Bukobawadau

UTANDAWAZI UNAVYOZISAMBARATISHA JUHUDI ZETU ZA KUPATA MAENDELEO

Na Prudence Karugendo
Ipo dhana ya kwamba kutawaliwa kulichangia maendeleo ya Bara la Afrika, ikiwemo nchi yetu ya Tanzania. Vilevile wapo wanaodhani kwamba mawazo ya kupenda kutawala, yaani sehemu moja kuinyang’anya sehemu nyingine uwezo na haki ya kujiamulia mambo yake kadiri ya utashi wake, hasa mawazo ya mataifa makubwa dhidi ya mataifa madogo, kwa wakati huu yamepitwa na wakati ndani ya ustaarabu wa dunia ya sasa.
Mawazo ya aina hiyo yote sikubaliani nayo, mtu kumtawala mwenzake ni dhambi ambayo, kama alivyosema Baba wa Taifa, ni sawa na binadamu kula nyama ya binadamu mwenzake. Anayeionja dhambi hiyo ya kishetani hawezi kuiacha kamwe, ataendelea nayo hata kama ni kwa njia tofauti tofauti.
Kwahiyo waliotutawala kamwe hawawezi kudai kwamba sasa hivi ni wastaarabu, kwamba hawawezi kuirudia tena dhambi hiyo ya kutamani kuwatawala wenzao.
Ushahidi ni mkubwa unaoonyesha jinsi mataifa makubwa yalivyo na hamu ya kuendelea kuyatawala mataifa madogo kupitia katika mbinu zinazobuniwa usiku na mchana, mbinu mojawapo ikiwa ni hii inayotumika kwa sasa ya utandawazi. Ingawa wapo wanaosema kwamba utandawazi haujaanza leo, wakiwa na hoja kwamba utandawazi ulianza rasmi baada ya Kikao cha Berlin (Berlin Conference), katika karne ya 19, utandawazi wa sasa kidogo ni tofauti na utandawazi ulioanzishwa wakati huo.
Utandawazi wa wakati huo ulikutana na vigingi, hasa kutoka kwa watawala wa asili wakiwa wanaungwa mkono na watu wao, baada ya kuishtukia hila iliyokuwa imebuniwa kufanikisha utandawazi huo katika maafikiano ya Berlin.
Utandawazi ule ulijaribu kutumia mbinu za hadaa, ziliposhindikana yakatumika mabavu. Watu kwa maelfu na baadhi ya wafalme waliuawa katika kushinikizwa waukubali utandawazi huo.
Tofauti na utandawazi wa mwanzo, utandawazi wa sasa hautumii mabavu, huu umewekewa tamutamu kiasi cha viongozi wetu, kwa hiari yao, kukubali kushirikishwa kwenye utapeli huo.
Mathalan, tumemshuhudia mmoja wa marais wetu akifanywa mwenyekiti mwenza wa utandawazi huku yeye akiwa amejawa majivuno yenye kuonyesha jinsi dunia inavyomthamini kwa kupewa nafasi hiyo! Mtu anajivunia kitendo cha kukubali kula sumu yeye mwenyewe bila kulazimishwa! Huo ni ujasiri wa aina yake katika utandawazi wa sasa!
Utandawazi umejikita katika kila sekta za uendeshaji wa maisha yetu. Hii maana yake ni kwamba tunatawaliwa tukiwa tunakushangilia kutawaliwa huko. Tunatawaliwa kwa hiari yetu!
Sekta mojawapo iliyoingiliwa na utandawazi na kudhoofishwa mithili ya mwili wa binadamu unavyodhoofishwa na ugonjwa wa ukimwi, ni sekta ya michezo, hasa mpira wa miguu. Hicho ndicho kitu kinachonifanya nianze kuulaani utandawazi huu wa sasa, na ndilo lengo langu la makala haya.
