MOTO WAMWAKIA MAMA ANNA TIBAIJUKA
Dar es Salaam/Mbeya. Viongozi wa vyama vya
siasa na wanaharakati wa masuala ya ardhi, wamesema kuzomewa kwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ni
matokeo ya makosa yanayowafanywa na Serikali kuwapendelea wawekezaji wa
nje na kuwapuuza wananchi.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Profesa
Tibaijuka kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo cha kumruhusu
mwekezaji kuendelea kumiliki shamba la Kapunga, wilayani Mbarali, mkoani
Mbeya lenye ukubwa wa hekta 7,370.
Wananchi hao walikasirishwa na kitendo cha Profesa
Tibaijuka kubadili msimamo wake awali wa kumpokonya ardhi mwekezaji
huyo kwani mara ya kwanza alishawaeleza viongozi wa vijiji kuwa serikali
itawarudishia eneo lao.
Mwekezaji huyo alitakiwa kumiliki ekari 5,500
lakini serikali ilimmilikisha ekari nyingine 1,870 ambazo ni mashamba ya
wanakijiji.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Ardhi, Yefuz Myenzi
alisema hayo ni makosa ya serikali kuwapa ardhi wawekezaji wa nje bila
kutenga ardhi ya wanavijiji.
“Serikali inabinafsisha hadi vijiji ambako
wananchi wangeweza kulima na kuendesha maisha yao, unategemea nini
wakimwona kiongozi wa serikali ni lazima watamzomea,” alisema Mnyezi.
Alisema ubinafsishaji wa ardhi unafanywa na ngazi
za juu za taifa bila kuushirikisha uongozi wa ngazi za vijiji hali
inayosababisha vurugu katika maeneo mengine.
“SiYo katika Shamba la Kapunga tu, kuna maeneo
mengi ambako wawekezaji wa kigeni wamepewa ardhi lakini wao wanaikodisha
kwa wananchi kitendo ambacho ni kosa,” alisema.
Myenzi alisema katika maeneo yenye matatizo kama
hayo, Rais anatakiwa kutumia madaraka yake kwa kubadilisha matumizi ya
ardhi ili wananchi waweze kupewa kwa ajili ya kilimo.
Viongozi wengine
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro
alisema viongozi wa Serikali wanawapendelea wawekezaji wa nje na
kuwapuuza wanavijiji.
“Migogoro hii ya ardhi inavyochukiza watu kama
kiongozi utakwenda kusuluhisha na kutoa majibu yasiyowaridhisha
wananchi, basi viongozi wataendelea kuzomewa kama Waziri huyo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema wananchi wanakatishwa tamaa na viongozi wa serikali kuwapendelea wawekezaji.
“Ajira pekee inayotegemewa vijijini ni kilimo,
serikali inabinafsisha hadi mashamba ya wanavijiji, wamekata tamaa ndiyo
maana wanazomea ovyo. Viongozi hawana nia ya dhati kutatua migogoro
iliyopo,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa NCCR
-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema ili kuondokana na migogoro, wawekezaji
wanatakiwa kuwa na vibali vya ardhi kutoka katika uongozi wa kijiji.
“Wanakijiji ndiyo wenye ardhi, migogoro ya namna hii isingetokea kama wangeshiriki kutoa vibali kwa wawekezaji,” alisema.
DC amtetea Tibaijuka
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kifu
amesema pamoja na kwamba wananchi wa kijiji cha Kapunga wanataka mgogoro
huo umalizike haraka, lakini anaamini uamuzi wa Profesa Tibaijuka
kufanya mazungumzo na mwekezaji wanayevutana naye utaleta ufumbuzi wa
tatizo hilo.
Profesa Tibaijuka alisema majuzi kuwa Kampuni ya
Kapunga Rice Project inamiliki kihalali mashamba kwenye eneo hilo na
kudai kuwa serikali ndiyo yenye makosa kwenye mgogoro huo.
Mashamba hayo mara ya kwanza yalikuwa yanamilikiwa
na Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco) lakini yalibinafsishwa na
kuchukulikuwa na mwekezaji huyo.
Kifu alisema pamoja na kwamba wananchi wengine
hawakuridhika na uamuzi wa Waziri lakini anaamini kuwa Profesa Tibaijuka
ndiyo yuko sahihi kuzungumza na wawekezaji ili waliachie eneo hilo
kwani hawana makosa.
VIA MWANANCHI
VIA MWANANCHI