Bukobawadau

ZITTO NI MWANA CHADEMA AU MWANA MAHAKAMA?

Na Prudence Karugendo
MAHAKAMA  Kuu ya Tanzania,  Kanda ya Dar es salaam,  imeridhia ombi la mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zubeir Zitto (Zitto Kabwe), la kuitaka Kamati Kuu ya chama chake (Chadema) isiujadili uanachama wake hadi kesi yake ya msingi itakapokuwa imesikilizwa na chama hicho.
Kawaida mahakama ikitamka ndio mwisho wa habari “Karti Locuta Causa Finita”, labda kama kesi inapelekwa mahakama ya juu zaidi.
Naomba nieleweke kuwa hapa sipingani na zuio la mahakama, ila nimejiweka katika muonekano ufuatao; kwanza mimi sio Kamati Kuu ya Chadema na wala siongelei uanachama wa Zitto kwa mamlaka ya kusema abaki au aondoke kwenye chama,  kwa maana ya kuvuliwa uanachama, kitu ambacho ni wazi Zitto anakichukulia kama kiama, isipokuwa najaribu kutazama kwa upana na kuyaangalia yaliyojiri kiasi cha kumfanya Zitto atimue mbio na kujisalimisha mikononi mwa mahakama ili ikamkingie kifua.
Penda usipende uamuzi wa mahakama unaheshimiwa na kuzingatiwa. Katika hilo nakumbuka kitu kimoja alichokisema aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Marehemu Francis Nyalali, alipotembelea shule yangu nikiwa kidato cha nne mwanzoni mwa miaka ya 1980. Alikiita kitu hicho kuwa ni maajabu ya mahakama.
Marehemu Nyalali alisema kwamba hata ikitokea jaji akashuhudia mzozo fulani na kujiridhisha kuwa ni upande gani umekosea, kisha mzozo huo ukaletwa mahakamani kama kesi na yeye akapaswa kuisikiliza, jaji huyo hapaswi kuandika hukumu kulingana na alivyoushuhudia yeye mzozo huo isipokuwa kulingana na maelezo yanayotolewa na walio kwenye kesi hiyo. Hata kama yule aliyemshuhudia akitenda makosa ameweza kujieleza vizuri mahakamani,  ndiye hukumu itakayempendelea! Hayo ndiyo Marehemu Nyalali aliyoyaita maajabu ya mahakama.
Kwa hapa maajabu hayo ya mahakama yanajitokeza kwa njia hii: Vyama vya siasa ni taasisi zinazopaswa kuwa na katiba zake kabla ya kukubaliwa, kusajiliwa na kuhalalishwa. Hilo ni jambo linalojulikana kwa kila jaji.
Katiba hizo za vyama vya siasa zinajieleza zenyewe, ndani yake kuna miiko, masharti, maelekezo nakadhalika, ambavyo havitakiwi kukiukwa na yeyote aliyetokea kukubaliana navyo kwa misingi ya kwamba yuko tayari kuviheshimu na kuvilinda kwa moyo wake wote, na hivyo kuwa mwanachama.
Hivyo yeyote anayeiona dosari baadaye katika katiba ya chama chake aliyoahidi kuiheshimu na kuilinda anapaswa aelewe kuwa amejiondoa mwenyewe kwenye chama husika. Hiyo maana yake ni kwamba dosari haimo kwenye katiba ya chama aliyotakiwa kuielewa tangu mwanzo kabla hajaahidi kuilinda, isipokuwa dosari inakuwa kichwani mwake.
Tukirudi upande wa Zitto Kabwe tutaona kwamba yaliyomkuta ndani ya Chadema yote alikubaliana nayo tangu mwanzo wakati anajiunga na chama hicho. Maana mwenendo wake ndani ya chama ulikuwa ukishughulikiwa kwa mujibu wa katiba ya chama aliyoisoma akakubaliana nayo na kuipenda yeye mwenyewe bila msukumo toka kokote kule.
Lakini leo hii, mahakama kwa kuutumia uadhimu wake, inamsikiliza Zitto na kuweka zuio kwa Chadema ili chama hicho kisitekeleze moja ya majukumu yake kwa mujibu wa katiba yake! Kwa mantiki hiyo iko wapi maana ya chama kuwa na katiba yake? Hayo ndiyo maajabu ya mahakama aliyoyasema Jaji Nyalali.
Tukiachana na suala la mahakama tutaona kwamba Zitto ni kijana aliyekuwa anajiamini kupita kiasi ndani ya Chadema, akijiaminisha kuwa anao ufuasi na uungwaji mkono uliopitiliza. Sina hakika kama hilo alilifanyia utafiti wa kutosha.
Sababu ni mtu huyohuyo anayejiaminisha kuwa ana ufuasi wa kupitiliza ndani na nje ya chama, anayekurupuka na kwenda kuiomba mahakama imkingie kifua ndani ya chama chake akiwa ameusahau ufuasi anaojidai nao ndani ya chama hicho!
Je, kitendo cha Zitto kwenda kuiomba mahakama ikizuie chama chake kisifanye moja ya shughuli zake, ambazo ni halali kikatiba, kinamnufaisha nani? Kinakinufaisha chama,  wafuasi wake au yeye binafsi?
Hivi kweli mtu anayekipenda chama chake anaweza akadiriki kukikwaza, akikimwagia kashfa kemkemu, akiwa ameyaangalia tu maslahi yake binafsi?
Kwa namna mambo yalivyo mpaka sasa ni kwamba mahakama imekubaliana na Zitto, inaonekana kakubalika zaidi kwenye mahakama kuliko anavyokubalika Chadema. Kwa mantiki hiyo bado tunayo haki ya kumuita mwana Chadema au yeye ni mwana mahakama? Maana kule ndiko anakokubalika zaidi.
Baadhi ya wananchi wakiwemo wenyeji wa mkoa wa Kigoma wametoa maoni yao kuhusu Kabwe Zubeir Zitto. Wapo wanaosema kwamba mtaji wa chama cha siasa ni watu. Hivyo eti kama Zitto anajiamini anao ufuasi wa kutosha kwenye Chadema ni kitu gani kinamfanya ang’ang’anie kubaki kwenye chama hicho, hata kwa kushikiliwa na mahakama, badala ya kuachana nacho na kuanzisha chama chake ili ufuasi huo alio nao ukamfuate huko?
Mtu mwingine anauliza kwamba kama Zitto anajiona anao ushawishi mwingi ndani ya Chadema kuliko hata Chadema yenyewe eti kwa nini hakuutumia ushawishi huo kupata wabunge wengi ndani ya mkoa wa Kigoma? Sababu eti katika majimbo 8 ya mkoa huo Chadema kinalo jimbo moja tu.
Au eti walau kupata madiwani wengi wa kutosha kuuongoza japo halimashauri moja mkoani Kigoma.
Mtu mwingine anasema kwamba hadi kitongoji cha nyumbani kwao Zitto cha Mwandiga mwenyekiti wake ni wa CCM! Eti atajilinganishaje na watu kama Mbowe, Dk. Slaa, Mnyika, Lema, Musigwa na wengineo ambao majimbo yao yana idadi ya kutosha ya madiwani wa Chadema?
Mmoja watu niliowasiliana nao toka Kigoma anasema kwamba mwaka 2005 jimbo la Kigoma Kaskazini lilipata madiwani 7 wa Chadema, lakini eti idadi hiyo imepungua na kubaki diwani 1 wa Chadema mwaka 2010! Mtu huyo anasema ikifikiriwa vizuri kile ambacho Zitto anadai ni ufuasi kwake kinaweza kikajiweka wazi kuwa si cha kweli. Au eti kama alikuwa nao basi ajue kuwa ufuasi huo umekwisha.
Mtu mwingine wa Kigoma ambaye hakutaka jina lake litokee gazetini,  amesema kwamba alichokifanya Zitto kinaweza kikawa sahihi kwa maana ya kutafuta haki,  ila hakukifanya kwa muda sahihi. Anasema kwamba lengo la Chadema ni kuchukua dola na wala si madalaka na nyadhifa kwa watu binafsi. Kwahiyo eti angevumilia hata kama ni kuvuliwa nyadhifa ndani ya chama na kukisubiri chama kitimize lengo ndipo mengine yafuatie.
Lakini eti tamaa binafsi ya Zitto inaweza ikakiyumbisha chama kikakosa kutimiza malengo yake,  kwahiyo akaishia kukiona chama kinakosa huku naye akiwa amekosa.
Mtu aliyejitambulisha kama msomaji wa Tanzania Daima toka Kusini mwa Tanzania, anasema kwamba jimbo kama Nachingwea ambalo miaka nenda rudi limo mikononi mwa CCM, linao madiwani 4 wa Chadema, lakini jimbo la Zitto, aliyekuwa kiongozi wa chama kitaifa, linaye diwani mmoja tu wa Chadema! Anasema kwamba kama hapo hapatupi la kujifunza basi sote tutakuwa ni vipofu kiakili!
Kwa upande mwingine wapo wanaomlaumu Mheshimiwa Tundu Lissu kwamba alikataa Zitto asijiuzulu na badala yake akataka afukuzwe. Eti hilo lilikuwa kosa la kiufundi maana Zitto angejiuzulu mambo yasingefika hapa yalipo.
Lakini je, kama Zitto angejiuzulu kitendo hicho kingeishawishi Kamati Kuu ya Chadema isiujadili uanachama wake kulingana na usaliti wa wazi anaouonyesha kwenye chama hicho. Je, kujiuzulu kwa Zitto kungemfanya aisahau mahakama kama angeona  Kamati Kuu inataka kumvua uanachama wake kabla hajatimiza alichokikusudia?
Wapenzi wengine wa Chadema wanasema kwamba mambo haya ni bora yangemalizwa kimyakimya pasipo kumwaga mchele kwenye kuku wengi. Ni wazi kwamba wapenzi hao wa Chadema wanasahau kuwa Chadema ilikuwa imeamua kufanya mambo yake kimyakimya ikiufuata utaratibu ulioainishwa kwenye katiba yake.
Isipokuwa mtu mmoja, Kabwe Zubeir Zitto, akaamua kuyaanika wazi mambo ya chama chake kwa kukimbilia mahakamani pale alipoona ukimya wa chama chake unataka kupindisha malengo yake binafsi. Kwa hapa inabidi tumwangalie na kumtambua ni nani aliyemwaga mchele kwenye kuku wengi, ni Chadema au Zitto?
Kadiri haya mambo, “timbwili la Zitto” yanavyosonga mbele ndivyo watu wengi wanavyopata nafasi ya kukielewa zaidi kinachoendelea. Mpaka sasa idadi kubwa ya watu niliowasiliana nao wanasema walivyofunuliwa na kuliona kosa walilokuwa wakilifanya, kosa la kushabikia zaidi mtu badala ya chama.
Wanasema Zitto alikuwepo hata kabla ya Chadema lakini hakuwa na umaarufu wowote na hakujulikana kwa yeyote. Eti umaarufu na anaouita ufuasi kavipata baada ya kuingia Chadema. Kwahiyo wanasema kwamba hata kama wanavutiwa naye ni kwa sababu ya mvuto aliopewa na Chadema.
Kwa maana hiyo, wanasema, Chadema ndiyo yenye mvuto zaidi kutokana na kumvutia hata yeye Zitto na kisha kummegea sehemu ya mvuto huo alio nao, kama kweli bado upo.
Nimalizie kwa kusema kwamba sheria zinazotumika katika utawala zilibuniwa na binadamu na nyingine bado zinabuniwa. Na sheria zinabuniwa au kutungwa ili zikayalinde maadili ya uraia mwema pamoja na uongozi bora.
Lakini hatahivyo zipo sheria zenye ukakasi hapa nchini mwetu. Mfano watu wanamchagua mbunge wao wanayemuona anawafaa, na lazima mbunge atokane na chama cha siasa, mara mbunge anakosana na chama chake nacho kinamvua uanachama, moja kwa moja anapoteza ubunge wake vilevile!
Sheria hiyo ina ukakasi! Sababu mtu kuwa katika chama fulani ni mapenzi yake binafsi, lakini mtu kuwa bungeni ni mapenzi ya wananchi wa sehemu anayotoka na kuiwakilisha. Kwa nini sasa mapenzi yake kwa chama, suala binafsi, yaingiliane au kuchanganywa na mapenzi ya wananchi kwa uwezo wake wa kuwawakilisha?
Hatahivyo sheria hiyo, kwa vile bado ipo, inabidi ifanye kazi. Sitegemei sheria iwepo kama “tisha toto” tu. Mbunge kama anakorofishana na chama chake nacho  kikaamua kumvua uanachama huku yeye akikimbilia mahakamani kuulinda ubunge wake, ingebidi aendeshe kesi akiwa nje ya Bunge sawa na yule ambaye ubunge wake umetenguliwa na mahakama na yeye akaamua kukata rufaa. Huyo hahesabiki kama mbunge mpaka rufaa yake inapopita.
Hatua hiyo ndiyo itaipa meno sheria ya kuvuliwa uanachama ambayo ni sawa na mahakama kuutengua ubunge wa mtu. Sababu kuendelea kuwa Bungeni kwa mbunge asiye na chama, wakati hakuna sheria ya mbunge binafsi, kunamfanya mbunge mhusika aonekane ni mbunge wa mahakama wakati mahakama siyo chama cha siasa wala jimbo la uchaguzi.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau