Bukobawadau

Mwalimu Nyerere: Mwanamikakati wa Usalama wa Taifa

Katika kumkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuzienzi kazi za kimapinduzi alizozifanya kwa maslahi ya taifa letu na watu wake, kila mtanzania mzalendo atakubaliana nami kwamba katika kipindi kifupi sana cha miongo miwili historia imetuonyesha kwamba mambo mengi aliyoyasimamia Mwalimu yalikuwa sahihi ingawa yametelekezwa. Maandiko ya Mwalimu kuhusu Azimio la Arusha, siasa ya ujamaa na kujitegemea, elimu, afya, kilimo, viwanda, reli, bandari, ustawi wa maisha ya wananchi, utu, haki sawa kwa wote, nk na mafanikio yake yanauonyesha umahiri aliokuwa nao katika kubuni mikakati ya kulikomboa taifa, ingawa wapo vibaraka waliolishwa kasumba ya kibeberu, ambao wanazibeza kazi za Mwalimu kwani zinasuta dhamira zao juu ya ustawi Tanzania na watu wake.

Katika ulimwengu wa sasa tunashuhudia mataifa yanatikiswa na mengine yameangushwa na kumegwa vipande vipande na magaidi na majasusi ambao wamevunja ngome za ulinzi na usalama wa mataifa hayo. Mamilioni ya watu wasiokuwa na hatia wameuwawa. Duniani kote mapambano dhidi ya magaidi na majasusi yanaendelea kwa siri na wazi ili kulinda uhai wa watu na mali zao na ustawi wa mataifa. Hali hii si ngeni. Imekuwepo kwa miaka yote. Kwa Tanzania, Mwalimu Nyerere aliliweka mwanzo kabisa suala la usalama wa taifa ambao kimsingi ndio uhai wa Tanzania. Katika kumkumbuka Mwalimu nitaidurusu kazi aliyoifanya ya kuimarisha na kuulinda usalama wa taifa, pia nitatoa maoni yangu ya nini kifanyike katika juhudi za kuimarisha usalama wa nchi yetu katika ulimwengu huu wa kigaidi na kijasusi.

Historia inaonyesha kuwa Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere ilianzisha sera ya kutetea na kusimamia haki watu duniani kote pamoja na kuongoza harakati za kupigania uhuru wa Afrika. Kwa kuwa harakati hizi zililenga kumkomboa mwafrika aliyenyonywa na kukandamizwa na mabeberu, mataifa makubwa yenye maslahi yake katika nchi za kiafrika yaligeuka kuwa hasimu mkubwa kwa Tanzania na yalitumia kila mbinu za kijasusi na kigaidi kutaka kulihujumu taifa letu na hata kuipindua serikali. Tanzania ya Nyerere ilikuwa macho na iliwadhibiti magaidi na majasusi kutoka kwa makaburu wa Afrika Kusini, serikali ya Ian Smith ya Rhodesia, serikali za kikoloni za Kireno wote hawa wakiungwa mkono na mataifa makubwa ya magharibi. Majasusi kutoka kwa Nduli Idd Amini nayo yalithibitiwa. Hali ya sasa ya ugaidi na ujasusi duniani na tishio lake kwa usalama wa Tanzania yetu inafanana na hali tuliyokumbana nayo wakati huo. Mbinu za magaidi na majasusi ni zilezile -- kujipenyeza kwa siri na kuujua udhaifu wa mfumo wa ulinzi na usalama na wapi pa kupiga kwa urahisi -- na malengo yao ni yaleyale -- kutia hofu, kuuwa watu na kuhujumu miundo mbinu ili kutimiza malengo yao ya kisiasa.

