NI KWELI NYERERE KAFA KWA HUZUNI
Na Prudence Karugendo
WIKI mbili
zilizopita niliandika makala iliyobeba kichwa cha habari cha “Mandela katuachia
fundisho, tutalitekeleza?” Katika makala hiyo nilijaribu kuyaangalia maisha ya
Mandela, hasa baada ya kuanza harakati zake za kuutokomeza ukaburu, akiwa uraiani, jela na baadaye uraiani tena,
na kupata mtazamo kwamba maisha hayo ya Mandela yalikuwa ni fundisho kwa
wanadamu wote wapendao haki, hususan Waafrika wenzake.
Lengo la
makala hiyo lilikuwa kwamba haitoshi kumpongeza Madiba kwa hotuba nzuri tu kwa
kuyatazama aliyoyafanya katika uhai wake na kisha kuyapiga kisogo. Kwa maana
halisi ya kuyapongeza aliyoyaishi ni vena nasi tukajaribu kuyaishi yale yote
aliyoyaamini.
Lakini
ninachojiuliza mpaka leo ni kwamba tutaiweza hiyo changamoto aliyotuachia
Madiba? Tutaweza kuishi kama alivyoishi yeye akiwa ameuweka umimi pembeni na
kuitanguliza haki ya kila mmoja ambayo yeye aliiona ni bora kuliko hata uhai wake? Kumbuka mara kwa mara
alikuwa akitamka kwamba yeye anapigania haki ya wote, bila kujali rangi, kabila
wala jinsia, muda wote akisisitiza kwamba ikibidi ni bora afe kwa hilo.
Mandela
aliyoyapigania yote kayashuhudia yakitimia akiwa bado hai. Ukaburu ukatokomea,
mfungwa maarufu duniani akatoka jela na kuwa rais wa kwanza mweusi nchini
kwake, akakaa kipindi kimoja madarakani na kuwaachia wengine watawale. Umimi
akiwa ameupiga kumbo.
Kwa upande
wake, kweli Mandela kayatimiza yote aliyoyapigania, ndiyo maana nasema kwamba
sidhani kama kuna mtu aliyepata kufa kwa furaha kama alivyokufa mzee wetu huyo.
Sababu mambo yote aliyokuwa akisema kwamba yuko tayari kuutoa uhai wake ili
yaweze kutimia yametimia bila uhaI wake kutoka! Ushindi ulioje?
Makala hiyo
ilipotoka msomaji mmoja akanitumia ujumbe mfupi wa maandishi akiniuliza kwamba
iwapo nasema kwamba Mandela kafa kwa furaha kwani Nyerere alikufa kwa huzuni?
Pamoja na
kwamba halikuwa lengo langu kuilinganisha hiyo misiba miwili, hatahivyo nadhani
hilo ni jambo lisilohitaji mjadala kwa
wale wenye uwezo wa kuchanganua mambo.
Kwa ufupi ni
kwamba ingetokea yale yote aliyoyapigania Mandela yakaanza kubadilika akiwa
hai, watu wakaanza kubaguana tena kwa misingi ya rangi na ukabila, haki za
wadogo zikaanza tena kumezwa na mapapa nakadhalika, bilashaka tungekuwa tunaongea mambo mengine juu ya
Mandela kwa wakati huu. Hata mimi nisingeweza kusema Mandela kafa kwa furaha.
Tukiviangalia
hivi vifo viwili, kifo cha Nyerere na kifo cha Mandela, tutayaona mambo mawili
yasiyofanana hata kidogo. Kifo cha Nyerere ulikuwa ni musiba mzito, majonzi
kila mahala hasa hapa nchini mwetu. Lakini kifo cha Mandela lilikuwa ni
tamasha, watu wakiimba na kucheza kwa furaha, furaha ya kumuaga shujaa.
Mantiki ni
kwamba mtu aliyefanikisha malengo yake ni shujaa. Mfano katika kabila la Wahaya
akifa babu au bibi, mzee aliye na wajukuu, haisemwi kwamba kafa ila wanasema
“yataya”. Sina tafsiri sahihi ya neno hilo kwa Kiswahili ila lina maana ya
kutimiza ada ya maumbile, kwamba kizaliwacho ni lazima kife.
Kwahiyo
kinachofuatia kwa Wahaya baada ya babu au bibi kufariki ni sherehe
inayoendeshwa na wajukuu wa marehemu, wao wanaita “okusiribya”. Maana ya
“kusiribya” ni kutania, sababu mjukuu ni mtani wa bibi au babu.
Kwahiyo
wajukuu wanachukulia kwamba babu au bibi kayatimiza yote aliyotumwa na Mwenyezi
Mungu. Kaoa au kuolewa, kazaa watoto nao wamezaa wengine, kipi tena ambacho
bibi au babu angekifanya zaidi? Hivyo inachukuliwa kwamba kumlilia mtu wa aina
hiyo ni sawa na kumkufuru Mungu.
Hivyo
wajukuu wanafanya sherehe ya kumshukuru Mungu ikiwa ni pamoja na kuwaliwaza wazazi
wao ili wasihuzunike sana kwa musiba wa mzazi wao ambaye kayatimiza yote yaliyomleta
duniani.
Hiyo ni
tofauti na anapokufa kijana. Kijana analiliwa na kila mtu, pengine kutokana na
ukweli wa kwamba anakuwa bado anayo mengi aliyotakiwa kuyatekeleza. Kwahiyo kwa
kijana Wahaya wanatumia usemi wa kwamba “omwana yagutuka” wenye maana ya kijana
kakatika, sawa na kusema kijana kakatisha maisha yake.
Lengo la
makala hii ni kujibu swali la msomaji aliyeniuliza kuwa kama nasema kwamba
Mandela kafa kwa furahaa ina maana Nyerere kafa kwa huzuni?
Kitendo cha
Nyerere kuliliwa na kila mtu kilikuwa na maana kubwa, hata kama waliolia si
wote waliokuwa na uwezo wa kutambua kwa nini walilia. Maana yake ni kwamba
waliolia walikuwa bado wanamhitaji Mwalimu, bila ya wote kuelewa kinagaubaga
maana ya majonzi yao, ukweli unabaki palepale kwamba kazi ya Mwalimu ilikuwa
bado haijatimia, au ilitimia baadaye ikapindishwa au kurudishwa nyuma!
Kwa mantiki
hiyo, ndiyo maana nasisitiza katika makala hii kwamba Nyerere alikufa kwa huzuni
tofauti na rafiki yake, Mandela, aliyekufa kwa furaha kubwa. Kwa nini nakuwa na
mtazamo huo?
Tangu kabla
Nyerere hajafa alianza kuonyesha namna alivyosikitishwa na mabadiliko
yaliyokuwa yakijitokeza yakiyaondoa karibu mambo yote aliyoyatengeneza yeye na
mambo hayo kuipa nchi yetu heshima ya pekee duniani kote.
Mwanzoni
Nyerere alilalamikia kitendo cha wafanyabiashara, wengi wao wakiwa ni vijana,
kuizoea Ikulu kiasi cha baadhi yao kufikia kumuita mke wa rais shemeji ilhali
akiwa ni Mama wa Taifa! Katika hilo heshima ilikuwa imeporomoka wala siyo
kupungua!
Baadaye
Nyerere akalalamikia kitendo cha wabunge kujitenga na wapiga kura wao na kutaka
wao waitwe waheshimiwa badala ya kuwa ndugu. Neno ndugu lilitutambulisha
duniani kote, heshima ya pekee, lakini wabunge wetu wakalikataa wakidai kwamba
wanapochaguliwa wanakuwa viumbe tofauti, siyo ndugu tena!
