Bukobawadau

Nini matilaba ya himaya hizi zinazoitwa dini kwa sasa?

Na Prudence Karugendo

SIKU moja nilikuwa kwenye mhadhara, mkutano wa kidini wa watu wanaofuata imani ya Kiislamu, dini ambayo chimbuko lake ni Asia ya Kati (Umangani), au Mashariki ya Kati kwa jiografia ya kidunia. Nikapewa fursa ya kuuliza swali lolote linalohusu imani ya dini kuu mbili zilizotamalaki mpaka kwenye eneo letu, Uislamu na Ukristu.

Kabla ya kuuliza swali nikaambiwa nitaje jina langu, nikataja, nikaulizwa madhehebu yangu nikasema Mhaya. Wahadhiri wakakataa kwamba wanachotaka ni madhehebu na siyo kabila, na mimi mikang’ang’ania kwamba madhehebu yangu ni Mhaya. Ndipo ikabidi tufafanuliane nini maana ya dini na madhehebu kulingana na upeo wa imani zetu tuliokuwa nao pamoja na ufahamu wa imani hizo.

Kulingana na imani yangu mimi binafsi, dini au kuabudu ni sehemu ndogo tu ya utamaduni mpana wa kila jamii. Historia ya dunia yetu inatueleza kwamba maelfu ya miaka iliyopita, binadamu wengi, kama sio wote, katika tamaduni zao mbali mbali, wamekuwa wakiamini kwamba kuna nguvu kuu isiyopimika, iliyo nje ya uwezo wao wa kukadiria, na iliyo juu ya kila kitu na inayoweza kuamua hatima yao na kila kitu kilichoponao ikibidi, pasipo wao kuwa na uwezo wa kuweka pingamizi. Mpaka hapa nilishawaonyesha kwa nini niitwe Mhaya na si Muislamu wala Mkristo.

Kanunu hii, ya kutambua na kuabudu nguvu hiyo kuu, waliyojipa wanadamu, ilitokana na kujaliwa uwezo wa kuwaaza na kufikiri, na ndiyo inayotofautisha maisha yao na ya wanyama wengine.

Kumbukumbu zangu zinaonyesha kwamba hapajatokea nguvu hiyo ya sehemu moja ikakinzana na nguvu ya aina ile ile ya sehemu nyingine. Hii imeleta ashirio kwamba nguvu hiyo ni moja iliyoenea kote.

Mfano, hakuna jamii isemayo kwamba kuiba ni kitu kizuri, kuuana ni kitu kizuri wala kufanyiana ubaya ni kuzuri kwa mujibu wa kila imani iliyo katika jamii husika.

Hapa nitazungumzia nguvu hiyo kwa upande wetu wa Afrika, au nisisiteze zaidi, kwetu sisi Waafrika weusi. Wahenga wetu waliishi kwa kuelekeza majaaliwa yao kwa nguvu hiyo kuu. Walitegemea kilimo chao, ufugaji wao, uvuvi wao, kuoa kwao, kufa kwao na kadhalika, vyote hivyo vifanikiwe kwa kudra za nguvu hiyo.

Ustawi wa maisha yao kwa ujumla uliitegemea nguvu hiyo na ndiyo maana hata walipotatizwa na mambo kadha wa kadha, walikuwa na njia za kuwasiliana na nguvu hiyo na kupata jawabu haraka, tofauti na ilivyo sasa.

Wakati wa majanga kwa mfano, kama mafuriko, njaa, ukame kimbunga, magonjwa ya milipuko na kadhalika, walikuwa na njia ya kuyanyoosha yote hayo kwa kuitegemea nguvu hiyo kuu. Waliweza kufanya ibada, matambiko, kutoa kafara (sadaka) na kurekebisha mambo yaliyokwenda tenge, yote yakiwa yameelekezwa kwa hiyo nguvu kuu, na baadaye madhila hayo yote yalikuwa yakitoweka.

