Bukobawadau

Watanzania tusiwe kama nyumbu kwa Chadema


Na Elia Kwayu

NYUMBU ni wanyama wa ajabu, nadhani ni wanyama walio na akili ndogo kuliko wanyama wote wa porini. Wanyama hao wakishaamua kufanya kitu watakifanya tu bila kujali ni madhara gani yatatokana na uamuzi wao.

Mfano nyumbu wanaweza kuwa na kiu wakaamua kwenda kunywa maji kwenye mto uliojaa mamba. Kwa wingi wao watafika mtoni na kuanza kunywa maji huku mamba wenye njaa kali wakijikamatia nyumbu mmoja mmoja wakizamisha majini na kujitafunia. Nyumbu waliobaki wataendelea kunywa maji bila kujali yanayowakuta wenzao, wakimaliza kunywa maji wanaondoka zao, lakini wakisikia kiu tena wanarudi palepale bila kukumbuka kuwa kuna wenzao waliotafunwa, na wanaendelea kutafunwa wengine!

Au wakati mwingine nyumbu wanaweza wakaamua kuvuka mto wenye kina kirefu, kwa kuutegemea wingi wao, wataingia kwenye mto ambapo karibu nusu yao watabaki maiti katika mto huo wenye kina kirefu huku wengine wakifanikiwa kuvuka.

Daima hayo ndiyo maisha ya nyumbu, kukilenga ili wakitimize kile wanachokiangalia kwa wakati huo bila kujali madhara ya baadaye.

Tofauti na nyumbu binadamu tumejaliwa akili, pamoja na matatizo na shida tunavyoweza kuwa navyo, katika kuvikabili ni lazima tupime madhara na faida ya kufanya hivyo. Kama madhara yanazidi faida tunaona bora tuache. Ni heri mtu kubaki na shida au matatizo kuliko kutoa uhai kwa tamaa ya kutaka kumaliza matatizo au shida.

Kwa nini nasema hivyo? Kwa sasa kuna mageuzi ya kisiasa, hasa katika nchi nyingi za Kiafrika, ambapo vyama vikongwe vya siasa, hasa vilivyopigania uhuru wa nchi vinazozitawala na kuupata toka kwa wakoloni, vinapata shinikizo toka kwa vyama vya upinzani la kuvitaka vyama hivyo vikongwe vikae pembeni na kuviachia vyama vipya vya upinzani kutawala.

Shinikizo hilo limefanikiwa katika baadhi ya nchi, ambapo vyama vya upinzani vimeviondoa madarakani vyama vikongwe. Lakini hatahivyo baada ya kuchukua madaraka, vyama vilivyokuwa vya upinzani, vimeshindwa kuionyesha neema viliyokuwa vikiimba kabla ya kuingia madarakani. Na badala yake vinafanya vibaya zaidi kuliko hata vyama vikongwe vinavyoondolewa madarakani.

Kabla sijaendelea naomba nieleweke. Sio kwamba naikataa demokrasia, mimi ni mpenzi mkubwa wa demokrasia, ila ninachokikataa ni demokrasia hiyo kutugeuza nyumbu ambaye kiu ya maji inamsahaulisha kuwa ndani ya mto kuna mamba, hivyo badala ya nyumbu kumaliza kiu yake akaishia kuumaliza uhai wake.

Ninachokitaka na kukiomba kwa Mungu ni demokrasia kwa maana halisi, demokrasia itakayotufanya tuyapate mabadiliko tutakayoyataka na kutuacha salama. Nadhani hiyo ina tofauti na mageuzi yanayoimbwa na walio wengi.

Sababu mabadiliko na mageuzi ni vitu viwili vinavyotofautiana, mabadiliko yanakuja taratibu kwa wanaoyataka kupata muda wa kuyatafakari ili wakayapate yaliyo mema. Lakini mageuzi hayatoi muda wa kutafakari.

Jambo la kusikitisha ni kwamba hapa nchini kwetu kuna kila dalili ya kutokea mageuzi. Watu hawaonekani kutafakari kuhusu kitu wanachokitaka kinachoweza kuwa mbadala wa kile walichokichoka. Wao wanachokitaka ni kukiona cha zamani kinaondoka na kuja kingine bila kujali kinachokuja kimekaaje, ilimradi tu yawepo mageuzi.

Mfano kuna Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chama hicho kinaonekana kupata ushabiki wa kisiasa kwa kasi sana. Naamini kabisa kwamba wananchi wametokea kukishabikia chama hicho bila kupata muda wa kutafakari kwanza. Wao wanachokiangalia ni mageuzi lakini hawajali mageuzi hayo yana nini ndani yake.

Hebu tukakiangalie hicho chama. Chadema kinaundwa na idadi kubwa ya vijana. Na kawaida ya vijana walio wengi hupendelea mageuzi badala ya mabadiliko, yaani kitu tunachoweza kukiita bandika bandua, hapo tuelewe hakuna muda wa kutafakari. Vijana mara nyingi hawana muda wa kuyapima mema na mabaya yaliyomo katika mageuzi wanayoyatamani na kisha kuyalinganisha.

Mfano wa hivi karibuni ni wa tukio lililotokea kwenye mkutano wa Kanda wa Chadema kule Arusha. Kutokana na sababu ambazo haziko wazi, kundi la vijana waliomchoka mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, likiongozwa na mbunge wa Arusha Mjini,Godbles Lema, liliuvamia mkutano huo wa kanda kwa mtindo wa shambulizi la kigaidi na kuanza kumchapa ngumi mwenyekiti huyo wa mkoa bila kuheshimu wala kufuata kanuni yoyote ya mkutano uliokuwa ukiendelea.

Kilichodaiwa ni kwamba eti Mwigamba aliandika mambo fulani kwenye mtandao wa kijamii. Kwahiyo vijana hao wakadai kwamba Mwigamba afukuzwe kwenye nafasi zake zote alizokuwa akizishikilia kwenye chama hicho. Wala Mwigamba hakupewa kwanza nafasi ya kujitetea kufuatia uvamizi huo wa kigaidi. Kwahiyo demokrasia iko wapi? Kilichoangaliwa pale ni mageuzi na sio demokrasia.

Nikirudi upande wa pili, tutaona kwamba Mwigamba ni mtu anayeipenda Chadema kuliko watu wengi walio wanachama wa chama hicho.

Naweza kusema kwamba bila yeye, Mwigamba, si ajabu Lema asingejuwa mbunge kwa wakati huu. Lakini inaonekana Lema anauangalia ubunge kuliko anavyokijali chama, pengine ndiyo maana akaongoza uvamizi huo ili kumchafulia Mwigamba kwa hofu ya kwamba pengine Mwigamba anaweza akautamani ubunge katika uchaguzi ujao na hivyo kumnyang’anya Lema kitumbua mdomoni.

Katika hatua nyingine ni kwamba yaleyale yaliyodaiwa na Lema kwamba Mwigamba aliyafanya kiusaliti, kuandika kwenye mtandao wa kijamii kukikosoa chama chake, naye Lema kayatumia vilevile kuwashambulia viongozi wa chama chake!

Lema kautumia mtandao wa kijamii kumshambulia Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zubeir Zitto maarufu kama Zitto Kabwe, akidai kwamba ni mtu mnafiki.

Hebu fikiria mtu aliyemshambulia mwenzake kuwa katenda kosa fulani analitumia kosa lilelile kuwashambulia wenzake kwa mtindo uleule, akiliona kosa hilo kuwa ni halali kwake!

Lakini hatahivyo tukiziangalia tuhuma zilizotolewa na Lema dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa chama chake pia tutagundua kitu kingine. Ni kwamba Zitto Kabwe muda wote amekuwa akijipambanua kama mzalendo wa kweli wan chi hii, mtu aliye na uchungu na nchi pamoja na watu wake. Mpaka Zitto akafikia hata kuzikataa posho za vikao vya bunge, wananchi wakamuona mzalendo kwa hilo.

Lakini kumbe mtu anayekataa kupokea shilingi 70,000/= kama posho ya kikao cha bunge anapokea kati ya shilingi 700,000/= na 1,000,000/= kama posho ya kikao cha Kamati ya Bunge anayoisimamia! Hivi kweli kuna uzalendo hapo? Huyu ni mzalendo au anayewageuza wazalendo kuwa matuyuyu?

Hayo niliyoyataja ni baadhi ya mambo machache yanayoonyesha mwenendo wa chama kinachotamaniwa na baadhi ya wananchi kuwa mbadala wa chama tawala. Hiyo ina tofauti gani na nyumbu wenye kiu kwenda kunywa maji kwenye mto uliojaa mamba?

Sababu yanayojitokeza kwenye chama hicho kikuu cha upinzani yanaonekana madogo kwa vile chama hicho hakijapewa ridhaa ya kuvisimamia vyombo vya dola, lakini pindi wananchi wakikipa ridhaa hiyo sitaona ajabu yakitokea hapa nchini kwetu kama yale ya Renamo kule Msumbiji, Unita kule Angola, M 23 kule Congo nakadhalika. Maana hayo yote ni matokeo ya uasi katika uendeshaji wa nchi, ambao tayari unajionyesha ndani ya Chadema.

Waswahili walisema kwamba dalili za mvua ni mawingu. Yanayojionyesha ndani ya Chadema kwa sasa yanaashiria hayo niliyoyataja kama chama hicho kinapewa ridhaa ya kutawala nchi.

Je, Watanzania tunakubali kugeuzwa nyumbu?
Next Post Previous Post
Bukobawadau