DC MULEBA ATAKA MAABARA SHULE ZOTE ZA KATA
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Muleba, Lembris Kipuyo
UJENZI wa vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Muleba, mkoani Kagera hauwezi kukamilika iwapo shule hizo hazitakuwa na maabara za sayansi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Muleba, Lembris Kipuyo, alipozungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.
Kipuyo alisema Rais Jakaya Kikwete akiwa katika ziara za kikazi Bagamoyo na Mwanza aliagiza ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenda sambamba na ujenzi wa maabara za sayansi ambazo ni za Baiolojia, Fizikia na Kemia kila shule ili ifikapo Septemba, 2014 viwe vimekamilika.
Alisema ujenzi huo wa maabara utahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na kuinua kiwango cha elimu hususan kwa wananfunzi watakaochukua masomo hayo ambao wataweza kujifunza kwa nadharia na vitendo.
Aliwashauri madiwani kutumia nafasi walizonazo kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa maabara kwa chochote walichonacho kupitia kikao cha maendeleo ya kata ( WDC ) kwa kujiwekea kiwango kinachotakiwa kuchangwa na kila mwananchi.
“Kupitia Kamati ya Elimu ya Wilaya mwaka 2012 niliagiza kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie sh 5,000, suala hili likisimamiwa litasaidia kutekeleza agizo la rais vilevile halmashauri ijipange na kuchangia ujenzi na ukamilishaji wa maabara mapema ewezekanavyo,” alisema Kipuyo.
Hata hivyo alisisitiza ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu muhimu katika shule za sekondari kwa kueleza kuwa jumla ya wanafunzi 9,914 walifanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu wilayani humo.
Alisema walijiwekea kiwango cha ufaulu wa asilimia 85, wakitegemea wanafunzi 8,427 kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ambapo vilikuwa vikitakiwa vyumba vya madarasa 211.
Na Ashura Jumapili.