Kwa sasa utandawazi unawawezesha Watanzania, hususan vijana, kuangalia mechi za kandanda moja kwa moja kutoka katika viwanja vya Ulaya. Huo ni utandawazi, na kuna wanaodai kwamba hayo ni maendeleo. Lakini matokeo ya maendeleo hayo ni kuua moyo wa vijana wa hapa kwetu wa kutafuta maendeleo yao. Moyo wa vijana wa kuipenda kandanda ya nchini kwao unatoweka, ushabiki wa kandanda , kwa vijana wengi wa Kitanzania, umehamishiwa katika vilabu vya Ulaya huku nyuma kandanda la Tanzania likidoda na kudumaa.
Moyo wa uzalendo uliokuwa unawasukuma wapenda kandanda nchini kuzishabikia timu zao za nyumbani, mathalan Yanga na Simba, kwa sasa umepeperushwa na upepo wa utandawazi. Tunaona jinsi wapenda kandanda hapa nchini walivyojigawanya katika vilabu mbalimbali vya Ulaya, hasa vile vya Ligi Kuu ya Wingereza.
Kuna hoja za kijinga zinazotolewa na wanautandawazi hao wanapojaribu kuufunika ulimbukeni wao. Wanadai eti wanafuata kizuri, mpira wa kwao ni wa hovyo, hivyo wanafuata mpira mzuri! Hawajiulizi uzuri unapatikanaje. Hoja zao haziwaelekezi kuelewa kwamba kila kizuri hutengenezwa.
Wasipokitengeneza wao sijui wanamtegemea nani awatengenezee uzuri huo wanaoutaka wao na kuamua kuufuata ughaibuni kupitia kwenye utandawazi.
Kabla ya utandawazi huu uliotujia kwa njia sawa na iliyotumiwa na ugonjwa wa ukimwi, kiwango chetu cha kandanda kilikuwa kinaeleweka. Tanzania ilikuwa katika ramani ya dunia ya kandanda. Katika miaka ya 1970, kwa mfano, lilikuwa jambo la kawaida kwa timu za daraja la kwanza barani Ulaya kuja kucheza michezo ya kirafiki nchini kwetu na wakati mwingine zikifungwa. Najua hilo litaonekana kama muujiza kwa wanautandawazi wa sasa.
Utandawazi unatufanya kwa sasa tuuabudu mpira wa Ulaya kiasi cha kuyaona kama maajabu kwa timu za Ulaya, hata ziwe zile za “chandimu”, kuja kucheza huku kwetu! Zamani timu kubwa za Ulaya zilikuwa zikija tukiyaona ni mambo ya kawaida, lakini kwa sasa imegeuka miujiza. Ndipo tujiulize utandawazi kwetu unaongeza unapunguza?
Wakati fulani tuliichukulia kauli ya Rais Kikwete ya kutaka kuileta nchini klabu mojawapo ya Hispania, ambayo tena kwa kiwango “ilishafulia”, kama kauli ya kutuonyesha milango ya ahera. Wakati kusema ukweli hayo ni mambo yaliyokuwa yamezoeleka kabla ya ujio wa saratani hii ya utandawazi.
Wakati ule wachezaji wetu walikuwa wanajituma ili wawe na uwezo wa kukabiliana na wachezaji nyota wa Ulaya na Brazil, hawakuwa wakicheza ili waitwe majina ya wachezaji hao nyota kama ilivyo sasa. Nasikia wachezaji wa nyumban kwa sasa wakiitwa Canavarro, Adebayor, Drogba nakadhalika, kitu ambacho kusema ukweli kinanitia kichefuchefu.

