MULEBA YASHAURIWA KUSOGEZA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera imeshauriwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi kwa kutekeleza mpango wa serikali wa kujenga zahanati kila kijiji sambamba na kuwa na mpango mkakati wa kudhibiti mlipuko wa malaria pindi unapotokea.
Ushauri huo ulitolewa na mkuu wa wilaya hiyo Lembris Kipuyo baada ya kutokea kwa mlipuko wa malaria wilayani humo kipindi cha mwezi Mei na Juni mwaka huu na kusababisha vifo vya watoto wengi chini ya miaka mitano.
Kipuyo alisema kwa sasa katika wilaya hiyo maambukizi ya malaria ni asilimia 22 ambapo alidai kuwa kiwango hicho bado ni kikubwa na kuwataka watendaji na viongozi wote wa halmashauri hiyo kuhamasisha wananchi umuhimu wa kutumia vyandarua na kusafisha mazingira ili kuharibu mazalia ya mbu.
Alisema ni wajibu wa halmashauri kuwasiliana na idara ya afya ili iwapatie wataalam wa afya wa kutosha yakiwemo madawa na vifaa tiba vya kutosha ili kukabiliana na tatizo la malaria katika wilaya hiyo.
Na Ashura Jumapili.