Bukobawadau

Kagasheki amuweka matatani DC

 MKUU wa Wilaya (DC) ya Misenyi, mkoani Kagera, Kanali mstaafu Issa Njiku, ameingia matatani na huenda akashtakiwa kutokana na kujipa mamlaka yasiyo yake ya kutoa vibali vya uvunaji wa magogo katika misitu ya hifadhi ukiwamo wa Minziro.
Mkuu huyo wa wilaya amekuwa akitoa vibali kwa taasisi za dini na shule mbalimbali wilayani humo kwa ajili ya kuvuna magogo kinyume na mamlaka yake.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, alisema mkuu wa wilaya hana mamlaka ya kutoa vibali kwa watu au taasisi yoyote kuvuna magogo ndani ya msitu wa hifadhi ya taifa wa Minziro ambao uko chini ya wizara yake.
Alisema kitendo hicho ni matumizi mabaya ya madaraka na kuwaagiza wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kufanya uchunguzi juu ya madai ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi kutoa vibali hovyo kwa watu kuvuna magogo ndani ya msitu huo.
Kagasheki alitoa msimamo huo baada ya kukabidhiwa nakala za  baadhi ya vibali ambavyo vimekuwa vikitolewa na watendaji wa halmashauri hiyo kikiwamo pia cha mkuu wa wilaya na afisa misitu wa wilaya, James Matekere, na mwenzake Thomas Matabaro.
Naye mkurugenzi wa TFS, Juma Mgoo, akizungumza mbele ya Kagasheki, alisema mkuu wa wilaya ya Misenyi si ofisa mwenye mamlaka ya kutoa vibali na hivyo kitendo alichokifanya anastahili kushtakiwa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa Januari 13 mwaka 2010, mkuu huyo alitoa kibali cha kuvuna magogo kwa ajili ya mbao chenye kumbukumbu namba KGR/MS/M.50/1117 kwa ajili ya misikiti, shule za msingi na sekondari.
Kwa mujibu wa kibali hicho ambacho nakala yake tunayo, walionufaika ni msikiti wa Kenkondo Mshasha, Bugorora, Shule ya Sekondari Gabulanga, Ruzinga, Bubale na shule za msingi za Bubale na Bugorora.
Vibali hivyo vinaonyesha kuwa mbali ya taasisi zikiwamo shule za msingi na sekodari, mahakama ya mwanzo Minziro na kituo cha polisi cha Minziro, watu binafsi nao wamenufaika ambao ni Laban Ibrahim na Yazid Saidi wakati hawakustahili kwa sababu si taasisi.
Kutokana na wimbi la maofisa wa halmashauri ya wilaya hiyo kutoa vibali kiholela, wakala wa TFS, umepanga kupeleka timu ya wataalamu kufanya uchunguzi, ukaguzi na tathmini ya uharibifu wa mazingira uliofanywa katika msitu huo wa Minziro.
Mbali na mkuu wa wilaya, wengine wanaodaiwa kutoa vibali bila kuwa na mamlaka ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Elizabert Kitundu, ambaye amekuwa akimtumia ofisa wake kutoka idara ya misitu wa wilaya hiyo, James Matekere, ambaye ndiye amekuwa akisaini vibali kwa niaba ya mkurugenzi wake.
Msitu huo wa Minziro unazungukwa na vijiji zaidi ya kumi vya Byamtemba, Igayaza vilivyopo kata ya Nsunga, Mtukula cha kata ya Mtukula na Mabuye, Kakindo vya kata ya Kassambya na Minziro, Kigazi na Kalagala vya kata ya Minziro na kata za Buyango na Luzinga.
Vibali hivyo vimekuwa vikitolewa kwa kisingizio cha shughuli za kijamii ikiwamo ujenzi wa shule, vituo vya afya, ujenzi wa mahakama lakini hutumika kuvuna shehena kubwa za mbao ambazo husafirishwa na kwenda kuuzwa Bukoba mjini na nchini  Uganda huku serikali ikikosa mapato.
Source;Tanzania Daima


Next Post Previous Post
Bukobawadau