Bukobawadau

JK KUKATAA KUITUA MIZIGO ANAMKOMOA NANI?

Na Prudence Karugendo
BINADAMU  tumeumbwa na hulka tofautitofauti, katika hulka hizo kuna watu wameumbwa na hulka za unafiki na wengine si wanafiki.
Pamoja na kwamba watu hatupaswi kujisifia lakini naamini kabisa kwamba mimi sikuumbwa na unafiki, na ninauchukia sana unafiki.
Hakuna kitu kibaya na cha hatari duniani kama unafiki. Nadhani ndiyo maana Wahaya wakabuni usemi kwamba ni heri ukawa na jirani jambazi kuliko kuwa jirani na mnafiki. Wahaya wanaamini kwamba jambazi unaweza ukamkabili kwa kujiimarishia ulinzi kitu ambacho hakiwezekani kwa mnafiki.
Mnafiki ataingia mpaka chumbani kwako akijidai ni rafiki na mtu mwema kwako anayekutakia mema kumbe mambo ni kinyume chake! Atachukua siri zako zote bila wewe kushtuka  aende kuzifanyia maovu yenye mpango wa kukuangamiza! Mnafiki ni mtu mchafu sana .
Kwahiyo kutokana na kuuchukia unafiki nakuwa muwazi kwamba naipenda sana nchi yangu, na hivyo kuuombea uongozi wake uliopo Mungu aujaze hekima za kuiongoza vyema nchi yetu. Pia nampenda rais wangu na kumtakia kila la kheri nikielewa kuwa kazi aliyo nayo ni mzigo mkubwa unaohitaji msaada wa kila mwananchi ili aweze kuubeba salama bila kuchoka katika kipindi chote anachokuwa madarakani kwa mujibu wa kanuni za nchi yetu.
Lakini pamoja na kumtakia mema rais wangu, hasa katika kumpunguzia uzito wa mzigo alioubeba, inaonekana kuna watu walio karibu zaidi na yeye wanaomweleza kwamba kwa nyenzo alizopewa hapaswi kuujali uzito wa aina yoyote katika mzigo ulio kichwani kwake!
Watu hao ni wanafiki wanaojifanya kumpenda sana , lakini kiukweli ni kwamba hawamtakii mema yeye binafsi, nchi yake pamoja na watu anaowaongoza. Wao wanaangalia tu nafsi zao zimekaa katika nafasi gani, na zitaendelea kukaaje ndani ya mzigo ulio kichwani kwa rais. Hawaujali uzito wake hata kidogo, ila nafasi zao tu basi.
Kama nilivyosema, kutokana na kuipenda nchi yangu nampenda  vilevile rais wangu bila unafiki wowote. Akishakuwa rais siangalii katoka chama gani cha siasa, isipokuwa kumtakia kila la kheri ili aweze kuwa na hekima za kuongoza vizuri kwa mustakabali mwema wa nchi yetu.
Kwa sasa tunaye kiongozi wetu mkuu ambaye ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete, aliyetokana na Chama Cha Mapinduzi, chama tawala. Kwa vile chama hicho ndicho kinachotawala tulitegemea kwamba kingempa rais msaada wa kila aina kusudi kada wake huyo kileyemuamini na kumnadi kwa wananchi ili akabidhiwe mzigo wa kuiongoza nchi asiweze kuuona uzito katika mzigo huo.
Lakini badala yake, rais aliye pia mwenyekiti wa chama hicho, wakati fulani akatoa kauli iliyoonekana kukisuta chama chake. Akasema chama kinapaswa kujivua gamba! Sidhani kama angeona kwamba chama chake kina msaada kwake akatamani kijivue gamba. Bilashaka kauli hiyo ilitokana na kuuona uzito wa mzigo alioubeba unazidi kumkandamiza yeye peke yake pasipo kuuona msaada wa chama chake.
Hatahivyo gamba aliloliona mwenyekiti lilishindikana kuvuliwa huku baadhi ya makada wakibeza kwa jeuri kwamba gamba limekwamia kiunoni na wenye uwezo wa kulitoa ni lazima watafute mashoka!
Lakini pamoja na hiyo yalifanyika mabadiliko katika chama hicho yaliyomleta mtendaji mkuu mpya, Katibu Mkuu,  Abdulrhaman Kinana, huku katibu mwenezi akibaki ni yuleyule Nape Nnauye.
Kusema ukweli mimi ni mmoja wa wasiokubaliana na sera za chama tawala, hasa baada ya chama hicho kukiuka misingi yake kwa kiasi kikubwa. Lakini pamoja na hilo nimewakubali kabisa watu wawili katika chama hicho tawala kwamba ni majembe ya uhakika. Hao ni wanasiasa kwa maana halisi. Watu hao ni Katibu Mkuu, Abdulrhaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Kilichonifanya niwakubali watu hao wawili ndani ya CCM ni hatua yao waliyoichukua ya kujitenga na wanafiki. Wameamua kufanya kazi yao kwa maana halisi ya chama tawala wakiwa wamelenga kumpunguzia rais uzito katika mzigo alioubeba.
Ni kwamba viongozi hao wa juu wa chama tawala wamezifanyia tathmini kero zote za wananchi na kugundua matatizo yalikolalia. Wakaona ndani ya kinachoitwa usaidizi wa rais ndimo kuna uzito zaidi. Hivyo wakaamua kutaja hadharani kuwa fulani na fulani ndio wanaosababisha kero hizo na kumzidishia rais uzito kwenye mzigo alioubeba. Na kwa vile mzigo huo ni wa rais na chama tawala, viongozi hao wa chama wakapendekeza kwa rais kuwa mizigo isiyo na chochote ndani yake ni bora ibwagwe chini.
Ni wazi kwamba kama rais angesikiliza ushauri huo na kuamua kuibwaga chini mizigo inayoleta usumbufu mambo mawili yangetokea kwa wakati mmoja. Moja ni kwamba chama tawala kingepata umaarufu na ushawishi zaidi, na pili yeye rais angeiona kazi hiyo nzito, uongozi wa nchi, kuwa ni nyepesi akiwa amejinufaisha na faida ya kuwa na chama tawala nyuma yake.
Lakini bahati mbaya sivyo ilivyokuwa. Badala yake rais kaamua kuubwaga chini ushauri wa chama chake na kubaki na mizigo yake kichwani! Hapo ndipo ninapojiuliza, kwa kufanya hivyo rais kamkomoa nani? Kaukomoa upinzani, kakikomoa chama chake au kajikomoa yeye mwenyewe?
Zipo tetesi kuwa rais kaamua kubaki na mizigo yake kichwani ili isije ikaonekana kaitua mizigo kwa kushurutishwa na walio chini yake kimaamuzi. Najiuliza tena, ni lipi ni rahisi kwake, kuonekana ameibwaga chini mizigo isiyo na faida yoyote na inayoleta kero kwake na kwa wananchi kwa kushurutishwa na walio chini yake kimaamuzi au kuendelea kubaki nayo kichwani na kuonekana ameshurutishwa na mizigo yenyewe kufanya hivyo?
Sababu inaonekana walio kwenye mzigo wa rais  wanapenda waendelee kula uhondo wakiwa wamebakizwa kwenye mzigo unaomsumbua rais kwa uzito wake hata kama kubaki uko hakuna faida yoyote kwa rais, aliyebeba mzigo, kwa wananchi wala kwa nchi zaidi ya kumsababishia rais wetu uchovu usio na mpangilio!
Kama watu hao, wanaoitwa mizigo,  wangekuwa na mapenzi ya dhati kwa rais wao wasingesubiri kupigiwa kelele, wangechukua uamuzi kama aliochukua aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki , wa kujiondoa wenyewe kwenye furushi lililo kichwani mwa rais.
Lakini kitendo cha watu hao, mizigo, kukaa kimya huku rais akipigiwa kelele za kumnusuru na wanaomjali wakimuonea uchungu kwa mizigo aliyoibeba, sioni kama kinaweza kuwafanya watu hao waonekane wana mapenzi na yeye hata kama yeye mwenyewe atakuwa anaichukulia hivyo.
Tatizo kubwa ninaloliona katika jamii yetu ni mazoea. Tunafika mahali mazoea tunayachukulia kama sheria pasipo kujali kama mazoea hayo yanatuathiri au la! Hapo ndipo rais naye anapoiangalia jamii yake jinsi ilivyozama kwenye mazoea ikamwia vigumu kuchukua maamuzi ambayo pengine anaona yanaweza yakakinzana na mazoea ya jamii yake na hivyo yeye kuonekana ni wa ajabu!  
Sababu mpaka sasa wapo watu wanaomsema Rais Kikwete kwa mshangao kwamba kwa kipindi cha chini ya miaka 10 kawa na maziri wakuu wawili. Watu hao wanasemea mazoea waliyoyapata kwa rais wa awamu ya tatu, Mkapa, aliyekaa na waziri mkuu mmoja tu, Sumaye, kwa kipindi chake chote cha miaka kumi bila kueleza hilo lilikuwa na tija gani kwa nchi.
Wanaosema hivyo hawataki kuangalia nyuma na kuona jinsi mambo yalivyokuwa hasa katika awamu ya kwanza. Mwalimu Nyerere alifanya mabadiliko mara tano katika nafasi ya waziri mkuu katika kipindi cha miaka 10 kati ya mwaka 1975 – 1985.
Alimbadilisha Mzee Kawawa na kumuweka Marehemu Sokoine, baadaye akaja Mzee Msuya na baadaye Sokoine tena, kisha Dk. Salimu.
Sasa wanaomshangaa Kikwete kwa kufanya mabadiliko mara moja katika nafasi hiyo kwa kipindi cha karibu miaka 10 wameyasahau hayo, hawayajui au wanashangaa kitu gani?
Hapa inabidi tuyaelewe mambo mawili, kwamba mazoea hudumaza na mabadiliko ni chachu ya maendeleo. Kisichobadilika kawaida hudumaa.
Nimalizie kwa kutoa mifano ya nchi mbili ambazo zinayapenda sana mabadiliko,  na tuziangalie jinsi zilivyo kimaendeleo. Nchi hizo ni India na Japan.
India ni nchi isiyojali mtu kakaa kwa kipindi gani madarakani ila kafanya nini akiwa pale. Iliwahi kuwa na waziri mkuu aliyeitwa Gulzarilal, alikaa madarakani kwa siku 26 tu, Charon Singh kwa siku 170, Chandra alikaa kwa siku 223, H. D. Deve Gowda alikaa kwa siku 324 na I. K. Gigral alikaa madarakani kwa siku 332. Katika hao hakuna aliyefikisha hata muda wa mwaka mmoja kwenye madaraka!
Japan nako mambo yako vilevile. Sanjo Sanetomi alikaa madarakani kwa siku 60 tu, Higashikuni Naruhiko alikaa kwa siku 53, Katsura Taro siku 61, Tsutomu Hata siku 63. Ni mawaziri wakuu wengi katika nchi hiyo ambao hawakufikisha hata mwaka madarakani.
Pamoja na nchi hizo kuwa na mabadiliko ya mara kwa mara katika serikali zake ni kipi tunachoweza kusema kuwa walau tunazikaribia kimaendeleo sisi tunaoyaogopa mabailiko?
Mwisho kabisa ni kwamba wanafiki ni watu wachafu sana . Hawa waliwahi kumtembeza mfalme akiwa uchi wakidai amevaa nguo isiyoonekana, kwamba wenye dhambi tu ndio waliomuona mfalme kuwa yuko uchi. Wanafiki hao walifanya hivyo kutimiza matakwa ya mfalme, ambaye kwa ulevi wa madaraka alitaka ashonewe nguo isiyoonekana!
Kinana na Nape wamejitenga na wanafiki, wametamka wazi kuwa Rais Kikwete kabeba mizigo  isiyo na maana, wakamshauri aibwage chini ili mambo yamuendee salama. Inavyoonekana Kikwete kawapuuza, bilashaka baada ya kuwasikiliza wanafiki.
Nafasi za Kinana na Nape ni kubwa na nzito katika uendeshaji wa chama tawala, kupuuzwa kwao ni kuzito vilevile, kunawafanya nao waonekane ni mizigo. Kwahiyo ili wasionekane ni mizigo wangefanya kama alivyofanya Mzee Edwin Mtei, wakati wa serikali ya awamu ya kwanza,  pale alipokwenda na mgeni toka Benki Kuu ya Dunia nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Msasani,  Nyerere akawaacha sebuleni na kwenda zake nje kupunga upepo na kusoma kitabu.
Akufukuzaye hakwambii toka. Alichokifanya Mzee Mtei ni kwenda ofisini kuandika barua ya kujiuzulu. Kinana na Nape mnasubiri nini? Lindeni heshima yenu.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau