KWA HERI 2013, NAJUA UMEWATESA VILIVYO WATANZANIA
Leo, ninafanya hivyo nikiwa mwenye furaha tele,
nakutakia heri ya mwaka mpya, yaani 2014, mwaka ambao panapo majaliwa
tutauanza hapo keshokutwa.
Ninasema kwa wiki 51 kati ya 52 mwaka huu nimekuwa
nawe bila kukosa. Ni wiki ambazo sikukosa kuwa nawe, ingawa kwa wiki
moja sikuonekana.
Ninatambua vizuri wajibu wangu kwako kwani kwa wiki ile moja ambayo hukuwa nami, hakika ulinikosa.
Kwa bahati mbaya, sikupata nafasi ya kukuomba
radhi msomaji wangu mtukufu kwa kukunyima uhondo ule wa siku zote ambao
kwa zaidi ya miaka minne umeupata kupitia safu hii.
Kwa kipindi hiki cha karibu miaka minne huenda
nimekukwaza kwa namna moja au nyingine, naomba unisamehe, kama ambavyo
pia ninafanya hivyo kwako.
Kwa pamoja tunaukamilisha mwaka hapo kesho,
lakini, ni mwaka ambao kama ilivyokuwa mingine iliyotangulia,
tumeshuhudia mambo mengi yakiwamo yale ambayo hakika hayakuwa yenye
kupendeza au hata kuvutia. Hata katika familia moja moja, jamii au hata
kitaifa, tumepitia katika mambo mengi magumu ambayo siwezi kuyaorodhesha
hapa chini.
Kikubwa, kama taifa tulifanikiwa katika moja, lile la kuendelea vyema na mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Nimeambiwa kuwa leo, mchakato huo unaingia hatua yake ya pili kwa Rais Jakaya Kikwete kupokea rasimu ya pili.
Ninaamini kazi iliyofanywa kwa umakini, umahiri
mkubwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba , chini ya Jaji Joseph Sinde
Warioba na wenzake wengi ni ya kupongezwa. Hata hivyo, niitaje kazi ya
tume hiyo, nikigusia pia kifo cha mjumbe wake, Dk Edmund Sendongo
Mvungi aliyefariki dunia miezi michache iliyopita na kuiacha kazi hiyo
ikiwa bado jikoni.
Ninachukua nafasi hii kumwombea pumziko la milele,
Dk Mvungi pamoja na Watanzania wengine wote ambao wamepoteza maisha
yao, mwaka 2013 kwa sababu zozote zikiwamo za ukatili wetu, sisi
binadamu.
Kwa wenzetu, wale ambao wamefariki dunia kwa ajali
za aina mbalimbali kama za barabarabani, angani, majini, kwa hakika
ninawakumbuka, pia nawaombea pumziko la milele, nikiomba Mwenyezi Mungu
awaangazie mwanga wa milele. Ninamkumbuka Padri Evarist Mushi wa Parokia
ya Minara Miwili, Jimbo Katoliki la Zanzibar ambaye aliuawa kikatili
kwa risasi, siku ya Jumapili, Februari 17
Matukio haya ya ukatili yalikuwa mengi, kama nilivyoeleza awali
ni pamoja na kuvamiwa, kupigwa, kuumizwa kwa Mhariri Mtendaji wa gazeti
la Mtanzania linalomilikiwa na New Habari Corporation, Absalom Kibanda.
Kibanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania alivamiwa wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Beach
jijini Dar es Salaam, Machi 6, 2013 na kisha kuumizwa vibaya sehemu
mbalimbali za mwili wake na hadi sasa ingawa amepata nafuu baada ya
matibabu ya gharama kubwa kule Afrika Kusini, hatuambiwi sababu, chanzo
na hata wahusika wa tukio hilo.
Kama vile haitoshi, Padri Anselmo Mwang’amba, pia
kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar alivamiwa na kumwagiwa tindikali kama
ilivyokuwa kwa katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Soraga karibu
na mwisho wa mwaka 2012.
Tukio hilo la Septemba linazidi kutia chachandu
matukio hayo mabaya ya kikatili ambayo yameukumba mwaka ambao funguo
zake zinawekwa kando, lakini pia unatukumbusha mengi yaliyoitia doa nchi
yetu.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa wasichana wa
Kizungu kule Zanzibar, hadi sasa halijawekwa wazi na vyombo vya dola iwe
kule visiwani au Tanzania kwa jumla, ni aibu nyingine ambayo nchi yetu
haiwezi kujivua.
Wasichana hao,Kirstie Trup na Katie Gee, wenye
umri wa miaka 18 walikuwa visiwani humo kwa kazi ya kujitolea,
walimwagiwa tindikali Agosti wakati wakiwa matembezi eneo la Mji
Mkongwe , Zanzibar.
Jambo la kushangaza ni kuwa tangu wakati ule mbali
ya kuhudumiwa katika hospitali zetu, Mnazi Mmoja na Muhimbili, kisha
kusafirishwa kwenda kwao, Uingereza walikofanyiwa upasuaji wa
kurekebisha sura zao, hatuambiwi nani mhusika.
Nimesoma mahali wasichana hao wanamedhamiria
kurudi Zanzibar kuendelea na kazi zao, wanailaumu serikali yaani SMZ
(Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) au ile ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na pia
huenda hata ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosimamia vyombo
vya dola likiwamo Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kulinda
raia na mali zao.
Tukio jingine n mfanyabiashara wa Dar es Salaam,
ambaye naye alimwagiwa tindikali na kuumizwa vibaya katika mlolongo wa
matukio hayo mabaya yanayoupamba mwaka huu.
Tukio hili na jingine la Arusha kwa mfanyabiashara
mwingine, pia yote yaliyotangulia limebaki siri baina ya watendaji
wake, polisi wanaochunguza na jamii inayosubiri kuona kinachoendelea .
Tumeambiwa kuwa mfanyabiashara huyo na mmiliki wa
maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad alimwagiwa
tindikali kwenye maeneo ya Msasani City Mall, saa 2 usiku ambako
inadaiwa kuwa mhusika aliyekuwa na pikipiki alitoka mbio, eti juhudi
za mlinzi kujaribu kumkamata zilikwamishwa na utelezi.
Hata hivyo, kama nilivyoeleza mwaka unaisha, lakini cha moto Watanzania walio wengi tumepata.
Hali ya maisha yetu, wengi imeendelea kuwa duni, ngumu, karibu
kila kitu kimepanda bei, isipokuwa hewa ambayo Mwenyezi Mungu hugawa
bure.
Mategemeo ya wengi kupata hali nzuri, maisha bora
ambayo tuliahidiwa na Rais Kikwete wakati ule wa kampeni yake ya kuwania
muhula wa pili wa uongozi wake, mwaka 2010 kwa jumla yamebakia ndoto za
mchana.
Kisiasa, wananchi tumeendelea kusikiliza ngonjera
za viongozi wetu wakiwamo wabunge wakiwa Dodoma ambako hupigana
vijembe, kejeli nyingi au kelele lukuki ambazo hazina tija.
Kelele zao (wanasiasa) hazina mwisho ,hazielekei
hata siku moja katika kuwafikisha kokote Watanzania hasa katika safari
waendako, ile ya kuishi vizuri tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita.
Kama kidonda chetu Watanzania kimetiwa chumvi na
ndimu, maisha yetu, wakulima na wafugaji yamewekwa rehani na mapigano
baina yetu ambayo yamezikumba wilaya na mikoa mingi nchini.
Uhasama umezidi, wengi wanaishi mtihili ya chui na
paka, viongozi wetu wamekosa mbinu za kuimaliza mizozo hii, wameshindwa
kuandaa mipango ya kutenga maeneo ya kudumu ya mifugo na kilimo bila
bughudha.
Binafsi, nasema yote yanawezekana, endapo kuna
dhamira hasa kwa uongozi wetu wa ngazi mbalimbali kujaribu kufanya
hivyo. Kama nchi, tujaribu tuone, naamini tunaweza.
Mwananchi.
Mwananchi.