Enzi za Edson Arantes Do Nascimento (Pele), sikusikia mchezaji yeyote hapa nchini kwetu akijiita Pele. Tulikuwa nao kina Sunday Manara, Gibson Sembuli, Abdallah Kibaden, Haidar Abeid na wengine wengi. Wao walikuwa wakiamini kwamba Pele ni bindamu kama wao waliyehitaji kumkabili kivitendo, na wala siyo kumtukuza kwa kugeza jina lake tu.

Kinachofanyika hapa ni kuua upinzani wa kisoka, kama ilivyo kwa mambo mengine yote, ambayo mataifa makubwa yanataka yabaki vinara bila upinzani hasa kutoka kwa mataifa madogo. Haiwezekani, kupitia katika ulimbukeni huu, pakatokea klabu yoyote katika Afrika, achilia mbali Tanzania, ikaleta upinzani kwa vilabu vya Ulaya. Wapenzi wa kandanda wa upande huu wameharibikiwa kisaikolojia, timu za kwao hawazioni, ila tu za Ulaya!
Wachezaji wazuri wanaozalishwa katika Afrika wote wako katika utumwa wa kujitakia wakifanyishwa mitulinga katika kile kinachoitwa uchezaji wa kulipwa.
Hebu tujiulize, tunawezaje kuinua kiwango chetu cha kandanda katika hali kama hiyo? Akili zetu zote zimezama katika kandanda la wenzetu, tunayashangilia maendeleo ya wenzetu huku tukiyakwamisha ya kwetu, kisa utandawazi!
Utandawazi umewapumbaza watu kiasi cha wengine kujiona ni wakazi wa Manchester, wengine Liverpool na wengine kuwa wakazi wa vitongiji vya London. Bila ya kuelewa wanachokifanya utasikia watu wanasema “tutakuwa nyumbani kwetu Old Traford” wengine Liverpool au tutakuwa kwetu Darajani, wapenzi wa Chelsea hao, nakadhalika.
Utumwa wa kutupakia kwenye majahazi na kutupeleka ughaibuni umepita, umekuja utumwa wa utandawazi. Tunafanywa watumwa hapahapa kwetu tulipo. Si ilisemwa kwamba mkataa kwao ni mtumwa? Mtu ukiacha kushabikia Simba na Yanga na badala yake ukawa shabiki wa Manchester, Arsenal au Chelsea utakuwa umeukwepa vipi utumwa?
Watu wazima wanapoteza muda kwa kuweka magenge, hata wakiwa maofisini, kuongelea Ligi Kuu ya Wingereza! Mtu anaona ufahari kutaja majina ya wachezaji wote wa timu ya Manchester United wakati akidai hayajui majina ya wachezaji wa Yanga wala Simba! Huu sasa si ulimbukeni bali upambavu. Hiyo ni kwa sababu sidhani kama unaweza kukutana na kitu kama hicho ndani ya Wingereza ambako watu wanaacha kazi na kuanza kutaja majina ya wachezaji wa vilabu wanavyovishabikia, pamoja na kuwa vya nyumbani kwao.
Vyombo vyetu vya habari navyo vimekumbwa na utandawazi, asilimia 90 habari za michezo vinaongelea ligi na michezo mingine ya Ulaya. Huu sio utandawazi ila unaelekea kuwa uchawi. Kama ni utandawazi kwa nini BBC au CNN navyo visionyeshe Ligi Kuu ya Tanzania? Au utandawazi unajitokeza tu kutoka kwa mkubwa kwenda kwa mdogo? Huu utandawazi utamsaidiaje mnyonge iwapo unamfanya mnyonge abaki kumtukuza mwenye nguvu bila mwenye nguvu kumjali mnyonge?

Ni dhahiri sasa kwamba utandawazi ni ukoloni mkongwe ambao, unatumia nguvu za kiuchumi kutuua, sio kututawala kama zamani, kiuchumi na kiakili. Hivyo kutokana na unyonge wetu hatunabudi kutumia ushirikiano wa “kimchwa”, kufanya kazi kama mchwa, kupambana na utandawazi huu ili tuutokomeze kama kweli tunauthamini utu wetu.
Ona sasa watu wanashangilia na kukimbiza kifimbo cha malkia! Kwa maana kwamba tunaendelea kumtukuza malkia wa Wingereza! Sijui huo uhuru tulioupata ulikuwa na maana gani! Kifimbo cha malkia kina maana gani nchini kwetu? Mbona hatukimbizi kifimbo cha Baba wa Taifa kilichokuwa kipenzi kwake naye akiwa kipenzi chetu?
Suluhisho: Ningekuwa rais ninayeitakia mema nchi yangu ningepiga marufuku televisheni zote hapa nchini kuonyesha michezo ya kandanda ya ulaya ikiwa ni pamoja na kuzizimia signali TV zote zinazofanya biashara ya ukuwadi wa kandanda la ulaya. Hiyo ni kwa sababu njia hizo zinawapumbaza sana wananchi wakidhani kwamba huo ni ustaarabu. Ustaarabu wa kujisahau wewe mwenyewe na kuwatukuza wenzako badala yake!
Mbinu za aina hiyo zilitumika na kuleta mafanikio katika nchi za Urusi, Uchina, Korea na katika baadhi ya nchi za Ulaya Mashariki. Katika Afrika zipo nchi kama Rwanda, ambazo zinakuja juu baada ya kujitambua. Mbali na mafanikio ya kiuchumi, hata kwa kandanda nchi hizo ni tishio kwa sasa, sisi tunakwama wapi?
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau