Bukobawadau

MWENYEKITI CCM ARUSHA : TUMECHOSHWA NA JINSI LOWASSA ANAVYOANDAMWA

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, akiambatana na Mwenyekiti wa Wilaya ya Monduli, Reuben Ole Kuney na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Isaack Joseph ameeleza kuchoshwa na kauli za vitisho zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa chama hicho dhidi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, wakati wanachama wote ni sawa na hakuna mwenye ukubwa mithili ya tembo wa kumtisha mwenzake.

Kauli ya kiongozi huyo, imekuja baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kukemea vitendo vya rushwa kwa watu wanaotaka kuwania urais na kuiagiza Kamati ya Maadili ya chama hicho inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula kuwashughulikia.

Akizungumza katika mkutano wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi katika Kata ya Monduli Mjini ambao pia ulienda sambamba na maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, Nangole alisema wanachama wote wa CCM wana haki sawa na hakuna wa kuogopwa kama tembo, wala mdogo wa kunyanyaswa kama sisimizi, ili mradi hakuna ambaye anavunja sheria na taratibu za chama hicho.

“CCM ni yetu sote, hakuna mtu wa kuogopwa kama tembo wala sisimizi, mimi binafsi sijaona kosa alilofanya Lowassa hadi sasa. Kwa nini wanamfuatafuata na kumshambulia kupitia vyombo vya habari?” alihoji Nangole.

Alisema anawashangaa baadhi ya viongozi kuanza kutoa kauli za kumshambulia Lowassa na kumtishia kumpeleka katika Kamati ya Maadili ya chama hicho kwa tuhuma kuwa, ameanza kampeni za urais, jambo ambalo sio kweli, kwani tangu mwaka 1993 amekuwa akiendesha harambee mbalimbali na amekuwa akifanya sherehe kila mwaka nyumbani kwake.

“Lowassa tangu mwaka 1993/4 alipokuwa waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alianza utaratibu wa harambee kusaidia wazazi waliokuwa na watoto wanaokosa nafasi ya shule na kuanzisha mifuko na alikuwa akienda kanisani na misikitini, iweje leo iwe nongwa?” aliuliza Nangole.
Next Post Previous Post
Bukobawadau