Nini kiliifanya Tanzania kuushinda ugaidi wa ujasusi? Jibu ni mfumo imara wa ulinzi na usalama ambao ulikuwa ni jukumu la kila mtanzania -- mfumo wa shina la nyumba kumikumi. Hapa neno shina lilimaanisha pia maofisi na maeneo yote ya kazi, starehe nk ili mradi upo mkusanyiko wa watu. Jukumu la usalama wa taifa halikuwa jukumu la vyombo vya usalama peke yake. Watu walilelewa hivyo na kuishi hivyo. Kila raia alikuwa ni askari katika kaliba yake. Mfumo huu imara aliounzisha Mwalimu Nyerere uliifanya Tanzania kuwa na ngome imara ya kuwadhibiti maadui wa ndani na nje na kudumu katika amani. Kila waliothubutu kuingia nchini kufanya ujasusi na ugaidi walikamatwa na kurejeshwa makwao. Kila mpango wa kijasusi na kigaidi ndani ya nchi ulijulikana na kudhibitiwa mapema. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, KIITIKADI (kijamaa), watanzania walitambua kuwa Tanzania ilikuwa na maadui wa ndani na nje na kwamba utayari wetu, mshikamo na ushirikiano wetu katika kuilinda nchi yetu ndiyo ilikuwa ni silaha yetu kubwa. “Moyo kabla silaha” yalikuwa ni maneno ya hamasa kutoka kwa Mwalimu. Idara ya Usalama wa Taifa ilitanda kila kona ya nchi si kwa maana ya maofisa kutoka “Idara ya Usalama Taifa” bali kila raia mwema, mzalendo, mwenye nia safi juu ya nchi yetu alikuwa ni mwanaidara. Kwa kujipanga sawasawa kimkakati tuliwashinda maadui. Tanzania ilibaki salama na hatimaye nchi za Angola, Namibia, Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini zilipata uhuru wake.

Tanzania ya sasa bado inao maadui wa ndani na nje na inakabiliwa na changamoto kubwa sana katika kukabiliana nao.. Lakini la kusikitisha ni kwamba suala la usalama wa taifa linaonekana kuwa ni suala la vyombo vya ulinzi na usalama tu. Haya ni matokeo ya kutelekezwa kwa mfumo wa usalama tuliokuwa nao baada ya kulitumbukiza taifa katika mfumo wa uliberali mamboleo. Tanzania ya katika mfumo mpya wa uliberali mamboleo ikasahau kwamba bado inao maadui wa ndani na nje. Tanzania ikacha milango na madirisha wazi na hata paa ikaezua. Mfano ni wahamiaji haramu wanaingia na kutoka Tanzania wapendavyo. Twiga na ukubwa wake anapitishwa uwanja wa ndege. Majengo marefu yamejengwa karibu sana na Ikulu jambo ambalo ni hatari sana kwa Usalama wa Taifa. Kisa? Eti wameweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Ajabu sana! Tanzania ikawa kituo cha madawa ya kulevya. Ujangili na wizi wa kutumia silaha ukashamiri. Silaha za kivita zikatapakaa kila pembe ya nchi. Uhujumu uchumi ukawa ni njia kuu ya kujitajirisha. Tanzania ikaendeshwa na rushwa. Rushwa kidogo inawasahaulisha wenye dhamana athari za wahamiaji haramu (rejea hotuba ya Rais Kikwete akihitimisha ziara mkoani Kagera: http://www.youtube.com/watch?v=Pxsbyi82uxM) au madawa ya kulevya kwa taifa na vizazi vyetu. Matokeo yake tukaupa kisogo mfumo wetu mzuri na imara wa ulinzi na usalama wa taifa kuanzia shina la nyumba kumikumi, kwenda kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji au mtaa, kamati ya ulinzi na usalama ya kata, wilaya, mkoa hadi ngazi ya taifa.

Tukumbuke kwamba katika shina ndipo anakopatikana adui wa ndani na nje. Tunaanzia kidogo kwenye wilaya. Lakini nguvu zetu zote tumezielekeza kwenye ngazi ya taifa na mkoa. Kwamba kupitia kwenye kamati za ulinzi na usalama za taifa, mkoa na wilaya Tanzania iko salama. Kwa kweli tunajidanganya. Katika shina ndipo kila mmoja wetu anamfahamu jirani yake na nyendo zake na hata siri zake. Kupitia ufahamu huu taifa linaweza kumdhibiti yeyote yule kabla ya kuleta madhara uraiani au katika vyombo vya ulinzi na usalama. Hata kwenye nchi zenye teknolojia ya hali juu ambazo zimetandaza kamera kila kona na kufuatilia nyenendo za watu kwenye mitandao ya simu na intanet kama Marekani na Uingereza, mambo yakiwazidia huwa wanarudi kwenye mashina ili kukabiliana na hujuma za kigaidi na kijasusi. Nchi kama Cuba ambayo bado inautumia mfumo huu wa shina na imeweza kuwepo mpaka leo licha ya kuwa karibu sana hasimu wao mkubwa tena mwenye nguvu sana -- Marekani. Haiingii mtu Havana akafanya ugaidi na ujasusi. Ni ngumu sana tena sana. Wachina wana mfumo huu wa shina. Hapenyi mtu pale.

Nitumie fursa hii kusema kwamba katika kumuenzi Mwalimu basi turejeshe na tuimarishe mfumo huu wa usalama kuanzia kwenye shina. Kiitikadi (maana itikadi ndiyo inayozaa uzalendo) wananchi wahamasishwe na kushirikishwa zaidi katika usalama wa taifa katika mashina yote nchini na taarifa zao zisivujishwe kwani kufanya hivi ni kuhatarisha maisha yao hasa pale wanapotoa taarifa kuhusu watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Mwaka 2010 nilikutana na mzee mmoja mkazi katika mojawapo ya vijiji vinavyozunguka jiji la Mwanza akaniambia kuwa kuna wakati aliitikia wito wa serikali wa kutoa taarifa polisi za wanaomiliki silaha za moto kinyume cha sheria lakini alipotoa taarifa hizo kesho yake wale aliowataja wakamwendea na kumtisha kweli. Hayo ndiyo matokeo ya mambo kuendeshwa kwa rushwa. Kwa hiyo tuwe na mtandao wa siri mpana na maalum wa upashanaji habari za kiusalama kuanzia ngazi ya shina ambao utaiwekea Tanzania ngome imara kwamba anapoingia muhamiaji haramu, gaidi, jasusi kwenye kaya au eneo fulani, shina linakuwa na taarifa hizo zinafikishwa kwenye vyombo husika haraka iwezekanavyo. Au raia mwema akishuku au kuwa na taarifa kwamba mtu fulani katika kaya, ofisi, au kundi fulani ana nyenendo za kutiliwa mashaka, basi habari zake zipelekwe kwenye vyombo husika mara moja na uchunguzi wa kina ufanyike haraka ili kuujua ukweli na kumdhibiti kabla hajafanya madhara. Tukifanya hivi tutaudhibiti vilivyo ugaidi na hujuma za jiasusi za aina yeyote. Tusisubiri CIA na FBI ambao kimsingi hawako kwa ajili ya maslahi ya Tanzania yetu.

Wapo wanaoweza kusema mfumo huo wa kuwa macho kuanzia kwenye shina unaifanya Tanzania itawaliwe kipolisi (police state) na kwamba unawaminya uhuru watu. Jibu kwa wasemao hivi ni kwamba hakuna kitu kinachoitwa UHURU-HURU. Uhuru usio na mipaka wala wajibu haupo. Uhuru wa watu kuachwa wakapanga mipango ya kigaidi na kijasusi ya kuhujumu nchi ni uhuru wa kuleta maangamizi. Kama taifa hatuwezi kukubali kuona watu wasio na hatia wanauwawa. Kwa hiyo, mfumo huu wa kiusalama katika mashina ni njia sahihi, nyepesi na ya uhakika ya kupata taarifa za magaidi na majasusi na kuwadhibiti. “Kinga ni bora kuliko tiba,” wahenga wetu walisema. Kwa mfumo huu tutawadhibiti wauza madawa ya kulevya. Tutawadhibiti majangili. Tutawakamata wakwepa kodi. Tutajua nani ni nani, yuko wapi, na afanya nini katika kulihujumu taifa na tutachukua hatua katika wakati muafaka kumdhibiti na kutokomeza uovu wake. Na teknolojia simu za mkononi katika mfumo maalumu itatusaidia sana wananchi katika kufikisha taarifa kwa vyombo husika ili mradi tu siri za watoa taarifa hazivujishwi na vyombo husika. Pia tuangalie uwezekano kurejesha sheria ya kizuizini ili mradi iwepo haki, uadilifu, udhibiti na ulinganifu katika kuitumia ili isije kutumika kuwanyamazisha watu. Katika kumkumbuka Mwalimu tujadili kwa mapana na marefu na kujikumbusha historia ya nchi yetu na mafanikio yake na umuhimu wa mchango wa wananchi katika usalama wa taifa letu. Na wala asikudanganyeni mtu kuwa vita baridi ilikwisha. Bado ipo tena ni hatari zaidi. Kwa mfumo wa shina wa kuwashirikisha wananchi Tanzania itakuwa salama na amani yetu itadumu.

Mungu ibariki Tanzania.

Mungu udumishe uhuru na umoja wetu.

Ndugu yenu

Amani Millanga
Next Post Previous Post
Bukobawadau