Baadaye
Azimio la Arusha likapigwa teke! Nyerere akalalamika sana na kusema kwamba yeye
hakuona kosa lolote la Azimio la Arusha, akaongeza kuwa lile lilikuwa ni azimio
la utu. Akasema mfukoni mwake alikuwa anatembea na vitabu viwili, Biblia,
kitabu cha Mungu, na kile cha Azimio la
Arusha.
Vilevile
Nyerere akawa anashangaa na kasi ya wananchi kuanza kutambuana kwa makabila yao.
Akatoa mfano jinsi alivyokwenda New York na kukaribishwa chakula na Mama
Mongella, kule kwenye chakula akakutana na mama mmoja wa Kiganda aliyemweleza
kuwa katika nchi nyingi za Kiafrika watu hutambuana kwa makabila yao lakini si
katika Tanzania. Nyerere akamwambia mama huyo “mama hayo ni ya zamani siku hizi
Watanzania wanatambuana mpaka kwenye vijiji wanakotoka!”.
Baada ya
hapo ukaja ubinafsishaji wa mali za umma hasa zile zilizotaifishwa kufuatia
Azimio la Arusha. Nyerere akasema kwamba mtabinafsisha mpaka Magereza!
Ndipo
baadaye likaja suala la Muungano, Nyerere akasema iwapo Watanzania mtaingiwa na
dhambi ya ubaguzi ya kusema wao Wazanzibari sisi Watanganyika, au sisi
Wazanzibari wao Watanganyika, dhambi hiyo itawatafuna. Mpaka Mwalimu akatoa
laana kwamba dhambi hiyo inabidi iwatafune ikiwa mtaiendekeza!
Na
yawezekana laana hiyo ya Mwalimu imeanza kufanya kazi, sababu majuzi mjini
Kigoma tulishuhudia kitu ambacho hatukukizoea. Watu walitayarishwa na kufanya
maandamano wakiwa na mabango yenye maneno “Wachagga waende zao watuachie Kigoma
yetu”! Ni lazima mambo hayo yanaandaliwa na kulindwa na watu waliofilisika
kisiasa wakitafuta pa kujishikiza ili kupata uhalali wa kisiasa.
Zipo sababu
mbalimbali zilizochangia kuihuzunisha roho ya Baba wa Taifa. Mbali na zile
zilizokuwa katika uwezo wake wa kuzikemea, ipo moja kubwa iliyokuwa nje ya
uwezo wake, nayo ni ya kufilisika kisiasa. Mwalimu aliwahi kusema kwamba mtu
akifilisika kisiasa ni lazima atafute mahali pa kujishikiza kujenga uhalali wa
kuendelea kuitwa mwanasiasa. Akasema mtu wa aina hiyo atatafuta ukabila, ukanda
au udini. Hayo ndiyo tuliyoyashuhudia Kigoma!
Kisha
akasema kwamba enzi zile za maadili mtu aliyeutamani uongozi wa umma alikuwa
anaangaliwa ana mali kiasi gani, maana alisema kuwa mali ilikuwa
“disqualification” ya kuupata uongozi, akasema kwamba kwa sasa mali diyo
“qualification!” ya kwanza katika kuutafuta uongozi!
Vilevile
Mwalimu alikuwa akisisitiza kwamba Ikulu ni sehemu takatifu, akisema kwamba
pale hapauzwi nyanya, kwa maana ya kutofanywa biashara yoyote katika eneo lile.
Lakini ajabu mtu ambaye Mwalimu alimpigania kumwingiza Ikulu akiwa na imani
kwamba angeweza kuyalinda maadili hayo, bila aibu wala haya, mtu huyo akaja
kusajili kampuni ya biashara akijitambulisha kama mjasiriamali anayeishi Ikulu!
Hayo na
mengine ndiyo yanayonifanya niamini kwamba Nyerere alikufa kwa huzuni mkubwa,
kwa hayo hawezi kufanana na Mandela hata kidogo.
0784 989 512