Bukobawadau

Kwa nini JK anamwachia Chiza aunyonge ushirika?

Na Prudence Karugendo SIASA, kwa vyovyote vile ni mfumo unaocheza na maisha ya watu, kusudi watu wapate maisha bora. Wapate chakula bora, matibabu bora, malazi bora, elimu bora nakadhalika. Pamoja na hayo wawe na uwezo wa kujikimu. Siasa ikitetereka kidogo tu na kuyasahau hayo mara moja inageuka uchwara, kwa maana ya mfumo usiowajali wananchi na hivyo wananchi kuuchukulia kama mfumo usiowafaa. Mtu mmoja anayetafuta maisha akiwa ameajiriwa kwenye kampuni moja toka nje ya nchi inayojishughulisha na ujenzi wa barabara Jijini Dar es salaam, kanilalamikia kwa uchungu kwa nini napendelea kuandika juu ya ushirika badala ya kuandika juu ya matatizo kama ya kwao, wazawa, wanayopewa na mwajiri wao, kampuni ya kigeni? Swali lake lilikuwa zuri, na ningependa nimjibu mtu huyo kupitia kwenye makala hii. Ni kwamba wananchi wazawa wanaoajiriwa na makampuni kutoka nje ya nchi wanayo hiari ya kukubali kuajiriwa au kutoajiriwa na makampuni hayo. Ajira zao sio za kulazimishwa. Wakiona waajiri wao wanawafanyia mambo yasiyokuwa ya kiutu wanaweza wakaachana nao ili tuone kama hao wazungu watawabeba wenzao toka kwao kuja kuwa vibarua huku kwetu. Sababu kinachowafanya watu hao waajiri wazawa ni unafuu wa gharama. Hivyo katika kutafuta maisha suala la mtu huyo aliyenitumia ujumbe mfupi wa maandishi ni tofauti kabisa na la mkulima anayeanzisha ushirika ili ukasimamie juhudi zake katika kilimo. Sababu ushirika unapomgeuka mkulima na kuanza kumwibia anajikuta hana njia nyingine ya kujinusuru. Pengine anachoweza kufanya mkulima ni kuyauza mazao yake kwa njia za magendo, kitu ambacho hakiruhusiwi kwa vile ni kinyume cha sheria. Kwahiyo mkulima anapoamua kuachana na ushirika kinachofuatia ni ushirika kufa kifo cha kawaida, na katika kifo cha ushirika mkulima naye anajikuta amenaswa mlemle kwa vile atakuwa amelazimika kuacha kilimo ambacho tunaelewa kuwa ndicho kilicho uti wa mgongo kwa binadamu, hasa kwa Watanzania. Binadamu akishavunjika uti wa mgongo maisha yako wapi tena? Sababu, kama inavyosemwa na wanasiasa, kilimo ndio uti wa mgongo kwa Mtanzania, na ushirika ndio unaopaswa kuwa uti wa mgongo wa kilimo, hasa kilimo cha biashara. Tunapouachia ushirika ufe maana yake ni kwamba wakulima wafe, ambao tena ndio wanaounda asilimia kubwa ya wananchi. Kwa kuuzingatia ukweli kwamba kilimo ndio uti wa mgongo kwa Watanzania, tuliona katika awamu ya kwanza jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alivyohangaika kuuongezea nguvu ushirika ili nao ukawaongezee nguvu wananchi, ambao idadi yao kubwa inaundwa na wakulima, kusudi nao wazidishe nguvu zao katika kilimo na hivyo kuyainua maisha yao pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla. Katika juhudi hizo zilizosimamiwa na Mwalimu tuliona zikiundwa Bodi za mazao mbalimbali ili kuyasimamia na kuhakikisha kilimo chake hakitetereki. Tuliona kwa mfano Bodi ya Kahawa, Bodi ya Pamba, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Korosho nakadhalika. Hata kama mambo hayakunyooka kama ilivyokuwa imekusudiwa kutokana na mpango mzima kuzingirwa na ubinadamu, lakini walau tuliziona juhudi za makusudi za Mwalimu Nyerere zilizokuwa na malengo mema. Sasa hivi ushirika unakufa, tena kwa kuuawa na waliopewa dhamana ya kuulinda! Sababu pamoja na kuwepo kwa nafasi za waziri na naibu wake, Kilimo, Chakula na Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika pamoja na Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika, bado nafasi hizo hazioneshi juhudi zozote za kuulinda na kuuzuia ushirika usife! Mashahidi wangu katika hili ni wanaushirika wa KNCU, SHIRECU, Nyanza, KCU (1990) Ltd., KDCU na wengine wenye uelewa wa ushirika. Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba wote niliowataja, walio katika nafasi za kumsaidia rais kuudumisha ushirika, wanafanya makusudi ya kumtengenezea Rais Kikwete historia chafu. Historia ya kwamba ndiye rais aliyeuzika ushirika nchini. Kwahiyo wakati tunamkumbuka Nyerere kwamba alifanya kila mbinu kuhakikisha ushirika unashamiri, hasa kwa manufaa ya wakulima, jambo lililowafanya wananchi watamani kubaki vijijini kuwa wakulima, wasaidizi wa Kikwete kwa upande huo wanafanya kila njia ili Kikwete abaki kukumbukwa kwa kifo cha ushirika, kitu kitakachowafanya wakulima waamue kukimbilia mijini kwa wingi. Kwa nini mkulima abaki kijijini akizalisha kitu kisichokuwa na manufaa kwake? Mfano mtu anazalisha kahawa kwa wingi, zao mojawapo kati ya mazao makuu ya kibishara, lakini analazimika kubaki ombaomba kama Marehemu Matonya, kisa chama chake cha ushirika kinamfanyia utapeli, huku wahusika waliowekwa na serikali kuhakikisha kitu kama hicho hakijitokezi wakiangalia bila kuchukua hatua yoyote! Mara nyingi wanaushirika, wengi wao wakiwa ni wakulima wa kawaida, hawana mahali pa kusemea zaidi ya vikao katika vyama vyao vya msingi ambako wana wawakilishi wao waliowachagua kwa ajili ya kuwawakilisha kwenye mikutano ya chama kikuu. Lakini bahati mbaya wawakilishi hao wametokea kugeuzwa miradi ya uongozi wa vyama vikuu, wakiwa wamewaterekeza wakulima wenzao wasio na mahali pengine pa kusemea. Nitatoa mfano mmoja wa chama kikuu cha ushirika ambacho kimeamua kujinyonga chenyewe, bilashaka kwa kuongozwa na maamuzi ya uongozi wake, pasipo kujali nini hatma ya wanaushirika wake. Chama hicho ni chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha mkoani Kagera. Kutokana na chama hicho kukabiliwa na madeni, mengine yakiwa ni yale kisiyoweza kuyatolea maelezo kwa wanaushirika, na deni kubwa likiwa ni la benki ya CRDB linalofikia shilingi bilioni 5, chama hicho kimeamua kuitisha mkutano mkuu wa dharura tarehe 22 Oktoba, 2013, ili kuwashawishi wajumbe wake waridhie chama hicho kujifanyia ufisadi, yaani kukomba pesa karibu yote kutoka kwenye kitengo chake kinachoitwa Moshi Export, kinachojishughulisha na masoko ya nje ya nchi pia kikiwa kama kitegauchumi kikuu kinachojitegemea. Wanaushirika na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa KCU (1990) Ltd. wanasema kwamba, kama kawaida yake, uongozi wa KCU (1990) Ltd. umelazimika kuwaona kwanza baadhi ya wajumbe kwa ajili ya kuwalegeza na kuwaelekeza watakachokifanya kwenye mkutano huo wa dharura. Kwahiyo wajumbe hao ambao tayari wanakuwa wameonana na uongozi na kuelekezwa cha kufanya ndio wanopewa kipaumbele kwenye mkutano, wakati wale wanaoshukiwa na uongozi wa ushirika kwamba wanaweza kuuliza maswali magumu na pengine kufumua siri iliyofunikwa na uongozi ili isijulikane kwa wanaushirika, hawapewi nafasi ya kuuliza maswali au wakati mwingine kuzuiwa kabisa kwa njia za kigaidi kusudi wasiweze kuingia kwenye ukumbi wa mkutano! Jambo linaloshangaza ni la kwamba inawezekanaje mjumbe, aliye mwakilishi wa wanaushirika, azuiwe kuingia kwenye mkutano unaojadili masuala ya wanaushirika ambao ndio wenye mali? Kwa nini wanaushirika wa sehemu fulani wakoseshwe uwakilishi kwenye mkutano wa chama chao? Cha kushangaza zaidi ni kwamba wengine wanaoshiriki hujuma hizo ni wafanyakazi waajiriwa tu wa hicho chama kikuu, wanaoingia kwenye mkutano mkuu kwa nafasi zao za kuajiriwa bila kumwakilisha mwanaushirika yeyote isipokuwa kuwatunikia tu wanaushirika. Kwa maana hiyo mwajiriwa anakuwa anamzuia bosi wake asishiriki maamuzi yanayompatia ajira! Kwa upande mwingine kuna mwenyekiti wa chama kikuu. Huyo kazi yake ni kuendesha mikutano na mambo mengnie wala siyo kuwapangia wanaushirika wa vyama vya msingi nani anafaa kuwa mwakilishi wao. Kwahiyo kwa nini mwenyekiti huyo, anayetakiwa kusikilizwa na wawakilishi hao kuona kama yuko sahihi katika mwenendo wa ushirika, ajipatie nguvu ya kumfukuza au kutomruhusu kuingia kwenye mkutano mwakilishi wa wanaushirika wakati mwenyekiti hana mamlaka hayo? Sababu yeye kuwa mwenyekiti haina maana kuwa ushirika tayari unakuwa umegeuka mali yake. Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa dharura wa KCU (1990) Ltd., tarehe 22 Oktoba, 2013, wanasema kichekesho ni kwamba pesa iliyotakiwa kuidhinishwa na mkutano huo kutoka kitengo cha Moshi Export ni pesa hewa! Eti pesa hiyo ilishatolewa zamani kinyemela na uongozi wa chama hicho na kutumika bila ridhaa yoyote. Kwahiyo eti kilikuwa kinaidhinishwa kitu ambacho hakikuwepo! Inasemekana kwamba mambo hayo ndiyo yaliyoufanya uongozi upange watu wa kuuliza maswali, wa kushangilia pamoja na kuzomea huku ukiwa umewazuia wengine wasiingie kabisa kwenye mkutano. Uongozi ulielewa kwamba kilichokuwa kinafanyika ni kitu ambacho kisingepata majibu kutoka kwa watu walio makini. Kwa hali yoyote ilivyo hizi ni dalili mbaya za ushirika unaokufa. Na mpaka kufikia hapo kila kitu kuhusu ushirika huo kinajulikana kwa wanaohusika, sababu hayo yote yameelezwa kwa waziri mhusika, pamoja na mrajis. Ila badala ya kushughulikia tatizo linalijionesha ili kuunusuru ushirika, waziri anataka tatizo lijishughulikie na kujitatua lenyewe! Mrajis wa Vyama vya Ushirika, ijapokuwa yeye hana muda mrefu kwenye nafasi hiyo, lakini yanayoihusu KCU (1990) Ltd. anayaelewa fika. Naye huyo haonyeshi dalili zozote za kuokoa jahazi. Je, tunaweza kusema kwamba hiki ndicho kiama cha ushirika nchini? Na je, kwa nini Rais Kikwete amruhusu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandidi Christopher Chiza, aunyonge ushirika na kumharibia historia yake anayojaribu kuitengeneza? Kama mambo ya ushirika yamekuwa magumu kwa Chiza kwa nini hamuombi bosi wake kukaa pembeni ili rais akawajaribu wengine kuona kama wanaweza kuuokoa ushirika, kuliko yeye, Chiza, kung’ang’ania kumchafulia JK historia yake? prudencekarugendo@yahoo.com 0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau