Bukobawadau

Mkanganyiko katika Elinu ni uzembe au mwanzo wa matabaka?

Na Prudence Karugendo

YANAYOJITOKEZA kwenye elimu nchini yameibua maoni ya kila aina toka kwa wananchi. Yapo maoni ya kwamba serikali inafanya makusudi kuiua elimu nchini ili kujenga taifa la mazuzu ambalo halitakuwa na uwezo wa kuyafuatilia mambo nyeti yaliyo muhimili wa nchi yetu.

Kwa maana hiyo eti, kwa siku za baadaye, maliasili za nchi zitaweza kuzolewa bila ya kuhojiwa kwa vile ambao wangehoji kuhusu suala hilo watakuwa hawana uwezo huo wa kufanya hivyo.

Maoni hayo yana ukweli wa aina fulani, ila ninachokiona mimi katika sakata hili la elimu nchini kina utouti kidogo. Ni kweli kwamba kuna makusudi, yaliyojichanganya kwenye uzembe wa wasimamizi wa elimu, ya kutaka kuishusha kiwango elimu yetu. Lakini kilicho kikubwa ninachokiona ni cha kutaka kutengeneza matabaka yasiyoondosheka kama tunayoyashuhudia katika baadhi ya nchi duniani.

Kwa miaka ya karibuni kwa mfano, kulijitokeza kampeni kamambe ya kutaka elimu nchini iendeshwe kwa kutumia lugha ya Kiswahili tu kuanzia shule za chekechea hadi vyuo vikuu, badala ya kuichanganya na Kingereza kama ilivyo kwa sasa. Kwa jinsi nilivyoelewa waliokuwa wanaendesha kampeni hiyo walikuwa na sababu kuu mbili, kwa mtazamo wangu.

Kwanza kulikuwepo madai kuwa wanapenda kuinua lugha yetu ya Kiswahili pamoja na kuinua uelewa wa wanafunzi wanaolazimika kutumia lugha ya kujifunza ili kujifunzia, yaani kujifunza lugha kwanza, Kingereza, na baadaye kuitumia lugha hiyo kujifunzia masomo mengine.

Sababu hiyo iliyotolewa ni ya kweli na ina mashiko, lakini walioileta na kuiweka mbele yetu hawakuwa wakweli. Na hilo ndilo linalonifanya niitilie mashaka mpaka sasa, na hivyo kulazimika kuiangalia sababu nyingine ambayo hawawezi kuiweka wazi.

Kitu kinachoshangaza mpaka sasa ni kwamba waliokuwa wanaongoza kampeni ya kutumia Kiswahili kama lugha ya kujifunzia hapa nchini, ukiwachunguza kwa umakini utaona kuwa hakuna hata mmoja ambaye anapenda watoto wake wasome kwa kutumia Kiswahili! Karibu wote wanaoongoza kampeni hiyo wanawapeleka watoto wao kwenye shule za Kingereza, “English Medium Schools”, shule ambazo kwa hapa nchini zimezoeleka kama “International Schools” au wakati mwingine zikiitwa “academies”, au kuwapeleka watoto wao nje ya nchi.

Tunalopaswa kujiuliza ni kwamba watu hao wanaosema Kiswahili ndicho pekee kitumike kufundishia nchini wanawapeleka watoto wao kwenye hizo “academies” na nje ya nchi wakajifunze kwa Kiswahili sanifu au kupata uelewa mzuri kwa kutumia hiyo Lugha ya Taifa? Sasa kama watoto wao wanapelekwa wakasome kwa Kingereza ni watoto wa nani wanaowataka wakajifunze kwa Kiswahili kwa kipindi chao chote cha masomo?

Mpaka hapo tutaona kuwa mpango mzima wa kutaka Kiswahili ndicho pekee kitumike kwenye elimu ya nchi yetu, umezingirwa na mpango mwingine uliojificha wa kutaka kujenga matabaka ndani ya jamii yetu. Yaani wawepo watoto waliosoma kwa Kiswahili pekee na waliosoma kwa Kingereza pamoja na lugha nyingine za kimataifa. Hilo lina maana kubwa katika mpango uliojificha wa kutengeneza matabaka hapa nchini mwetu.

Sababu tukishakubali mambo yawe hivyo, kuwa na watoto waliojifunza kwa Kiswahili tu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, katika ajira au uongozi wa nchi zitaanza kutolewa sababu za kuwapa kipaumbele wale waliosoma kwa kutumia lugha za kimataifa. Zitatolewa hoja kwamba waliosoma kwa Kiswahili pekee hawawezi kuwasiliana vizuri na watu wa mataifa mengine. Kwahiyo wao wabaki kuwa chini ya wale waliosoma kwa kutumia lugha za kimataifa.

Mpangilio wa aina hiyo, matabaka katika jamii, ndio unaoongoza katika nchi kama India. Mtu anayezaliwa katika tabaka la masikini hana njia nyingine ya kujinasua katika tabaka hilo na kuingia kwenye tabaka la juu yake. Atabaki hivyo kwenye tabaka la masikini maisha yake yote.

Ni kwamba kwa mpangilio wa aina hiyo ya elimu tayari matabaka yanakuwa yamejitengeneza yenyewe hapa nchini kwetu. Mambo hayo sio kwamba nayasema kwa kubuni tu, ila natumia ukweli ambao unajionesha. Mara kadhaa tulisikia kwenye kampeni za ubunge na urais ikisemwa kwamba mgombea fulani hawezi kujieleza kwa Kingereza, hivyo hafai kuchaguliwa, hata kama mgombea huyo ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili!

Kwa maana hiyo mapenzi kwa Lugha ya Taifa yanabaki kwenye nadharia tu, lakini kivitendo lugha hiyo inatumika kusimangana, kwamba fulani hawezi kitu kwa vile anaongea Kiswahili tu!

Kama ungekuwepo msukumo wa kweli wa kutaka kuiinua lugha yetu ya Kiswahili pamoja na kuwarahisishia uelewa watoto wa Kitanzania, basi ingetengenezwa sheria itakayolifanya kuwa kosa la jinai tendo la mtu kumsomesha mtoto kwenye shule zinazofundisha kwa Kingereza au kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya masomo. Hiyo ingeenda sambamba na kuzipiga marufuku nchini shule zote zinazofundisha kwa Kingereza.

Lakini kama ni rukhsa kuendelea kuwepo shule zinazoitwa za kimataifa huku zikiimizwa shule nyingine za kata basi ieleweke kwamba kinachotafutwa sio elimu bali matabaka.

Ndiyo maana tunaona kwamba serikali imefikia kuleta kinachoitwa mfumo mpya wa ufaulu. Mfumo ambao lengo lake hasa ni kuwaremba watoto waliofeli katika mitihani mbalimbali ya kitaifa ili nao waonekane wamefaulu japo kwa kiwango fulani, badala ya kuonekana wamefeli kabisa na hawajui lolote! Kwakweli hicho ni kilemba cha ukoka.

Mwaka juzi walizolewa watoto kibao wasiojua kusoma wala kuandika na kupelekwa kidato cha kwanza! Hiyo haikuwa bahati mbaya hata kidogo, ni mambo yaliyopangwa makusudi ili watoto hao wakawasindikize wale waliosomea kwenye shule za “English Medium”, wakati nchi ikijilazimishia sifa isiyo ya kweli kwamba imewawezesha watoto wengi kwenda kidato cha kwanza. Kumbe watoto hao ndio wanaoburuzwa hadi kidato cha nne wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

Sasa kama mtoto anamaliza kidato cha nne akiwa hajui kusoma na kuandika atawezaje kufaulu mtihani wa kidato cha nne? Si ni lazima apate sifuri? Ndio hao ambao, serikali kwa kutaka kujitoa aibu, inawaremba kwa kuondoa neno sifuri na kuweka daraja la tano ili nao wajione wameshinda.

Hata kama waliopata sifuri watajiona wameshinda kwa daraja la tano au wakati mwingine nao kuburuzwa mpaka kidato cha tano, kwa mpangilio wa kielimu unaojionesha wa nchi yetu, sitashangaa tukipata wanafunzi wa chuo kikuu wasiojua kusoma na kuandika. Sababu, kwa upande mwingine, kinachoangaliwa ni Matokeo Makubwa kwa Sasa na wala sio Matokeo Mazuri kwa Sasa.

Maana mwanzo kinacholengwa ni wanafunzi kuonekana wamefaulu kwa wingi. Uelewa ni jambo lisilopewa umuhimu wowote. Isingekuwa uelewa unapewa umuhimu serikali ikahangaika kushusha viwango vya kupasi pamoja na kuondoa maneno ya kufeli na sifuri huku ikiongeza daraja la kufaulu hadi daraja la tano.

Lakini ikumbukwe kwamba matokeo hayo yanawalenga watoto wa walalahoi, waliosomea kwenye shule za “Kayumba”, na sio waliosomea nje ya nchi.

Serikali inayojali uelewa wa mtu ingekuwa inakazania kiwango cha uelewa, kwa maana hiyo daraja la nne lingeondolewa, kwa maana ya mtu anayepata alama za daraja la nne kuonekana amefeli, na kutotakiwa kumwendeleza mahali popote kielimu isipokuwa kukariri darasa.

Lakini kwa sasa serikali imeamua kuwaburuza tu wasiojua chochote ili wakawasindikize wanaojua, kusudi wakifikia kiwango cha kutafuta ajira ndipo wale wasiojua chochote wakamatwe, wengi wao watakuwa hawajui kusoma na kuandika, hawajui Kingereza na mambo mengine kibao. Kwahiyo watu hao waliosomea kwenye shule za “Kayumba” watabaki kutumikishwa na wale waliosomea kwenye shule za Kingereza na wengine waliotoka kusomea nje ya nchi.

Nani atabisha kuwa hapo hakuna matabaka?

Watoto wote ni wa Watanzania sawa, lakini wapo waliosomea kwenye shule za Kingereza na waliosomea kwenye shule za kata. Wapo ambao watakuwa wamefaulu kweli mitihani na wengine kupata sifuri lakini wakiambiwa wamepata daraja la tano! Wapo watakaokuwa na uwezo wa kuwa mameneja na wengine kuishia kuwa wafagiaji. Wapo watakaokuwa na uwezo wa kugombea ubunge na wengine kuishia kuimba “Chama kina wenyewe” huku wakiwasindikiza wale wanaopata ubunge.

Hayo ndiyo matabaka ninayoyaona yanayojengwa.

Tuelewe kwamba hiyo ni aina ya matabaka ambayo hatuwezi kuiondoa ikishajisimika. Msingi wake unaanzia kwenye elimu tukiwa tunaangalia na kushangaa bila kuchukua hatua yoyote.

Ni kwamba tunapotaka matokeo bora kielimu, kwa matokeo yasiyo ya kibaguzi, ni lazima tuwekeze kwenye elimu kwa maana halisi kitaifa. Tuwekeze bila kujali nani ni mtoto wa nani. Tuhakikishe kwamba aliyeshinda kashinda kiukweli na aliyeshindwa kashindwa kiukweli. Pasiwepo na kuyaonea haya maneno ya sifuri na kufeli ambapo yanaletwa maneno mbadala ya kuvishana vilemba vya ukoka, mara daraja la tano, mara kufaulu kiudhaifu nakadhalika.

Kitu kinachosahaulika ni kwamba elimu ndiyo taaluma ya kwanza, taaluma ambayo mtu anapitia kuzifikia taaluma nyinginezo.

Bila mwalimu bora hatuwezi kumpata mhasibu bora, bila mwalimu bora hatuwezi kumpata daktari bora, hatuwezi kumapata mwanasheria bora, mhandisi bora nakadhalika.

Kwahiyo kinachotakiwa ni kuwapata walimu bora kwanza. Na ili tuwapate walimu bora hatunabudi kuyatengeneza kwanza mazingira ya uwalimu kusudi yawe na mvuto bora. Mvuto kama uliomo kwenye nafasi za makalani wa benki, wahasibu wa TRA nakadhalika.

Bila kuyaangalia hayo tuelewe kwamba tunayakaribisha kwa nguvu matabaka ambayo yanajengwa na kusimamiwa na serikali yetu.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau