Bukobawadau

WANANCHI WASEMA KIPOFU KAONA MWEZI BAADA MRADI WA MAJI KUKAMILIKA NA KUTOA MAJI KATIKA MAKAZI YAO

Wananchi wa Rulenge Wilayani Ngara wasema kipofu kaona mwezi baada ya mradi wa maji kukamilika na  kuanza kutoa maji safi katika sehemu mbalimbali za makazi yao ambapo vimejengwa vituo vya kuchotea maji.
Mradi wa maji Rulenge umetekelezwa na kukamilika kwa asilimia mia moja na kugharimu kiasi cha zaidi ya  milioni 640 pia ni mradi mmojawapo kati ya miradi ya maji inayotekelezwa katika  vijiji kumi kwenye wilaya ya Ngara.
Mzee Nicholaus Karumna ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maji Rulenge alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Massawe alipofika Rulenge kukagua na kuhakikisha mradi ulivyokamilika, kuwa siku ya kwanza maji yalipoanza kutoka siku hiyo ilikuwa kama kipofu kaona mwezi.
“Mkuu wa Mkoa maji yalipoanza kutoka mara ya kwanza siku hiyo ilikuwa kama kipofu kaona mwezi, wananchi walipigana kuchota maji wakijua kwamba maji hayo yanatoka kwa muda kwa hiyo kila mmoja alipigana ili kuhakikisha anapata maji kabla ya kukatika.” Alieleza Mzee Nicholaus.
Mzee huyo aliendelea kusema kuwa maji yaliendelea kutoka tena kwa nguvu tangu siku hiyo bila kukatika, aidha  aliishukuru serikali kukamilisha mradi huo kwani hapo awali alisema wananchi walipata shida ya maji na kutumia maji ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu.
Pia mwananchi mwingine ambaye alikutwa katika kituo cha kuchotea maji Sokoni Rulenge Tatu Dominick alisema akina mama wanaishukuru serikali kwa kuwasogezea maji karibu katika makazi yao na maji hayo ni salaama kwa matumizi ya binadamu. Mradi huo baada ya kukamilika unahudumia wananchi wapatao 800
Kati ya miradi kumi ya maji vijijini katika wilaya ya Ngara mradi mmoja wa Rulenge umekamilika kwa asilimia mia moja na mradi wa maji Ngundusi umekamilika kwa asilimia 75 aidha miradi mingine mitano inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2014 na mitatu itakayokuwa imebaki itakamilishwa mwaka 2015.
Na Sylvester Raphael 

Next Post Previous Post
Bukobawadau