Mwandiki:Uongozi wa KCU (1990) Ltd. unanihofia kwa sababu ya madhambi yake
MWANACHAMA wa chama cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha mkoani Kagera, ambaye pia ni mwakilishi wa chama cha msingi cha Kamachumu,Archard Felician Muhandiki, amekuwa akisakamwa sana na uongozi wa chama hicho cha ushirika kiasi cha hata kufukuzwa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho na
wakati mwingine kuzuiwa asiingie kabisa kwenye mkutano. Kutokana na matendo hayo yanayojionyesha wazi kuwa ni hujuma dhidi ya wanaushirika,nimeamua kumtafuta Mzee Muhandiki ili kujua sababu zinazoufanya uongozi wa chama hicho kuchukua uamuzi huo wa aina yake. Yafuatayo ndiyo mazungumzo kati ya mwandishi wa makala hii na Mzee Muhandiki.
Karugendo:Mzee Muhandiki, kwa muda mrefu umekuwa ukiishi Dar es salaam,ni kitu gani kimekuhamasisha utake kuwa mwakilishi wa wanaushirika katika chama cha msingi cha Kamachumu?
wakati mwingine kuzuiwa asiingie kabisa kwenye mkutano. Kutokana na matendo hayo yanayojionyesha wazi kuwa ni hujuma dhidi ya wanaushirika,nimeamua kumtafuta Mzee Muhandiki ili kujua sababu zinazoufanya uongozi wa chama hicho kuchukua uamuzi huo wa aina yake. Yafuatayo ndiyo mazungumzo kati ya mwandishi wa makala hii na Mzee Muhandiki.
Karugendo:Mzee Muhandiki, kwa muda mrefu umekuwa ukiishi Dar es salaam,ni kitu gani kimekuhamasisha utake kuwa mwakilishi wa wanaushirika katika chama cha msingi cha Kamachumu?
Muhandiki:Kwanza, nimemaliza muda wangu wa kuajiriwa hapa Dar es salaam,nimeona nirudi nyumbani kwa vile bado nina nguvu ili nikasaidie kupunguza umasikini nyumbani kwetu.Basi niliona niingie kwenye ushirika kwa vile ninao uzoefu mkubwa kwenye masoko hasa yanayohusiana na mambo ya ushirika. Nikaona namna ya kumkwamua Mhaya kiuchumi ni kulitafutia soko zuri zao lake kuu la kibiashara,kahawa.
Karugendo:Habari za wewe kuamua kurudi kijijini na kujiingiza moja kwa moja kwenye ushirika zilipokelewaje na wanaushirika?
Muhandiki: Wanaushirika wa chama changu cha msingi walizipokea habari hizo kwa furaha kubwa. Ila habari hizo zilipowafikiaviongozi wa ushirika, kuwa na mimi naingia kwenye ushirika, viongozi wa ushirika wetu wakaanzisha majungu hata kabla sijachaguliwa kuwa mwakilishi wa chama changu cha msingi. Ikadaiwa kwamba mimi ni tajiri sana kwahiyo kwa nini nitamani kuingia kwenye ushirika.Wengine wakadai kwamba mimi ni mhuni, mwizi nakadhalika. Hayo yote yaliandikwa kwenye baadhi ya magazeti na kwenye vipeperushi.
Karugendo:Uliuonaje upinzani huo dhidi yako na uliuchukuliaje?
Muhandiki:Mimi niliuona wote ni upuuzi huo.Lakini pamoja na hiyo uongozi karibu wote wa KCU (1990) Ltd. ulihamia kwenye chama changu cha msingi wakati wa uchaguzi ili kuhakikisha unaniangusha, lakini ukashindwa.
Karugendo:Baada ya kuelewa kuwa uongozi wa chama kikuu haukutaki ni kitu gani kilikupa ujasiri wa kuendelea kubaki kwenye ushirika mpaka ukapata ushindi wa kishindo? Kwa nini uliyoyashuhudia toka kwa uongozi wa chama kikuu hayakukukatisha tamaa?
Muhandiki:Mimi sikwenda kijijini kuutetea uongozi wa ushirika, nilienda kuwatetea wakulima, wanaushiria. Kwahiyo yaliyokuwa yanafanywa na uongozi wa ushirika yasingeweza kunikatisha tamaa, mambo yao hayo ndiyo yaliyonisukuma nikawatetee wakulima. Ningekuwa naelewa kwamba wakulima wanatendewa haki nisingekuwa na haja ya kwenda kule. Hicho ndicho kilichonipa ujasiri.
Karugendo:Kabla hatujaendelea, je, wewe nimwanaushirika?
Muhandiki:Ndiyo ni mwanaushirika.
Karugendo:Una uhakika kuwa unakubalika kwa wanaushirika wa chama chako cha msingi unaowawakilisha, na kama unakubalika unakumbuka walikuchagua kwa kiasi gani?
Muhandiki:Mimi nakubalika sana kwa wanaushirika wa chama changu cha msingi. Nakumbuka walinichagua kwa zaidi ya asilimia 95.
Karugendo:Kuna wakati ulifukuzwa kwenye mkutano mkuu wa chama kikuu, na mara ya pili ukazuiwa kabisa kuigia kwenye mkutano wa dharura wa chama hicho kikuu wa tarehe 22 / 10 / 2013, ukiwa mwakilishi halali wa chama chako cha msingi. Unadhani ni kitu gani kinasababisha mambo hayo?
Muhandiki:Sababu ni kwamba uongozi wa chama kikuu cha KCU (1990) Ltd. unanishuku kuwa nitayaweka wazi maovu yake yote unayoyafanya.
Karugendo:Kwa nini uongozi wa KCU (1990) Ltd.unatokea kukuhofia hivyo, na ni nani hasa anayeonekana kuongoza hofu hizo dhidi yako?
Muhandiki:Kama nilivyokueleza, ni kwamba uongozi wa KCU unanihofia kwa kutaka kuyaficha madhambi yake. Unaelewa kabisa kuwa mimi nimeingia kwenye ushirika kwa ajili ya kuwatetea wanaushirika na wala sikuingia mle kwa sababu ya njaa. Kawaida ya uongozi wa chama kile unapendelea wawakilishi wanaosukumwa na njaa kuutaka uwakilishi, sababu hao wanaweza kuwamudu kadiri watakavyo kwa vile wanaongozwa na njaa na si matakwa ya wanaushirika wanaowawakilisha.Wanaoonekana kuongoza hofu dhidi yangu ni watu wawili, Mwenyekiti John Binunshu na Meneja Mkuu Vedasto Ngaiza. Wanahofia kwa vile wamefanya uchafu mwingi mno kwenye chama hicho cha ushirika.Uchafu huo niliuona mara tu baada ya kusoma kwa mara ya kwanza nyalaka zinazoonyesha utendaji wa chama kikuu ulivyo. Niliona mambo kama ya hisa zilizokuwa CRDB na baadaye kuuzwa kwa bei ya kutupa bila pesa iliyotokana na hisa hizo kuonekana ilikokwenda. Pia niliona mambo kama ya hoteli ya Yasila, ujenzi wa jengo linalodaiwa ni la kitegauchumi nakadhalika. Yote hayo ni mambo ya kutia mashaka makubwa.Kawaida wawakilishi wengi hawana mazoea ya kusoma nyalaka wanazopewa kwenye mkutano,wengi hufanya kazi ya kuidhinisha tu basi, pasipo kukielewa wanachokiidhinisha.
Karugendo:Baada ya kuyaona hayo ulichukua hatua gani?
Muhandiki:Nilianza mara moja kuulizia juu ya madudu hayo lakini nikaonekana nafanya fujo kwenye mkutano. Wawakilishi wenzangu, ambao si kawaida yao kusoma makabrasha, nao wakaungana na uongozi kuniona kwamba nafanya fujo kuulizia mambo hayo! Wengi wao wanauona mkutano kama unawapotezea muda baada ya kupewa posho nzuri, wanachokijali zaidi ni kwenda kufanya “shopping” na kuondoka zao nyumbani kuwatambia wanaushirika wanaowawakilisha!
Karugendo:Juhudi gani ulizozifanya, kama mwanaushirika hai, kuonyesha kuwa KCU inafanya ndivyosivyo?
Muhandiki:Mwanzoni kabisa nilienda mahakamani ili kutengua matokeo ya uchaguzi mkuu kwa vile mkutano mzima wa kwanza kuhudhuria ulikuwa batili. Lakini bahati mbaya mwanasheria wangu kuna mambo yalimghafilisha na hivyo kuifanya kesi isisikilizwe.
Karugendo:Kwahiyo baada ya mahakama kutoisikiliza kesi yako ukaamua mambo yaishe?
Muhandiki:Hapana, sikukubali yaishe,niliendelea na msimamo wangu wa kutoridhishwa na mwenendo wa chama kikuu.Niliandika barua kwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza. Pia nikaamua kwenda kumuona vilevile ofisini kwake Dodoma, sikufanikiwa kuonana naye baada ya kuambiwa na katibu wake kuwa hana nafasi ya kuniona. Pia nilijaribu kumuona katika ofisi ya Dar es salaam ikashindikana.
Lakini baadaye wakati nafukuzwa kwenye mkutano mkuu wa tarehe 14 Mei, 2013, mwenyekiti wa KCU alinionyesha barua niliyomuandikia Waziri Chiza akisema kwa kejeri kuwa waziri aliirudisha barua hiyo kwake eti akiuliza kwamba nyie Wahaya mkoje? Eti waziri akasema hebu muiteni huyo mkamshughulikie.Na baada ya hapo Meneja Mkuu, Ngaiza, aliandika barua kwenye chama changu cha msingi akikiamrisha kinifute uanachama!
Karugendo:Je, ukiwa Dar es salaam, viongozi wa KCU (1990) Ltd. wanaweza kuwasiliana na wewe nakukutaarifu juu ya masuala ya KCU, mikutano nakadhalika, kama wafanyavyo kwa wawakilishi wengine?
Muhandiki:Hawafanyi hivyo hata mara moja. Kwanza wanapigana kufa na kupona kuhakikisha naondolewa kwenye uwakilishi wa chama changu cha msingi na kisha kuvuliwa uanachama,watawezaje kunipa ushirikiano wa aina hiyo?
Karugendo:Uonavyo wewe viongozi wa KCU (1990)Ltd. wanayo nia ya dhati kuuona ushirika ukishamiri na kuwainua wakulima kiuchumi?
Muhandiki:Nikionacho mimi ni kwamba nia ya uongozi wa KCU (1990) Ltd. ni kuhakikisha chama hicho kinakufa kabisa na kuwaona wakulima wa kahawa wanadhalilika. Sababu hawawezi kuwa wana nia tofauti na hiyo wakayafanya wanayoyafanya.
Karugendo:Kuna kila dalili kwamba viongozi wa KCU (1990) Ltd. wanakitumia chama hicho kama kitegauchumi chao. Unasemaje kuhusu dalili hizo?
Muhandiki:Ni kweli kabisa. Mfano mmojawapo ni wa hizo hisa za CRDB. Pamoja na hisa hizo kuuzwa kwa bei ya kutupa pesa zilizopatikana inaonekana zilikwenda mifukoni mwa viongozi wa ushirika. Maana haiwezekani zikawa zimewekwa mahali fulani ushirika ukaendelea kulia na deni la CRDB ambalo nalo halijulikani chama kililifanyia nini.
Karugendo:Ni mambo gani ambayo wewe, kama mwakilishi wa chama cha msingi, unaona yangekinyoosha chama kama yangefuatwa?
Muhandiki:Yapo mambo kadhaa. Kwanza chama kinakosa uwazi, kama ilivyo kaulimbiu ya ushirika kote ulimwenguni. Kila kitu kinachofanywa kwenye KCU kinafanywa siri kiasi cha baadhi ya wafanyakazi kuachishwa kazi kwa madai kwamba wametoa nje siri za ushirika!
Uongozi wa ushirika unafanya hivyo bila kuelewa kwamba hiyo ni kinyume kabisa na mwenendo wa ushirika. Sababu mambo yote ya ushirika yanapaswa kuwekwa wazi kiasi cha kila jambo linalofanyika ndani ya chama kuwekwa kwenye ubao wa matangazo ili kila mwanaushirika, hata asiyeshiriki vikao vua uongozi, aweze kuona
kilichofanyika au kuamuliwa.Uwazi wa aina hiyo ukijitokeza ni lazima KCU isonge mbele. Tatizo lililopo sasa ni kwamba hata viongozi waliopo hawajui wafanye nini kuendeleza chama, mawazo yao yote ni ya wafanye nini ili wanufaike wao binafsi bila wanaushirika kuelewa. Ni mambo hayo yanayowalazimisha wafanyie mambo uvunguni, au gizani. Na kwa mtindo huo ni lazima wanaushirika wapunge mkono wa kwaheri kwa chama chao kikuu cha ushirika,KCU (1990) Ltd.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512