Ni nguvu gani hiyo iliyojaa ukarimu wa ajabu namna hiyo? Bilashaka yoyote huyo ndiye Mungu, ambaye alizikubali dini hizo katika uasili wake na kuyasikiliza maombi ya watu wake pamoja na kuwapa majibu kila walipomwendea.

Kumbe dini tulikuwanazo. Sasa hawa wenzetu Warabu na Wazungu walituletea habari gani? Hapa panahitaji umakini ili kubaini hila iliyokuwa ndani ya misafara ya hawa maustadhi na wamisionari, walioleta haya mambo huku wengine wakidai kuwa walicholeta ni habari njema, kwa maana ya Injili.

Baadhdi ya malengo yao makuu yalikuwa kusambaza tamaduni zao pamoja na kupanua himaya zao, kutafuta makoloni, na kupata wajakazi wa kuwafanyia kazi zao nzitonzito bila ujira, watumwa.

Kuanzia karne ya kumi na sita Afrika ilianza kuvamiwa na wageni kutoka mabara mengine, hasa ya Ulaya na Asia ya kati. Msukumo mkubwa wa uvamizi huo ulitokana na kile kilichoitwa uvumbuzi wa ardhi mpya katika Amerika, maendeleo ya viwanda katika Ulaya na hali ngumu ya maisha katika Asia. Kwa hiyo Afrika iliyokuwa na wakazi wachache na eneo kubwa lenye utajiri mkubwa wa maliasili ikaonekana ndiyo sehemu muafaka ya kupatia suluhisho la mambo yaliyotajwa hapo juu.

Baadhi ya mbinu walizotumia wavamizi hawa katika kuiteka Afrika na wakazi wake ni pamoja na kupenyeza tamaduni zao za kiimani na kuwashawishi Waafrika kwa njia ya kuwalazimisha, ili waamini kwamba hizo ndizo dini alizokuwa akizitambua Mwenyezi Mungu. Na katika kukubaliana na ghiliba hizo za wavamizi Waafrika wakajikuta wanaanza kususa dini zao za jadi na kuziita upagani usiokubalika kwa Mungu huku wakiukumbatia vizuri utamaduni wa wavamizi hao wakiuita kuwa ndio wokovu!

Dini hizi za kigeni ndizo zilizotoa mchango mkubwa sana katika ustawishaji wa utumwa na ukoloni barana Afrika pamoja na kudunisha fikra za Waafrika hata leo.

Bahati mbaya ni kwamba mateka wa kwanza wa utamaduni huu wa kigeni ni wale wa tabaka la wasomi (wanazuoni) katika jamii yetu. Mpaka sasa, tabaka la wasomi, ndio waathirika wakubwa wa ubeberu huu, wengi wao wakiwa wanatumikishwa kama mawakala katika kuzibeza na kuzikandamiza tamaduni zao za asili, wakati huo huo wakizitukuza tamaduni za kigeni kuwa ndio ustaarabu wa dunia ya leo.

Ni wasomi haohao wanaong’ang’ania kuwapa watoto wao majina ya Kizungu na Kiarabu wakidai kwamba ni majina ya kidini ambayo ndiyo pekee anayoyatambua Mungu! Kasumba hii inawafikisha, baadhi ya wanajamii wenzetu, mahali pa kudhani kwamba hata lugha zetu hizi hazifahamiki wa Mungu na hivyo kutumia lugha za kigeni tu katika ibada zao!

Linalonisikitisha kupindukia ni hili la kuendelea kumuabudu Mwenyezi Mungu katika misingi ya ubaguzi kiasi hiki. Hasa sisi waafrika tunaoukubali na kuuendeleza ubaguzi huu dhidi yetu!

Wakati wamisionari wanaeneza ukristo walikuja na ushauri kwamba waamini wao hawakupaswa kuwaogopa na kuwatii viongozi wao, kama vile wafalme, ila aliyepaswa kuogopwa ni Mungu pekee. Ushauri wa aina hiyo ulipelekea baadhi ya Waafrika kunyongwa kwa amri za wafalme wao, kama ilivyotokea kule nchini Uganda enzi za mfalme Mwanga.

Na kwa vifo hivyo watu hao walionyongwa wakatangazwa na Papa Paulo wa sita, mwaka 1969, kuwa ni watakatifu. Baada ya dini zao kusimikwa na ukoloni kuota mizizi, somo likabadilika ikawa kwamba kuwatii watawala ni sharti toka kwa Mungu. Wakati huo watawala walikuwa tayari ni wakoloni wenyewe au vikabaraka wao.

Nia ya wavamizi hao kutufanyia hivyo ilikuwa ni kutuhakikishia kwamba tamaduni zao ndizo bora na kwamba zetu sisi ni za kijinga na za kishenzi ambazo hazikufaa kuhusishwa na Mwenyezi Mungu hata kidogo! Hili ni jambo ambalo hadi sasa baadhi ya wanajamii wetu bado wanakubaliana nalo!

Kibaya zaidi ni wale wasomi (intellectuals) ndio wametokea kuwa mawakala wa ubeberu huu. Hawa ni pamoja na mapadri, maaskofu, maimamu na masheikh. Wengi wao wamesoma mpaka viwango vya udaktari wa falsafa, lakini usomi wao huo haujawafanya wagundue na kuamini kwamba hata sisi weusi tumeumbwa na Mungu sawa na weupe na tuna nafasi sawa mbele yake. Na kwamba tulikuwa na njia ya kuwasiliana naye kwa mujibu wa torati zetu.

Nataka niungame kwamba mimi ni mkristo ambaye lakini sikushiriki kwa njia yoyote ile katika maamuzi ya kuingia katika imani hiyo. Niliingizwa katika imani hiyo nikiwa na takribani masaa 30 ya kuishi duniani! Baada ya kupata fahamu ndipo nikawa najiwa na maswali kadha wa kadha. Kwa sababu hiyo nitatumia ukristo kama sampuli ya tamaduni za kigeni zilizoletwa kufunika tamaduni zetu za asili.

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” Mt. 5:17. Haya ni maneno yanayopatikana katika kitabu kinachoitwa Biblia, kitabu ambacho ni mkusanyiko wa maandishi yenye ujumbe mbali mbali uliojaa hekima uliotolewa na wazee wa sehemu mojawapo ya chimbuko la tamaduni hizi tunazoziita dini, wazee ambao kutokana na busara zao waliitwa mitume.

Maneno haya yanayosadikika yalisemwa na Bwana Yesu, kwa mujibu wa kitabu cha Biblia, yalikuwa yanawahimiza wakazi wa sehemu hizo kulinda na kuenzi tamaduni zao zinazotajwa kama torati na kutochukulia ujio wake kama chanzo cha kuvuruga utamaduni huo. Maneno hayo ya busara ya Bwana Yesu aliyalenga kwa wale aliokuja kwa ajili yao kama mwenyewe alivyosema “akajibu, akasema, sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” Mt 15:24.
Kama Yesu anakataa kwamba hakuja kutengua torati, tena zilizojaa dosari, bali kuzitimiliza, iweje torati zetu sisi ambazo hazikuwa na dosari ndizo zitenguliwe?.

Ingawa sehemu kubwa ya wanajamii wetu imeukumbatia utamaduni huu kutoka ughaibuni na kujifanya nao eti ni wana wa Israel, itakuwa haileti maana wala faida yoyote iwapo uloweza huu utatufanya viziwi tukashindwa kuyasikia hata aliyoyanena yeye yule ambaye, tumeacha kujitambulisha kwa makabila yetu na au utaifa wetu badala yake tunajitambulisha kwa jina lake, Wakristo!

Torati ambayo Bwana Yesu anasema hakuja kuitengua ni nini? Yatasemwa mengi kadiri kila mmoja anavyoleweshwa na kasumba hii ya kukumbatia tamaduni za wengine, lakini ukweli utabaki kwamba torati ni utamaduni wa kila jamii. Mumo humo, katika kila torati kuna sheria kuu za Mungu, kama amri kumi na mengineyo. Kwa mfano, hakuna jamii yoyote ambayo tamaduni zake zinakinzana na sheria kuu za Mungu.

Asiyekubaliana nami kuhusu ilo aniambie kwa mfano, ni jamii gani ambayo mtu alipokuwa akiiba kitu cha mwenzake anafanyiwa sherehe ya kumpongeza. Wakati kwenye torati za wayaudi ilikuwa kwamba mtu aliyekuwa anabainika kwamba kazini, adhabu ilikuwa kwamba anapigwa mawe mpaka afe, sisi kwetu Bukoba, msichana aliyekuwa anapata mimba kabla ya kuolewa alikuwa anajidhihirisha kwamba kazini na adhabu yake ilikuwa ni kufungwa jiwe zito shingoni na kutoswa kwenye mto wenye kina kirefu au ziwani.
Kwa maana hiyo inabidi ieleweke kwamba kila anayekiuka na kuanza kubeza tamaduni zake, anakuwa amekiuka na kubeza torati, hata kama ni zile zilizo kwenye mapokeo simulizi tu. Na kwa maana nyingine anakuwa amembeza Kristo vile vile, ijapo atakuwa anajiita mkiristo.

Imani yangu inanituma kuamini kwamba wenzetu kututangulia kujua kuandika na hivyo kuwahi kuweka tamaduni zao (torati) katika maandishi haiwapi uhalali na haki ya kukandamiza au kufuta tamaduni (torati) zetu.

Katika kujitafutia uhalali wa nawao kuitwa wana wa Israel, hawa watu wa sehemu zetu wanaojiita Wakristo wamekuwa wakinukuu maneno kutoka kwenye Biblia yanayosema “enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na mwana na Roho Mtakatifu” Mt. 28:49, bila kuelewa kwamba mataifa yanayoongelewa katika kitabu kile ni yale ya Mashariki ya Kati hasa yaliyoizunguka Israel. Huo ndiyo ulimwengu unaoongelewa kwenye kitabu kile. Ingawa yanaweza yakajitokeza madai ya kwamba majina ya nchi zetu hizi yalikuwa hayajakuwepo kama yalivyo leo, hakuna ushahidi wowote kwenye Biblia unaoonyesha kwamba kinachotajwa ni sehemu hizi tulizopo sisi kwa sasa.

Kuna dhana nyingine ya kiimani kwamba sehemu zile za Mashariki ya Kati ni sehemu takatifu kutokana na Mungu kuzipendelea na kuwashusha mitume wake eneo lile pekee. Hizi ni fikira tatanishi ambazo napingana nazo katika misingi ya kwamba ni kumkufuru Mwenyezi Mungu katika kumhusisha na upendeleo.

Ninaloamini ni kwamba yale ni maeneo yaliyokubuhu kwa maasi na kumchukiza Mungu kiasi cha yeye kutaka kuyaangamiza. Hakuna sehemu nyingine duniani iliyopata kumchukiza Mungu kama sehemu zile. Hebu tuangalie ushahidi wa Biblia; “Mungu akamwambia Nuhu, mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma basi nitawaharibu pamoja na dunia” Mwa 6: 13. Ushahidi kama huu ni mwingi wenye kutanabahisha kwamba yale yalikuwa ni maeneo yaliyojaa maasi. Mfano, ni yale yaliyotokea Sodoma na Gomora. Na yale ya Yona na Niwawi, yote haya yanaainisha hasira za Mungu juu ya maeneo yale.

Mwenyezi Mungu ni mwenye mapenzi, kama alivyotupenda sisi kwa kutuumba na kutuweka eneo letu na tukawa wanyenyekevu, nao aliwapenda pia na kuwapa eneo lao wakashindwa kuwa wanyenyekevu. Ili kuwanusuru asiwateketeze, kwa mapenzi yake, akawashushia hao mitume. Huu ni upendeleo wa kuwanusuru, sio upendeleo wa kuwaona bora kuliko sisi. Hatuna haja ya kuwa na husuda nao, sababu sisi ni wema kwa Mwenyezi Mungu.

