kwamba kuna mtu mzito kalitembelea. Hiyo ilikuwa ni sifa na heshima ya pekee kwa nchi yetu. Tusimuenzi Nyerere kwa hilo tufanye kitu gani kingine?
 
Katika hotuba ya kumkaribisha Nyerere, Augast 4, 1977,  Rais Carter alisema maneno yafuatayo, “Miaka 14 iliyopita kiongozi kijana wa taifa letu, John Kennedy, alimkaribisha kiongozi kijana wa taifa jipya, Julius Nyerere, kwenye nchi yetu. Ilikuwa ni heshima kwa nchi yetu kutembelewa na kiongozi huyo mpya wakati nchi yake ina umri wa miaka 2 tu”.
 
Kwahiyo tunaweza kuona ni uzito kiasi gani aliokuwa akitupatia Nyerere, na tukitaka tunaweza kuulinganisha na uzito waliotupatia wengine ili kuona kama tunachokifanya kwa sasa, kumuenzi Nyerere, kinasababishwa na msukumo wa hisia tu au ukweli usio na ubishi wowote.
 
Kitu kingine ni kwamba Nyerere alikuwa ndugu kwa wananchi wote. Kila Mtanzania alikuwa ndugu yake wa kweli. Hakuwahi kuonesha tofauti yoyote kati ya ndugu wa tumbo moja na ndugu wengine wa kitaifa.
 
Halafu yeye alikuwa baba wa watoto wote wa nchi hii. Hakuonesha tofauti yoyote kati ya watoto wake wa kuwazaa mwenyewe na watoto wengine wa kitaifa. Hatukuwaona watoto wake wakiishi maisha yaliyo tofauti na ya watoto wengine wa kitaifa.
 
Kama ni shule watoto wake walisoma shule za kawaida sawa na walizosoma watoto wa wananchi wa kawaida, vivyo hivyo kwa vyuo nakadhalika.
 
Mwaka 1985, wakati Mwalimu anakaribia kustaafu, mmoja wa watoto wake alifanya vurugu katika sehemu moja ya sitarehe na kufikishwa katika kituo kimoja cha polisi. Askari kuona hivyo walichokifanya ni kupiga simu nyumbani kwa Mwalimu Msasani, bahati mbaya simu hiyo akaipokea Nyerere mwenyewe.
 
Nyerere aliwauliza askari hao kwamba ina maana kila mtu anayefanya vurugu na kufikishwa kituoni hapo askari hao wanampigia simu baba yake?
 
Tukiangalia tutaona kwamba hiyo ni tofauti kabisa na sasa hivi ambapo askari anayejitakia usalama ni vigumu kabisa kumweka chini ya ulinzi mtoto wa rais. Mtoto wa rais anaweza kufanya lolote analotaka na askari asifanye kitu.
 
Hiyo ni heshima nyingine ambayo Nyerere ameijengea hata familia yake mbali na aliyolipatia taifa. Inaonekana kwamba katika Afrika, watoto wengi wa marais wastaafu wanaishi maisha ya tabu, wengi wanaonekana wananyanyaswa achilia wale wanaotumikia vifungo vya muda mrefu na wengine kuuawa. Hiyo ni kutokana na watoto hao kuutumia vibaya muda ambao wazazi wao walikuwa vinara wa nchi zao.
 
Watoto wengi wa marais wa Kiafrika waliotumia vibaya muda wa wazazi wao kuwa Ikulu,  kwa kufanya mambo yasiyokubalika kijamii, wamejikuta katika matatizo makubwa baada ya wazazi wao kuondoka Ikulu. Ipo mifano ya Marehemu Wezi Kaunda mtoto wa Mzee Keneth Kaunda wa Zambia, Atupele Muluzi motto Bakili Muluzi  wa Malawi, ambaye yuko kifungoni, mtoto wa Abdoulaye Wade, rais mstaafu wa Senegal, Karim Wade,  ambaye naye yuko kifungoni nakadhalika.
 
Lakini mpaka sasa watoto wa Mwalimu Nyerere bado wanaishi kwa raha musitarehe kutokana na baba yao kutowaachia nafasi ya kufanya mambo yasiyokubalika kijamii. Hicho ni kitu kingine cha kumuenzi Baba wa Taifa.
 
Yapo malalamiko toka kwa baadhi ya watu wasiojua kuchambua mambo kwamba Nyerere aliufanya uchumi wa nchi udidimie! Cha kuangalia ni kwamba hata kama hoja hiyo ni ya kweli lakini hakufanya hivyo kwa lengo baya, hasa kwa yeye kujinufaisha binafsi kwa kujirundikia mali. Yeye alikuwa analenga kuwanufaisha wananchi wote badala mmojammoja kuonekana kama visiwa vya kijani katikati ya jangwa.
 
Katika kufanya hivyo alikataa kuingia katika mikataba ya kitapeli ambayo ingeweza kuwanufaisha wachache huku walio wengi wakitaabika. Mikataba ya kuzoa kila kitu kanakwamba baada ya kizazi hiki hakuna kizazi kingine, au mali ya nchi iliyopo chini ya ardhi na juu yake ni kwa ajili ya kizazi kilichopo peke yake.
 
Mfano kuhusu madini alisisitiza kwamba yabaki ardhini mpaka pale wananchi watakapokuwa na uwezo wa kuyachimba bila kutapeliwa, maana maliasili hiyo siyo ya wananchi waliopo kwa sasa peke yao, ni mali ya hata vizazi vijavyo.
 
Kuhusu rushwa inayowahangaisha watu kwa sasa, Nyerere alisema jinsi walivyokuwa wameitafutia dawa, kifungo na viboko, kuingia na kutoka gerezani, kwa wale waliojihusisha nayo. Hiyo haikuangalia ni mtu gani anayehusika.
 
Kwa upande wa demokrasia, tunajua Nyerere alivyoendesha nchi kwa mtindo wa chama kimoja cha siasa, lakini ulipofika wakati akaamini kuwa sasa Watanzania wanaiweza demokrasia ya vyama vingi alishauri iachiwe nafasi hata baada ya Watanzania, kutokana na upofu wa karibu miongo mitatu ya giza, asilimia 80 kusema kwamba wanataka chama kimoja.
 
Kuhusu uzalendo kwa chama chake cha CCM, chama alichokiasisi yeye mwenyewe, Mwalimu alikuwa anaamini katika nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu. Alikuwa anaamini katika kutumia hoja kukilinda chama badala ya kutumia polisi na risasi ili kukilinda.
 
Na baada ya vyama vingi kuwa vimeanzishwa, Nyerere alitamka kwamba chama ambacho anakiona kinaweza kuwa mbadala kwa CCM ni Chadema. Aliyasema hayo Chadema kikiwa bado hakijapata nguvu kama kilizo nazo kwa sasa. Huo ndio tunaweza kuuita unabii wa kisiasa alikokuwa nao Nyerere, je, tuna haki ya kutomuenzi mtu huyo?
 
 
Next Post Previous Post
Bukobawadau