Bukobawadau

RAIS UHURU KENYATTA WA KENYA AMJIBU RAIS KIKWETE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe akimsindikiza  mgeni wake Waziri mwenza wa Kenya, Amina Mohammed baada ya waziri huyo kumaliza  kuzungumza na waandishi wa habari Dar Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman. 

Ni kufuatia hotuba aliyoitoa mwishoni mwa wiki kuhusu hali tete iliyoanza kujitokeza katika Jumuiya hiyo inayojumuisha nchi Tano.

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku nne baada ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia Bunge mjini Dodoma akilalamikia kutengwa na nchi washirika Afrika Mashariki,Kenya imekuwa ya kwanza kutamka hadharani kushirikiana na Tanzania.

Rais Kikwete katika hotuba yake,alielezea kushangazwa na washirika wenza wa Afrika Mashariki,Kenya,Uganda na Rwanda kufanya mikutano ‘kimyakimya’ bila kuwashirikisha.

Inadaiwa baada ya mkutano wa Aprili 28,mwaka huu mjini Arusha,wakuu hao wa nchi za Kenya,Uganda na Rwanda walikutana kimyakimya Juni 25 na 26,Entebbe nchini Uganda kabla ya kukutana tena Oktoba 28, Mjini Kigali,Rwanda katika mkutano waliouita “coalition of the willing”(Ushirikiano wa hiyari) wenye nia ya ujenzi wa Afrika Mashariki mpya.

Kupitia Waziri wake wa Mambo ya nje wa Kenya, Amina Mohamed, Rais Uhuru Kenyatta ametuma salamu akisema kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba walijiingiza katika mazungumzo yake na Uganda na Rwanda kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta bila kufahamu kwamba ilikuwa inavunja misingi ya jumuiya hiyo.

Salamu hizo zilizowasilishwa na waziri huyo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,alisema kuwa hawaoni sababu hasa ya kuitenga Tanzania hasa kwa suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC).

Waziri Amina aliyewasili nchini juzi kuzungumzia ushirikiano huo alisema, Tanzania na Kenya ndiyo waasisi wa EAC hivyo hawawezi kuacha ife.

Cuf watoa neno

Chama cha Wananchi (Cuf),kimesema Tanzania itazame na kuzirekebisha kasoro zinazosababisha nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuamua kuitenga badala ya kulalamika na kutafuta huruma.

Mwenyekiti wa Cuf, Profesa ,Lipumba alisema kumekuwa na kasoro mbalimbali zinazosababisha Tanzania kulalamikiwa na kufikiriwa kukimbiwa.

Alisema taarifa kuhusu uamuzi wa nchi za Rwanda na Uganda kutotumia Bandari ya Dar es Salaam lisitazamwe kisiasa badala yake iangalia udhaifu na upungufu uliopo katika bandari hiyo.

“Rwanda na Uganda si pekee wanaolalamikia Bandari ya Dar es Salaam bali wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi zikiwamo Kongo, Zambia na Malawi nao wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu.”
Alisema bandari hiyo ina matatizo mengi yanayowakwaza wafanyabiashara na wengi wao wakiwamo wa nchi hizo zilizoamua kujiondoa.

“Bandari hii ina sifa ya ucheleweshaji wa kupakua shehena za mizigo kutoka kwenye meli,upakuaji makontena na vifaa vya magari,ukubwa wa tozo za bandari na barabara,uchakachuaji wa mafuta pamoja na ucheleweshaji wa mizigo kutoka bandarini…hizi ni miongoni mwa kero za kuangalia badala ya kulalamika,” alisema Profesa lipumba.

Alisema asilimia 90 ya biashara Tanzania na nchi za nje inapitia Bandari ya Dar es Salaam lakini kumekuwa na ushindani mkubwa kutoka bandari ya Mombasa ambayo inafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Aliongeza kuwa Bandari ya Dar es Slaam haifanyi kazi zake kwa ufanisi na Ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha, iwapo bandari hiyo itafanya kazi kwa ufanisi kama ile ya Mombasa, pato la taifa litaongezeka kwa dola bilioni 1.8 kila mwaka sawa na asilimia 7 ya pato la taifa la sasa.

Pia alisema ukilinganisha na Bandari ya Mombasa gharaza za Tanzania zipo juu kwa asilimia 22 kwa kontena huku tozo na ushuru zikiwa juu kwa asilimia 74 .
Next Post Previous Post
Bukobawadau