Uhalifu wa jadi wa maeneo yale (Mashariki ya Kati), bado ungalipo hata sasa. Yanayotendeka kule kwa wakati huu ni ushahidi tosha. Vita isiyoisha, watu kukosa mapenzi ya kiutu kiasi cha kuvaa mabomu kwa lengo la kujilipua ili wakawaue wenzao, watu kuwachinja wenzao kama vile wanachinja wanyama n.k, ni matendo ambayo sio tu kwamba yanaonyesha kwa nini Mungu aliwateremshia hao mitume, bali yanaashiria ujio wa mitume wengine. Sababu naamini Mwenyezi Mungu hajawachoka.

Hawa watu tunaowaita mitume, ni watu ambao waliasisi mitazamo fulani ya kiimani katika kuboresha tamaduni zao, kitu kilichopelekea waendelee kuheshimiwa na kuenziwa kadiri tamaduni hizo zinavyoenea katika mataifa mengine. Mara nyingi watu hao hawakuanzisha tamaduni hizo, ambazo zimetokea kuwa maarufu huku kwetu kama dini, ila walikuwa na vipawa vikubwa vya kutafakari mambo ya kiimani na kuweza kupambanua halali na batili na kutoa miongozo ya maisha au masuluhisho adhimu ya matatizo au majanga yaliyokuwa yakizikabili jamii zao kwa wakati huo.

Lakini kwa vile watu wote duniani tuna hisia zinazokaribia kufanana, tuna shida na faraja zinazofanana, mema na mabaya ni yale yale, basi mengi ya masuluhisho au miongozo iliyoainishwa na watu hao inaweza ikatumika popote duniani bila ulazima wa kuathiri tamaduni za sehemu husika.

Hata hivyo, sio kweli kuwa sisi hatukuwa na watu waliokuwa na busara kiasi cha kupewa heshima ya unabii. Shida ni ule usemi kwamba nabii hakubaliki kwao. Usemi huo ndio unaoviza imani zetu na kutufanya tuamini kwamba manabii walitokea kule ughaibuni tu. Lakini kumbuka tatizo hili sio letu peke yetu, ila ni la wanadamu karibu wote. Tunasoma katika hadithi zinazomuhusu Bwana Yesu jinsi ambavyo hakukubalika kwao kiasi cha kujengewa kesi iliyopelekea kusulubiwa kwake na kuwambwa msalabani, tendo ambalo, kulingana na mila za Wayahusi, walikuwa wanafanyiwa wahalifu wa daraja la kwanza!

Kama Bwana Yesu alifanyiwa mambo hayo na watu wa jamii yake katika kile kinachoaminika kwamba ilikuwa ni mikakati ya kupinga unabii wake, ni kitu gani kinachozuia akili zetu kufunguka ili tuweze kuamini kwamba hata sisi tulikuwa nao manabii ambao lakini kutokana na ufukara wa kutoweza kutunza kumbukumbu andishi manabii hao walitoweka na wakati?

Mwandishi maarufu, Hussein Siyovelwa, anatayarisha kitabu, ambacho pengine kitatumika kama biblia, kwa ajili ya kulinda imani yetu ya asili. Tayari baadhi ya watu wameuelewa na kuupenda mtazamo wake. Ni imani yangu kwamba wote wanaojitambua watauelewa na kuupenda mtazamo wa Siyovelwa.

Nataka nihitimishe makala yangu haya kwa swali. Kwa vile karibu sababu zote zilizochochea ujio wa tamaduni hizi za kigeni, ambazo tayari zimeishajigeuza kuwa himaya, kupitwa na wakati, ni nini haja ya himaya hizi (dini za kigeni) kwa sasa?

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau