Bukobawadau

Wassira na kauli za ajabu, kuna umakini?

Na Prudence Karugendo

MWANZONI mwa juma hili tulikumbuka kifo cha mpendwa wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mtu ambaye sioni kama kuna mwingine katika miaka 100 ya karibuni ambaye Watanzania wataweza kumuenzi kama yeye.

Sababu zinazomfanya Nyerere apendwe na kuenziwa hata na kizazi ambacho hakikushuhudia uhai wake, kama mwanagu Livinus Mushobozi aliyezaliwa mwaka 2002, miaka 3 baada ya Mwalimu kututoka kimwili, ziko wazo kabisa.

Nyerere aliipenda nchi yake na watu wake kwa maana halisi. Yeye hakuwa tayari kumvumilia mtu aliyeidhalilisha nchi yake, utu wa mtu, hata awe wa nchi nyingine, achilia mbali kudhalilishwa kwa utu wa mwananchi mwenzake.

Mfano, Mwalimu aliwahi kuwafuta kazi viongozi mbalimbali kutokana na kauli zao chafu dhidi ya wananchi. Bila kuwataja wote, kuna kiongozi aliyesakamwa na wananchi kuhusu usafirishaji, yeye akabwabwaja kwamba wanaomsakama wanaweza kwenda kuzimu “they can go to hell”. Kiongozi mwingine akasema “Mwalimu kaamuru tusage hivyohivyo, kwahiyo sageni hata kama ni kuchanganya mawe na mbao, wananchi watakula tu” akimaanisha unga wa mahindi. Kumbe Mwalimu alikuwa anamaanisha kusaga bila kukoboa.

Wakati fulani watu waliokuwa wanawahoji washukiwa wa mauaji ya rais wa kwanza wa Zanzibar, Karume, walitoa kauli kwamba “twendeni tukale tukirudi tuwalawiti”, kwamba ni lazima watasema hawa. Kauli hiyo Nyerere akaidaka.

Wote hao Mwalimu hakuwavumilia hata kidogo, aliwawajibisha mara moja. Sababu walikuwa wanaudhalilisha utu wa wananchi wake. Maana yeye Nyerere alikuwa mtu aliyetokana na watu akiwatumikia watu hao.

Lakini katika mchakato unaoendelea kwa sasa wa kuiandika Katiba mpya ya nchi tunaona kuwa yamejitokeza mambo mengi ya ajabu. Wapo watu wakiwemo viongozi waandamizi waliodai tangu mwanzo kuwa hicho ni kitu ambacho hakiwezekani. Kwamba Katiba haiwezi kuandikwa upya sababu tayari ilikuwepo. Uko pia ni kuwadhalilisha wananchi.

Lakini viongozi makini, wanaoitwa wapinzani, wakashikilia msimamo wao huku wakiungwa mkono na umma wa Watanzania kwamba Katiba mpya ni lazima iandikwe.

Kuona hivyo, Rais Kikwete, kwa nia njema kabisa akiwa ameuangalia umakini waliokuwa nao viongozi wa upinzani, hakujali wapambe wake wanasemaje, akasema ni kweli, wapinzani wana hoja, lazima Katiba mpya iandikwe hata kama hilo halikuwa kwenye Ilani ya chama chake. Pale Kikwete alitumia tu busara ya ubaba, sababu rais ni baba wa nchi.

Ndipo rais akasema upelekwe Bungeni muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Lakini jinsi ulivyoshughulikiwa muswada huo na wabunge wengi wa chama tawala haikuwaridhisha wapinzani. Kwahiyo wapinzani wakaamua kwenda Ikulu kumuona rais pamoja na kumshauri asiutie mkono muswada huo.

Kinachojionesha ni kwamba wao, wapinzani, wanalitazama suala hilo kwa maslahi ya nchi, tofauti na wenzao wanaolitazama kwa maslahi ya chama na ya kwao binafsi, huku wakiwa wameegemea kwenye wingi wao Bungeni.

Rais naye, kwa kuyaangalia maslahi ya nchi, akakubaliana na wapinzani lakini akiwaomba autie mkono muswada huo ili baadaye apeleke marekebisho Bungeni. Na kweli rais alifanya hivyo.

Baada ya hapo ukapelekwa muswada mwingine ambao nao umepitishwa kiubabe na wabunge wa CCM kama ilivyo kawaida yao, kiasi cha wabunge wa upinzani kuususia vilevile.

Baadaye ndipo waziri, Stephen Wassira (Ofisi ya Rais – Mahusiano na Uratibu) na wenzake wawili, Lukuvi na Chikawe wakiungwa mkono na Mwanasheria Mkuu, Jaji Werema, wakaanza kuwakebehi wapinzani. Katika kebehi hizo ndipo Wassira akatamka kwamba mara hii wapinzani wasitarajie kwenda tena Ikulu kunywa chai na juisi! Hilo ndilo lengo la makala hii. Tushirikiane pamoja kuitafakari kauli hiyo ya Wassira.

Ninachojiuliza ni kwamba huyu Wassira, mtu mzima na mwelewa, anataka Watanzania wamwangalie vipi? Hivi ni kweli Wassira yupo katika nafasi ile kwa kufurahia tu gari, shangingi, viyoyozi kwenye ofisi na mambo kama hayo ya chai na juisi, au kuitumikia nchi yake na wananchi wenzake?

Mtu aliye tayari kuitumikia nchi yake na wananchi wenzake anawezaje kuwaza mambo ya juisi na chai badala ya kuwaza mustakabali wa nchi yake? Je, huyu ni mtu makini anayepaswa kuwa kwenye safu ya wasaidizi wa kiongozi mkuu wa nchi? Ana tofauti gani na wale niliowataja mwanzoni kuwa waliwajibishwa na Baba wa Taifa baada ya kuonesha utovu wa umakini kwa wananchi?

Wassira anajionesha wazi asivyokuwa makini, sababu umakini uendana na uvumilivu, hivyo vitu viwili vikiachana panatokea ombwe. Sababu tukijikumbusha tutaona kwamba baada ya Wassira kuishiwa uvumilivu ndani ya CCM alitimkia NCCR Mageuzi, baadaye sijui chama gani na kisha akaenda chama kingine tena kabla ya kugeuka nyuma na kurudi CCM.

Kwahiyo kwa kutumia kauli yake mwenyewe, ni kwamba huko kote alikuwa anatafuta chai na juisi, akiikosa anahamia kwingine!

Kwa mantiki hiyo, mtu yeyote aliye makini, katika nafasi aliyopo Wassira anatakiwa ajiondoe mwenyewe kwenye nafasi hiyo baada ya mawazo yake kupishana na ya bosi wake, rais.

Haiwezekani uendelee kumshauri rais mambo anayoyaona ni upuuzi na wewe uone sawa tu na kubaki kwenye safu ya wasaidizi na washauri wake. Labda kama lengo ni hilo tu la kunywa chai na juisi Ikulu.

Sababu Wassira alisema kwamba milango ya Ikulu imefungwa, kwamba wapinzani wasitarajie kwenda tena Ikulu kunywa juisi na chai, bosi wake akampuuza, akasema milango ya Ikulu iko wazi kwa majadiliano. Hiyo ni kwa sababu kiongozi wa nchi anaangalia musitakabali wa nchi yake wakati msaidizi wake anawaza juisi na chai.

Hilo tu lilitosha kumfanya Wassira aachie ngazi hasa baada ya kuwashuhudia viongozi wa upinzani wakiingia Ikulu kwa mara ya pili, kitu ambacho Wassira alikuwa anasisitiza kwamba kisingetokea kamwe.

Hivi kweli tuendelee kuamini kuwa huyu ni mtu mwema kwa nchi hii? Mtu anayemshauri mkuu wa nchi mambo ambayo sote tunaona kuwa hayawezekani kwa vile hayana nia njema na nchi, huku kiongozi wa nchi naye akidhihirisha kwamba hautilii maanani ushauri wa mtu huyo!

Nakumbuka Mwalimu Nyerere alisema kwamba kama mtu ni rafiki yako unaweza kumkaribisha kwako kupiga naye soga pamoja na kunywa naye mvinyo, lakini si kumweka kwenye utumishi wa umma kama unamuona hafanani na umma.

Kitendo cha Wassira kuifikiria Ikulu katika kiwango cha juisi na chai tu kinamuonesha kuwa hafanani hata kidogo na umma anaopaswa kuutumikia.

Sababu ni kwamba Ikulu ni sehemu takatifu, ni sehemu ya umma wote wa Watanzania, utakatifu huo unakuja kwa umma wa Watanzania kumpata mtu unayeamini kuwa ndiye anayefaa kuikalia sehemu hiyi kwa muda fulani.

Hivyo Wassira kusema kuwa milango ya Ikulu imefungwa, tena yanapotakiwa kujadiliwa mambo nyeti yanayohusu mustakabali wa umma, ni sawa kabisa na kuudhalilisha umma. Huyu ni mtu ambaye tayari kaishajitenga na umma, anapaswa kuachana nao kwa kujiondoa kwenye nafasi hiyo ya juu ya kuutumikia umma.

Kama yeye halioni hilo basi bosi wake angemsaidia kuliona na kulitekeleza. Hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Mwalimu Nyerere. Maelezo mazuri kuhusu hatua ya aina hiyo yanaweza yakapatikana kwenye kitabu cha Mzee Edwin Mtei, From Goatherd to Governor, ambacho ni cha maelezo ya maisha binafsi ya Mzee Mtei.

Mle Mzee Mtei anaeleza alivyokwenda nyumbani kwa Mwalimu, Msasani, akiwa Gavana wa Benki Kuu, akiwa ameongozana na mgeni kutoka Benki ya Dunia. Lakini kutokana na Mwalimu kutofautiana na watu hao wa Benki ya Dunia, aliwasalimia tu Mzee Mtei na mgeni wake, kisha akenda zake kujisomea kitabu chake kwenye busitani nje. Baada ya hapo Mzee Mtei hakufanya lingine isipokuwa kwenda ofisini na kuandika barua ya kujiuzulu. Je, hayo kwa sasa yameenda wapi?

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau