Tafsiri ya usaliti ya Zitto na umaarufu wa Kibuzwagi
Na Prudence Karugendo
WIKI mbili
zilizopita niliandika nikiishauri Chadema ifanye mambo yake kichama na sio
kimitandao. Nikaonyesha tofauti kati ya chama cha siasa na kikundi cha
wanaharakati.
Sasa nimefarijika
sana kuona Chadema inafanya mambo yake kichama, kwa maana halisi, ikiwa
imejitofautisha na kikundi cha wanaharakati. Chadema imefanya maamuzi magumu
kama chama kilichokomaa kwa kuwavua nyadhifa waliokuwa viongozi waandamizi wa
chama hicho bila kuujali umaarufu waliokuwa nao ndani ya chama hicho.
Sababu
umaarufu wa mtu mmoja mmoja ni tofauti na nguvu ya chama, maana yake ni kwamba,
kwa watu binafsi, umaarufu ni wa
wahusika ndani ya chama, na kwa chama, nguvu ya chama inajengwa na wanachama wote katika
umoja wao ambao ndio wenye chama. Kamwe vitu hivi viwili haviwezi kutunishiana
misuri.
Waliovuliwa
nyadhifa ni Kabwe Zubeir Zitto, maarufu kama Zitto Kabwe, aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu, Dk. Kitila Mkumbo, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, na Samson Mwigamba,
aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Arusha.
Watu hao
watatu wamevuliwa nyadhifa zao kutokana na kufanya usaliti na uhaini ndani ya
chama. Kilichothibitisha usaliti na uhaini wao ni waraka ulioandaliwa kwa siri,
unaoelekeza namna ya kufanya mapinduzi ndani ya chama. Lakini waraka huo ukaja
kufumaniwa na wataalamu wa chama na baadaye kuwekwa mikononi mwa viongozi wa
chama.
Ndani ya
kikao kilichowavua vyadhifa viongozi hao hawakusema lolote lenye kupingana na
hukumu iliyotolewa, sanasana Zitto alikiri kuwa chama kimefuata utaratibu wake.
Kwa ufupi ni kwamba walinyamaza, na kawaida ya mashtaka kunyamaza ni kukiri
kosa.
Lakini baada
ya siku tatu wavuliwa nyadhifa hao wakapata nguvu ya ziada iliyojionyesha
kwamba ilikuwa na msukumo toka nje ya chama, wakazungumza na waandishi wa
habari. Picha ya msukumo huo ilijiweka wazi baada ya watu wasiojulikana wala
kutambulika ndani ya Chadema, wakiwemo wana UVCCM, kuonekana ndio waratibu wa
mkutano huo!
Katika
makala hii nitamuangazia zaidi Zitto kutokana na sababu maarumu.
Utetezi wa
Zitto alioutoa kwa waandishi wa habari, badala ya kuutolea kwenye kikao cha
chama kilichomvua nyadhifa, kumbuka wanahabari sio waliomvua nyadhifa, ulikuwa
na mambo mbalimbali likiwemo la kwamba hasingeweza kukisaliti chama
alichokitumikia kwa zaidi ya nusu ya umri wake.
Utetezi wake
huo, moja kwa moja unahalalisha madai yaliyomuandama mpaka akavuliwa nyadhifa
zake kwenye chama. Sababu usaliti au kusaliti ni kitendo cha kwenda kinyume na
mwenendo mzima ambao mtu anakuwa ameapa au kuaminisha wengine kuwa ataufuata.
Anayotuhumiwa
na kushutumiwa nayo Zitto yako wazi kama nitakavyojaribu kuonyesha hapa chini.
Kwa vile
Zitto anasema mwenyewe kuwa ameitumikia Chadema kwa zaidi ya nusu ya maisha
yake, halafu baadaye akaonekana anaenda kinyume na mwelekeo wa chama chake,
hata kama kinakoelekea hakufai, basi akubali kuwa amekisaliti.
Mfano
Chadema haiwezi kusema kwamba Mwigulu Nchemba kaisaliti, sababu yule yupo
kuhakikisha kwamba Chadema inaporomoka na kuangamia, naye anajigamba hivyo. Kinyume chake ni usaliti
kwa chama anachokitumikia, CCM.
Kinachoweza
kulalamikiwa na Chadema toka kwa Mwigulu ni uvamizi na si usaliti, ila kwa
Zitto ni usaliti.
Kwahiyo wale
wote walioyumbishwa na kauli ya Zitto ya kwamba asingeweza kuisaliti Chadema
waelewe kuwa aliitoa kauli hiyo ili kuwafurahisha waandaaji wa wa mkutano wake
huo bila kuifanyia tafakuri tafsiri ya neno usaliti.
Tukirudi
nyuma kidogo, ni kwamba Zitto alikuwa ametokea kupata ushabiki mkubwa ndani ya
Chadema, baadhi ya wanachama na wapenzi wa chama wakampenda sana na kujenga
imani naye. Ikafikia wakati hata yeye akaanza kujiona kuwa ndiye Chadema na
Chadema ndiyo yeye!
Hivyo
akaanza kujiona kuwa yeye ndiye anayekipatia chama umaarufu. Kwahiyo umaarufu
wake akauona uko juu ya umaarufu wa chama. Hapo ndipo Zitto akanikumbusha wimbo
wa Kihaya wa “Nkurukumbi niyo yazaire Mahinja”, unaomaanisha kwamba mwanamke
mlemavu asiye na miguu wala mikono kutokana na ugonjwa wa ukoma, ndiye mama
mzazi wa mrembo aitwaye Mahinja. Kwahiyo usimpige wala kumtukana kama unamtamani
Mahinja.
Hebu
tuangalie nyuma tena ili tukajikumbushe ukweli ulivyo. Umaarufu wa Zitto
umeanzia Bungeni akiwa mbunge kwa tiketi ya Chadema, pale alipouvalia njuga mkataba
wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.
Baadaye
alisimamishwa vikao vya Bunge kwa kilichodaiwa kwamba alilidanganya Bunge,
Julai 2007.
Buzwagi,
neno la Kisukuma lenye asili ya Kisumbwa, lina maana ya mambo yanayojitokeza
kwa kuchipua bila mpangilio ulioratibiwa. Pengine mvua zimenyesha na majani
kujiotea, basi majani hayo ni buzwagi.
Kwahiyo hata
Zitto, kwa umaarufu alioupata kutokana na mkataba wa mgodi wa Buzwagi ambao
alikuwa hakuupanga yeye, ni umaarufu wa kibuzwagi. Umaarufu uliojitokeza bila
yeye kuutafuta.
Ni kwamba
baada ya Zitto kufukuzwa Bungeni, chama chake, Chadema, kilimbeba mgongoni na
kumzungusha karibu nchi nzima kikiyataja aliyoyasema na kumsababishia kufukuzwa
Bungeni. Hivyo Chadema ikawafanya watu wamuonee huruma kijana aliyeonekana ni
jasiri, huku wakichanga na wengine kuahidi kumchangia pesa kwa ajili ya kufidia
mshahara na posho alivyovikosa kwa kipindi chote alichokuwa nje ya Bunge.
Kwa maana
hiyo ni Chadema iliyompatia Zitto umaarufu tofauti na yeye anavyotaka
kuwaaminisha watu kuwa kakipatia chama hicho umaarufu.
Yeyote
anayeuelewa umaarufu wa Zitto kabla ya hapo aueleze na aseme alishaifanyia nini
Chadema kilicho zaidi ya wananchama wengine.
Chadema
imemjenga Zitto na kumpa umaarufu mkubwa uliouzidi uwiano wa umuhimu wake,
umaarufu wa kibuzwagi, ikitegemea
matokeo makubwa zaidi toka kwake. Lakini kinyume chake zikajitokeza tuhuma na
shutuma lukuki dhidi yake, zikiwemo za yeye kukikosesha chama hicho, tena kwa
makusudi, zaidi ya majimbo 50 ya uchaguzi. Hizo ni tuhuma na shutuma za
kukisaliti chama.
Mbali na
tuhuma zinazohitaji mlolongo mrefu kuzithibitisha, zipo tuhuma za wazi kabisa
za kwamba Zitto alikuwa na zaidi ya miezi saba bila kukanyaga kwenye ofisi za
makao makuu ya chama chake wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu! Je, hilo linaleta
picha gani zaidi ya picha ya usaliti?
Rafiki yangu
mmoja anayedai kuwa anapendelea kuongelea hoja bila kuwagusa watu wala
kuwajadili, anasema alivyousoma waraka unaotajwa bila kuona mahali popote
panapoonyesha usaliti wala uhaini.
Ni wazi
kwamba mtazamo wake unakinzana na maelezo ya watayarishaji wa waraka huo
waliokiri kwamba waraka husika ulikuwa wa siri. Kukiri kwa watayarishaji kuwa
waraka ulikuwa wa siri tayari ni kukiri kuwa ulikuwa wa kihaini.
Vingevyo
waraka huo ungekuwa wa wazi ukifuata taratibu zote za chama. Lakini usiri
ulioufunika waraka huo hauwezi kuondoa mashaka ya kwamba pengine ulikuwa
unaandaa vikundi kwa ajili ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama, kitu
ambacho ni uhaini uliopitiliza.
Tutaona
kwamba Chadema, kama ilivyokuwa ANC ya Afrika Kusini enzi za makaburu, ni chama
kinachopata msukosuko mkubwa toka kwa watawala. Watawala wanakisakama chama
hicho kwa njia zote hasa kwa kutumia nguvu za dola. Misukosuko hiyo wakati mwingine
inaonekana imelenga hata kupoteza uhai, uwe wa wanachama, wapenzi na hata wa
viongozi wa chama.
Ni jambo la
kushangaza kwamba karibu mara zote ambazo Chadema imepata misukosuko ya aina
hiyo, mikubwa na ya hatari, Zitto Kabwe huwa hayupo.
Nimepokea
simu nyingi na ujumbe mwingi wa maandishi toka kwa wanachama na wapenzi wa
Chadema wa sehemu mbalimbali nchini wakiuliza kwamba; kwa nini karibu mara zote
ambazo Chadema inakumbana na mabavu ya vyombo vya dola kiasi cha vyombo hivyo
kupoteza uhai wa wananchi na wanachama wasio na hatia Zitto huwa hayupo?
Wanasema sehemu nyingi anazokuwapo Zitto huwa hapatokei patashika
zinazosababishwa na mabavu ya vyombo vya dola.
Wanazitaja
sehemu kama Nyololo, Mfindi Iringa ambako viongozi wa Chadema walishambuliwa na
askari wa kikosi cha kutuliza ghasia na kuishia kuuawa mwanahabari, Daudi
Mwangosi, kwamba mbali ya kutokuwepo Zitto hajawahi hata kwenda kutoa pole!
Wanataja
Morogoro ambako aliuawa muuza magazeti katika shambulio lilionekana kuilenga
Chadema, Zitto hakuwepo wala hakwenda kutoa pole. Wanataja Soweto, Arusha,
ambako bomu lilirushwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema na kuua watu
kadhaa, Zitto hakuwepo na wala hajawahi kwenda kutoa pole!
Swali
wanalojiuliza ni kwamba hiyo inatokea tu kwa bahati aliyo nayo Zitto au huwa
anazo habari za kiintelijensia zikimtahadharisha asiende kwenye maeneo husika?
Yanasemwa
mengi kwa wakati huu, mengine kwa nia njema na mengine kwa nia mbaya. Lililo la
muhimu ni kuyatafakari maneno haya ili kuangalia ni lipi la kutilia maanani na
lipi la kupuuzia.
Mfano kwa
upande wangu sijawahi kumshabikia Zitto hata mara moja, maana mara zote
nimeyapima aliyoyafanya kuona kama kuna alichowazidi wengine na sijawahi
kukiona. Huwa namchukulia kama nilivyomuelezea hapo juu.
Ni kwamba
naamini kabisa kwamba umaarufu alio nao ni wa kibuzwagi, sio umaarufu
ulioratibiwa kutokana na juhudi zake binafsi, bali unaochipuka tu kutokana na
hali ilivyo. Kwa maana hiyo watu wote wanaoyapenda mageuzi ingebidi wafanye
tafakuri ili kumwelewa mtu huyu vizuri kabla ya kumwachia kuwapoteza kimkumbo.
0784 989 512